Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi na waumini wa madhehebu ya dini nchini kujiepusha na migogoro ambayo imekuwa ikiharibu sifa na heshima ya taasisi hizo muhimu katika jamii.

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito huo leo tarehe 04 Februari, 2018 mara baada ya kuhudhuria Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu wa Tano wa Dayosisi ya Dar es Salaam Baba Askofu Jackson Sosthenes Jackson katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano Upanga.

Mhe. Rais Magufuli amesema viongozi wa Serikali husikitishwa na uwepo wa migogoro katika madhehebu ya dini, na hupata mashaka kama kweli viongozi wa madhehebu husika wanazingatia matakwa ya uchungaji.

Amempongeza Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Jacob Chimeledya kwa kuumaliza mgogoro uliokuwa ukilikabili Kanisa hilo na hatimaye kufikia hatua ya kumweka wakfu Baba Askofu Jackson Sosthenes Jackson kuwa Askofu wa Tano wa Dayosisi ya Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Baba Askofu Jackson Sosthenes Jackson kuwa Askofu wa wote, kuvunja makundi yaliyokuwepo katika Dayosisi hiyo, kutolipiza kisasi na kusamehe yote yaliyopita na badala yake ajenge Dayosisi imara na aongoze kwa haki na upendo kwa wote.

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia viongozi wa Kanisa la Anglikana Tanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kushirikiana na kanisa hilo na madhehebu mengine ya dini katika shughuli zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za kijamii kama vile hospitali, na shule.

Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson Mwansasu, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa na Mkewe Mhe. Mama Anna Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba.

 

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

04 Februari, 2018