Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kufuatia watu 11 kupoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Nyangozi, Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera.
Ajali hii imetokea jana tarehe 14 Januari, 2018 majira ya saa 11 jioni baada ya basi dogo la abiria aina ya Nissan Caravan lililokuwa likitoka Kakonko Mkoani Kigoma kuelekea Kahama Mkoani Shinyanga kuligonga ubavuni lori la mizigo kisha kugongana uso kwa uso na lori jingine na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine 6 kujeruhiwa.
Mhe. Rais Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Watanzania hao na amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kumfikishia pole kwa familia za Marehemu wote, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimehuzunishwa na kusikitishwa sana na vifo hivi, nawapa pole wafiwa wote, ninawaombea marehemu wapumzike mahali pema na majeruhi wapone haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na ameviagiza vyombo vinavyohusika kuongeza jitihada za kukabiliana na ajali za barabarani ili kuokoa maisha ya watu na mali zinazopotea kutokana na ajali.