Wiki iliyopita, Rais John Mafuguli alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam. Kati ya vitu alivyovikuta ni pamoja na makontena 20 ya mchanga unaopelekwa nje ya nchi kuchenjuliwa. Baadaye idadi ya makontena iliongezeka kufikia 263. Makontena hayo yanamilikiwa na migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, inayomilikiwa na kampuni ya Acacia.

 

Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) umesema kiwango cha madini ya dhahabu kilichopo katika mchango huo uliopo kwenye makontena ni asilimia 0.02, shaba ni kati ya asilimia 17 na 20 na fedha ni asilimia 0.02. 

 

Kampuni ya Acacia imesema kuwa makontena hayo kushikiliwa inapata hasara ya Sh bilioni 40 kila wiki.

Rais Magufuli akiwa bandarini, alisema taratibu zifanywe makontena hayo ikibidi yafunguliwe na kuchunguzwa kwa uwazi dunia na Watanzania wajue kilichomo. Sisi tunapenda kusema bayana kuwa tunaunga mkono msimamo wa Rais Magufuli katika suala hili la kuzuia mchanga kwenda nje ya nchi.

 

Hatua ya Acacia kutangaza kuwa inapata hasara ya Sh bilioni 40 kwa kila wiki unaposhikiliwa mchanga huo, imeongeza wasiwasi tuliokuwa nao. Kiwango cha madini kinachotajwa kuwamo kwenye mchanga, kinatutia shaka kama kinahalalisha Acacia kusafirisha mchanga huo kutoka Tanzania kwenda Japan. Gharama za kusafirisha mchanga huo tunadhani ni kubwa kuliko thamani ya madini inayoelezwa kuwamo kwenye mchanga.

 

Muda mrefu tumekuwa na wasiwasi kuwa huenda kampuni hii na nyingine zinaingiza madonge ya dhahabu na madini mengine kwenye makontena haya na kudai kuwa ni mchanga. Kampuni hizi, kama zinapata ujasiri wa kudai zinapata hasara hapa nchini badaye zikabainika zinapata faida kwenye masoko ya hisa ya kimataifa zikapigwa faini ya Sh bilioni 90 zikalipa, hatuna sababu ya kuziamini kuwa kwenye makontena kuna mchanga kweli.

 

Pia kama zina nia ya dhati tangu mwaka 1998 zilipoanza kusafirisha mchanga nje ya nchi iwapo zina mpango wa kuendeleza uchumi wa nchi yetu, zingekwishajenga kiwanda cha kuchenjua mchanga hapa nchini. Umbea kwamba kujenga kiwanda ni gharama kubwa unaacha maswali mengi kuliko majibu.

 

Tunapenda kusisitiza kuwa tunaungana na Rais Magufuli kutaka uchunguzi huru. Hata kama nchi itaingia gharama kuleta wataalamu wa kimataifa wakashirikiana na wazalendo kupima angalau makontena 50 kati ya 263 tujiridhishe iwapo wanachodai ni mchanga kuwa ni ‘mchanga kweli’. 

Tukikuta ni mchanga tuwaombe radhi, tukikuta ni dhahabu tuwadai gharama halisi kwa mali watakayokuwa wametuibia tangu mwaka 2008. Mungu ibariki Tanzania.