2Wiki iliyopita vyombo vya habari vimetangaza habari nyingi za kukamatwa, kusafirishwa, kushikiliwa polisi, kufunguliwa kesi mahakamani, kesi kuendelea hadi saa 3:00 usiku na kisha Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kujidhamini. Binafsi sina nia ya kurejea matamshi ya Lissu, lakini nitaangalia nguvu kubwa inayotumiwa na dola kumdhibiti Lissu.

Kabla sijaendelea kudadavua suala la jinsi gani Rais Magufuli anamjenga Lissu, naomba uniruhusu msomaji wangu nitumie mfano wa uwindaji porini kwa kuulinganisha na uchaguzi mkuu. Simba ni mfalme wa pori. Katika kila mawindo, iwe chui, tembo au mnyama yeyote awaye anakuwa macho na simba, ila hata simba huwa anakuwa macho na baadhi ya wanyama kama mbwa mwitu.

Mfano huu nautoa kwa kukumbuka filamu niliyoiona kwenye idhaa ya Discovery World. Katika filamu hii, simba aliua pundamilia. Kama kawaida yake kwa kuogopwa na wanyama wengine, akakaa akaanza kutafuna nyama. Amekula hadi akasinzia. Mbwa mwitu wakamkuta simba amelala, wakadhani naye amekufa. Walipomtia jino moja tu, akaamka na kuwafukuzia mbali.

Kwa kawaida katika hatua kama hii, simba hufahamu hatari inayomnyemelea, huachana na mzoga akaenda zake, kwa maana kwamba siku inayofuata atarejea mawindoni. Kwa bahati mbaya, simba huyu alikuwa mbabe. Mbwa mwitu walikuwa na njaa ya kufa mtu. Pamoja na kwamba simba huyu ameshiba, badala ya kuwaachia mzoga wakaendelea kuburudisha mioyo yao, yeye akaendelea kuwatisha.

Alifanikiwa kufanya hivyo mara nne. Kama wamepagawa vile, mbwa mwitu wale walimzukia simba kama nyuki waliotoka kwenye mzinga. Kilichofuata ni historia. Mbwa mwitu wale walimla simba, wakamaliza wakala na mzoga aliokuwa anauzuia wasiule. Kama hujapata kuiona filamu hii ingia kwenye you tube ipo, utabaki kinywa wazi.

Sitanii, hamisha mfano huu wa mbwa mwitu na simba kwenye uwanja wa uchaguzi. Chama kinachoshinda uchaguzi kinakuwa sawa na simba aliyeua pundamilia. Kinayo nafasi ya kujenga mwili wake, kwa kuwa cha kwanza kula kikashiba na kikaweka utaratibu mzuri wa kuwinda siku inayofuata (uchaguzi ujao). Ikiwa chama hiki kitafanya ubabe sawa na simba niliyemtaja hapo juu, mbwa mwitu (yaani vyama vya upinzani) vinaweza kukivamia kama nyuki, vikakila chama hicho na mzoga kinaoulinda (vikashinda uchaguzi kwa huruma ya wananchi).

Ni katika hatua hii, Rais John Pombe Magufuli ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi mwaka 2020 tutakapofanya uchaguzi mwingine. Hata ikitokea mtu akapiga kelele kiasi gani, hakuna mwenye uwezo wa kumnyang’anya ushindi huo Rais Magufuli. Hapa nakubaliana na Rais (mstaafu), Jakaya Kikwete kuwa kelele za mlango, hazimzuii mwenye nyumba kulala.

Hata hivyo, ikiwa CCM kitatumia nguvu kubwa na hasa vyombo vya dola kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, mfano wa simba utakuwa jirani. Ikiwa polisi wamefikia hatua ya kutangaza kuwa wanawasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuangalia uwezekano wa kumfugia Lissu simu zake kwenye mitandao, nadhani wanatengeneza joto la kisiasa lisilo la lazima.

Sitanii, Lissu ni mwanasheri mzuri. Anafahamu anachofanya. Polisi naamini wanao wanasheria, lakini wakiendelea na mkondo huu wa kukamata wapinzani na kuwafungulia kesi, kama dhana ni kufikiri kuwa wanawaogopesha, wataishia kuwajengea usugu na kuwafanya wananchi wawaamini. Wananchi wakiwaamini, Serikali itafanya kazi sawa na wakoloni kutumia nguvu kunyamazisha sauti bila mafanikio.

Narudia, katika hili niliamini na naendelea kuamini kuwa Rais Magufuli alianza vyema kwa kuondoa uozo katika jamii (operesheni tumbua majipu). Wapinzani katika mikutano ya hadhara wanazungumza uozo unaofanywa na baadhi ya watendaji serikalini kama inavyoripotiwa na Msimamizi na Mkaguziu Mkuu wa Serikali (CAG). Nguvu inayotumika kuzuia mikutano, hapana shaka inalenga kunyamazisha hao wanaoonyesha ufisadi ulipo.

Si nia yangu kuandika mengi leo, ila Rais Magufuli unao uwezo wa kuwinda pundamilia wengi leo, kesho na kesho kutwa ukawaacha hawa wenye kuvamia mizoga, wakatafuna angalau mfupa nao wakajenga uwezo wao wa kuwida kwani wapo kisheria. Kuendelea kuwazuia sawa na polisi wanavyofanya kwa Lissu, wanawajengea usugu na wakiungana kama wale mbwa mwitu, watakula simba na mzoga anaoulinda. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika na tudumishe amani yetu. Tafakari, chukua hatua.