Wakati wa kudai Uhuru, wapo Waafrika waliodhani mapambano yale yasingefanikishwa na Waafrika.
Waafrika shupavu kwa pamoja na Wazungu na Waasia wachache walipounganisha nguvu kuutokomeza ukoloni, bado kukawapo watu walionekana kutofurahishwa na hatua ya kujitawala!
Kwa kutofurahishwa huko, wakaamua kuwa vibaraka wa maadui wa ndani na nje ya nchi yetu.
Hostoria inabainisha wazi kuwa kuna Watanganyika (wakati huo) waliochukizwa na kitendo cha Tanganyika kupata Uhuru! Hao walitamani waendelee kuwa chini ya utawala wa wakoloni, hata kama kwa utawala huo walikuwa wakikosa heshima na usawa kama binadamu wengine.
Wapo Waafrika waliopinga kujitawala kwa sababu waliamini chini ya utawala wa weusi wenzao wasingeweza kufika kokote kimaendeleo. Hawa ni wale walioamini kuwa Mzungu ni ‘mungu’’. Waliamini Mwafrika amezaliwa kumtumikia Mzungu! Haishangazi hadi leo kuwasikia watu wakisema: “Ana akili kama Mzungu!” “Jamaa anazingatia muda kama Mzungu!” Alimradi kuna mambo mengi ya kuutukuza uzungu.
Tunachojifunza hapa ni kwamba binadamu wamekuwa wagumu kuyapokea na kuyakubali mabadiliko mara moja.
Kwenye safu hii nimewahi kuhoji swali hili: “Lini maisha yalikuwa rahisi?” Sikupata majibu.
Niliuliza swali hili nikirejea kauli za mitaani kwamba uongozi wa Rais John Magufuli, umesababisha maisha ya Watanzania yawe magumu.
Wale walioonja maisha ya awamu zote tano za uongozi wa Taifa letu, watakubali kuwa kilio hiki cha maisha magumu kimekuwapo kwa awamu zote.
Kuna jambo moja muhimu kwenye awamu zote hizi nne-nalo ni kwamba malalamiko ya wananchi kuhusu ugumu wa maisha yamekuwa hayakosekani. Hakuna awamu ambayo kilio hiki hakikusikika.
Namba 66 ni 66 kwa upande ulipo. Namba hiyo kwa mwingine ni 99! Ni kwa sababu hiyo haitarajiwi kuwasikia wale waliozoea pepo ya ukwepaji kodi wakiisifu Serikali hii.
Ugumu wa maisha wa leo unaweza kuwa tofauti na awamu zilizopita. Sijui ni wangapi-hasa hawa vijana wa kizazi cha bodaboda- wanaotambua kuwa enzi zile aliyeonekana kutumia pikipiki, ama alikuwa padri, katibu tarafa, au tajiri.
Sijui ni wangapi wanakumbuka kuwa redio zilikuwa chache kiasi kwamba wenye nazo kijijini walikuwa radhi kuwapokea wanakijiji jioni kusikiliza taarifa ya habari au kusikiliza hotuba ya kiongozi wa kitaifa!
Lakini ni wakati huo ambao wanafunzi walisomeshwa bure kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu. Ni wakati ambao huduma za maji zilitolewa bure; na wagonjwa hospitalini walitibiwa bure na wakapewa chakula bure!
Zama hizo ni tofauti na sasa. Wakati pikipiki zamani ilionekana kifaa maalumu kwa watu maalumu, leo kijana anaweza kuamka akaenda dukani na kurejea na pikipiki yake nyumbani.
Leo Mtanzania kuezeka kwa kutumia mabati si jambo la anasa wala la kushangaza, lakini zamani nyumba za bati zilikuwa ni kwa watu wachache na ofisi za umma! Sasa sijui tafsiri halisi ya maisha magumu au mepesi inapatikana kwa vigezo vipi. Lakini lililo wazi ni kuwa kwa awamu zote, waliofanya kazi halali walifanikiwa na kuwa na maisha mazuri kuliko wale ambao hawakupenda kufanya kazi.
Awamu ya Tano imeingia madarakani kwa staili nyingine. Wale wanaotaka Rais Magufuli, aongoze kwa kufuata mifumo au staili zilizotumiwa na watangulizi wake, hawamtendei haki.
Malalamiko mengi ya ugumu wa maisha yanayoendelea sasa yanaashiria kuwa nchi hii ilishafika mahali sheria na kanuni vilitupwa kabisa.
Miongoni mwa vilio vya sasa ni kodi. Kosa la Rais Magufuli, na Serikali yake ni la kusimamia ukusanyaji na matumizi ya kodi! Hilo ndilo kosa lake! Kama kweli hii ndiyo sababu inayotumiwa kumsakama, nadhani si kumtendea haki.
Ukwepaji kodi katika Serikali yoyote makini ni jambo linalopigwa vita. Wananchi wanataka huduma za kijamii- wanataka maji safi na salama, wanahitaji matibabu, wanahitaji walindwe ili waishi kwa raha mstarehe! Watumishi wa umma, si tu wanataka mishahara minono, bali hata hiyo midogo waipate kwa muda unaostahili. Nchi inahitaji miundombinu ya barabara, reli, umeme, usafiri wa anga n.k.
Wanafunzi wanataka wapate madawati, shule na vyuo vitosheleze mahitaji, wataalamu walipwe vizuri n.k. Haya yote hayatawezekana kwa hisia. Yanawezekana kwa Watanzania kuchapa kazi, kulipa kodi; na kusimamia matumizi ya fedha za umma.
Mwalimu Nyerere alishasema wazi kuwa serikali ya wala rushwa haikusanyi kodi. Rais Magufuli, mapema kabisa akiomba ridhaa ya kuongoza Taifa letu aliapa kupambana na wakwepa kodi. Kama ilivyo ada, Watanzania waliomsikia walijua ni yale yale ya miaka yote!
Wanasiasa kadhaa kwa kutaka kujijengea uhalali wa kisiasa wameamua kuupotosha umma kuhusu suala hili la ‘maisha magumu’. Wanasema nchi inayumba, na kigezo wanachotumia ni cha watu kubanwa kulipa kodi!
Watanzania ni waelewa. Wiki iliyopita mamia kwa mamia ya wananchi walijitokeza kulipa kodi mbalimbali. Niliwasikia Watangazaji runinga wakistaajabu umati mkubwa wa walipakodi. Hata TRA nako kuna watumishi walishangaa mwitikio wa watu.
Kulipa kodi ni thawabu. Nilidhani wanasiasa wangeandaa hoja ya kumshambulia Rais Magufuli, miezi kadhaa ijayo kwa kuhoji matumizi ya kodi inayolipwa na wananchi; lakini si kumshambulia kwa kukusanya kodi.
Wanaomshambulia wanatumia kigezo cha Bandari kukosa meli kuwa ni matokeo ya uongozi wake. Kwa maneno mengine wanataka Bandari ijae meli zenye bidhaa zisizolipiwa ushuru wala kodi. Kuna faida gani ya kuwa na meli 50 zisizolipa kodi kuliko kuwa na meli 20 zinazolipa kodi stahiki?
Wapo wanaomtisha kwa kusema msimamo wake kwenye kodi utasababisha wawekezaji wakimbie! Hapa huhitaji akili kutambua kuwa kumbe Tanzania ilikuwa pepo ya wakwepa kodi, na kwa maana hiyo kuna mawakala wa hawa manabii wa ubepari wanaowatetea wawekezaji wezi waendelee kufaidi pepo hiyo.
Mataifa yaliyoendelea ukwepaji kodi, si tu ni kosa, bali ni fedheha kwa anayekwepa kodi. Kwa mataifa makubwa yanayosisitiza wananchi kulipa kodi hayawezi kusimama kuilaani Serikali ya Rais Magufuli. Lakini kwa kuwa mataifa makubwa yana sera zinazotekelezwa na wezi waliopachikwa jina zuri la “wawekezaji”, haitashanga wakipandikiza vibaraka wao wa ndani na nje ili waendelee kuupotosha umma kuhusu uhalali na faida za ulipaji kodi.
Huwezi kuzungumza masuala haya ya maendeleo bila kufanya rejea kwa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alisema haya ambayo kiongozi makini kama Rais Magufuli, ndimo anamopita.
Mwalimu alisema: “Kama nilivyowaambieni kwamba, kazi ya utajiri ni kuondoa dhiki, kazi ya mali ni kuondoa dhiki. Lakini serikali yetu inapotaka kupata fedha kidogo za kuondolea dhiki, na matajiri wa Tanzania ndiyo wenye fedha, Serikali yetu haiwaombi. Hivi huwaomba hawa? Hatuwaombi. Tunawatoza kodi. Uende uwaombe matajiri, unapita unawaomba matajiri, watakubali? Wanapigwa kodi; wapende wasipende wanatozwa kodi, asiyelipa tunamtia ndani.
“Njia peke yake duniani ya kuvamia mali ya matajiri, isaidie kuondoa dhiki, ni kuwatoza kodi. Hakuna njia nyingine. Kama mali yenyewe mmewaachia mpaka wakawa nayo, wanatozwa kodi; hawaombwi. Kuomba unaomba zaka! Lakini unaweza kuendesha nchi kwa zaka ya Jumapili? Ile zaka ya Jumapili ni ile ya makanisani ambako mtu anapitisha bakuli. Sasa, waheshimiwa, mwingine ataweka shilingi moja, mwingine senti hamsini. Tajiri, pengine jizi, hilo hutumbukiza arobaini, linafurahi lenyewe, linakwenda nyumbani linajitapa, ‘Leo nimeweka shilingi arobaini katika sahani kanisani!’
“Yote hiyo anayafanya ili aseme vizuri na masheikh na mapadri, nao wataanza kumtetea kwa sababu kajenga msikiti au kanisa. Na umaskini bado upo, bado uko hapa na pote duniani. Na misikitini wanapokea zaka zao zile kila siku, haziishi. Jumapili, leo, tumetoa; na umaskini bado uko pale pale. Umaskini hauondoki kwa zaka za Jumapili; umaskini unatolewa kwa kodi, au kwa kila mtu kufanya kazi.
“Lakini dunia haina Serikali, Serikali itakayowatoza matajiri; rafiki zangu Marekani watozwe kikodi kidogo, Waingereza, Wajerumani, Warusi na matajiri wengine duniani wapigwepigwe vikodi kidogo, nchi ambazo ni maskini zenye dhiki ziweze kusaidiwa. Eti tunategemea zaka, zaka; zaka za matajiri! Tunatengeneza mpango wetu, mpango wetu wa miaka mitano, kumbe ni mpango wa zaka!
“Basi wananchi nasema kwa sababu hiyo tunafanya makosa. Tunafanya makosa kwa nini? Kwa sababu hatuwezi kuzipata fedha za matajiri. Tunajidanganya kwamba tutapata pesa za matajiri, kwa kudhani watakuja wanazitoa tu. Au tunapokuwa hatufikirii zaka za Serikali tunafikiria za wale matajiri, kwamba eti makampuni yatakuja yataanzisha viwanda, bora tuseme nao vizuri tu!”
Kwenye Kitabu cha Warumi, tunasoma maneno haya: 1 Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. 2 Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe, 3 Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu; 4 maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kutoa adhabu. Yeye ni mtumishi wa Mungu na huitekeleza ghadhabu ya Mungu kwao watendao maovu. 5 Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo. 6 Kwa sababu hiyohiyo ninyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao. 7 Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima.
Kama kweli tunataka kuiona Tanzania mpya, kwa hili la kodi hatuna namna isipokuwa kumuunga mkono na kumheshimu Rais Magufuli na Serikali yake. Tunachopaswa kujiandaa kuhoji ni hayo matokeo ya hizo kodi zinazolipwa sasa, basi.