Rais John Magufuli amekataa mapendekezo ya wanavijiji katika Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, ya kutaka wamegewe ardhi katika Pori la Akiba la Selous.
Amewaonya wanasiasa ambao hutumia ghiliba wakati wa kampeni kwa kuahidi kuwa wakichaguliwa watahakikisha wanamega maeneo ya hifadhi na kuwapa wananchi. Rais Magufuli yumo katika ziara ya siku tano mkoani Ruvuma.
Amesema Tanzania ina ardhi kubwa ambayo ikitumiwa vizuri itatosheleza mahitaji ya wananchi, wakiwamo wakulima.
Amesema maeneo ya hifadhi yamekuwapo tangu zama za ukoloni na kuendelezwa na Baba wa Taifa, kwa hiyo hawezi kuua maeneo hayo.
“Suala la shamba, kuchukua hifadhi ya wanyama ili mkalime, lazima niwe mkweli hapa. Lazima niwe mkweli. Nisipokuwa mkweli nitakuwa mnafiki na unafiki ni dhambi.
“Tanzania nzima tangu enzi za Baba wa Taifa [Mwalimu Julius Kambarage Nyerere] kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanyama, kwa ajili ya uvuvi ambako ni ziwani na mitoni na kwa ajili ya wakulima kufanya kazi.
“Maeneo haya yamekuwapo tangu enzi za ukoloni. Maeneo haya yana faida zake. Unapokuwa na wanyama maana yake watu watakuja kutalii kuangalia mbuga zetu – wale ambao wanyama wao waliwamaliza. Wakishakuja huku wanaachia pesa. Ukiwa na mbuga hii ya Selous kwa sababu sasa hivi kuna barabara watalii wataanza kuongezeka. Utajenga ‘guest’ watalalala. Utalima tikiti maji watakuja kula. Utalima mahindi watakuja kula na ndiyo maana sisi kama taifa ni lazima hifadhi za wanyama tuzilinde. “Tusipozilinda watoto na wajukuu watakaokuja watakuwa wanaona tembo kwenye picha tu. Watakuwa wanamwona chui kwenye picha tu. Watamwona swala kwenye picha tu. Tutaanza na sisi kwenda kwenye nchi nyingine kutalii – tukalipe pesa.
“Utalii huu unaleta pesa ambazo zinatusaidia kutengeneza barabara, sasa hatuwezi mbuga zote za nchi hii tukazimaliza kwa sababu ya kulima. Kupanga ni kuchagua na ndiyo maana nimewaeleza wenzenu kule nimewakuta wako katikati ya pori la Selous wanasema: ‘Mazao yetu yanaliwa na tembo.’
“Nikawambia: ‘Ninyi ndiyo mmewachokoza tembo kwa sababu hivi vilikuwa vituo vya wanyamapori.’ Wale wafanyakazi wakaanza kuzaa, wakaleta ndugu zao mwishowe wakaanza kulima mahindi, baadaye wanalima…lile ni eneo la tembo. Tembo akipita pale atakula tu kwa sababu ndilo eneo lake.
“Kwa hiyo saa nyingine tunawachokoza tembo; na tembo hawawezi wakaja kwangu kulalamika kwa sababu hawazungumzi. Wao wanafanya vitendo kwa kula mazao yetu. Mmenielewa ndugu zangu?
“Kwa hiyo hilo eneo ambalo lipo kwa ajili ya hifadhi mimi siwezi nikaliachia. Nawaachia halmashauri,” amesema Rais Magufuli.
Msimamo huu wa Rais Magufuli unaleta mwanga wa uhifadhi nchini kwani unaonekana kuainisha bayana msimamo wa sasa wa serikali, tofauti kidogo na ule alioutoa Januari 15, mwaka huu.
Kwenye tamko la tarehe hiyo, alizuia wavamizi kuondolewa maeneo yaliyohifadhiwa kisheria. Aliagiza wataalamu/viongozi wa wizara wadau wa uhifadhi wayatambue maeneo yote yaliyovamiwa na kuanzishwa vijiji 366 yarasimishwe kwa ajili ya shughuli za kibinadamu.
Aliagiza maeneo ya wanyamapori na misitu yasiyo na rasilimali hiyo yagawiwe kwa wafugaji na wakulima, na akataka sheria ya vyanzo vya maji iangaliwe ili kutowazuia wananchi wanaozalisha mazao kando kando ya mito. Sheria ya sasa inazuia shughuli za kilimo na ujenzi ndani ya eneo la mita 60 kutoka chanzo cha maji.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli ilipokewa kwa mitazamo tofauti huku baadhi ya wananchi wakiamua kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria na kuanza kujitwalia ardhi. Hali hiyo ilisababisha Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa nyakati tofauti kukemea wavamizi hao kwa maelezo kuwa rais hakuagiza kufanyike uvamizi.
Septemba 1961, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitoa ilani iliyokuja kujulikana kama ‘Ilani ya Arusha’ kuhusu uhifadhi.
Alisema: “Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi si tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.
“Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.
“Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri si tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”