Juhudi zinafanywa na watu mbalimbali kumkwamisha Rais John Magufuli.

Tukio lililoibua gumzo kubwa nchini ni la uhaba wa sukari unaodaiwa kusababishwa na hujuma za baadhi ya wafanyabiashara wakubwa nchini.

Tusingependa kuwa sehemu ya mgongano huu, lakini lililo wazi ni kwamba uamuzi wa Rais Magufuli, wa kudhibiti uagizaji sukari kutoka nje ulikuwa na nia njema kwa viwanda na wakulima wa Tanzania.

Nia hiyo ililenga kudhibiti bidhaa hiyo kutoka nje ili wakulima wetu walime zaidi; viwanda vizalishe zaidi na kwa maana hiyo visaidie kuongeza ajira kwa maelfu ya vijana wanaotaabika.

Kinyume cha nia hiyo njema ya Rais Magufuli, kumejitokeza ‘mshikamano’ unaodaiwa kufanywa na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa kuficha bidhaa hiyo ili iadimike, na kwa sababu hiyo waruhusiwe kuingiza sukari kutoka nje.

Tayari Rais Magufuli ametangaza uamuzi wa kuitwaa sukari itakayobainika kufichwa katika maghala. Kwa uamuzi huo, bila shaka wapo watakaoumia.

Rai yetu kwa wafanyabiashara ni kuwaomba wajitahidi kusoma alama za nyakati ili watambue kuwa zama hizi si zile za wafanyabiashara kuwa na sauti na nguvu ya kufanya mambo hata kama ni kwa kuvunja sheria.

Ni ukweli ulio wazi kuwa sukari imekuwa mwanya mkubwa katika mianya mingi ya ukwepaji kodi nchini mwetu. Katika mazingira ya aina hiyo, na kwa kuzingatia msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuziba mianya ya rushwa na kusimamia ulipaji kodi, ni wazi kuwa bado Rais Magufuli ataungwa mkono na wananchi walio wengi kwa hatua zozote atakazochukua.

Kama kwa miaka mingi wafanyabiashara walizoea kufanya kadiri walivyotaka bila kubughudhiwa, watambue kuwa zama hizi ni tofauti. Endapo watafuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, bila shaka Tanzania itakuwa mahali pazuri pa kila mfanyabiashara kuendesha shughuli zake kwa amani.

Lakini jambo jingine lililo muhimu kwenye tukio hili la sukari, ni ile dhana ya Serikali kutojisahau au kutobweteka na kuamini kuwa sekta binafsi inapaswa kuachiwa kila kitu ikiendeshe. Hili la sukari ni salamu kwa Serikali kuwa inapaswa kuwa na miundombinu imara katika kila nyanja ili kukabiliana na tishio linaloweza kuletwa na sekta binafsi.

Leo wanaweza kuwa ni waagiza sukari, lakini kesho wanaweza kuwa wasafirishaji. Ndiyo maana tunasisitiza kujengwa kwa miundombinu kama reli ili muda wote Serikali iwe na hakika ya kuendelea kuwahudumia wananchi bila kutetereka.

Tunatoa rai kwa wafanyabiashara kujiepusha na aina zote za hujuma kwa Serikali hii ambayo inajitahidi kurejesha nidhamu katika masuala mbalimbali, yakiwamo ya mwanya wa ukwepaji kodi katika uagizaji bidhaa kutoka nje.