Hatua ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwafutia mashitaka ya ujangili watu tisa, wakiwamo wenye nasaba na Mbunge wa Mbarali, Haroon Mulla; imeibua ‘kilio’ miongoni mwa watu walio katika mapambano dhidi ya ujangili nchini.
Kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao kunaelezwa kuwa ni jaribio kubwa kwa uongozi wa Rais John Magufuli, ambaye ameapa kupambana na vitendo vya ujangili ili kulinda wanyamapori.
Wiki iliyopita, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, ililazimika kufuta kesi dhidi ya watu hao waliokutwa na bunduki 17 baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha maombi ya kufutwa kwa kesi hiyo.
Kwa uamuzi huo, watuhumiwa wote waliachiwa huru na kukabidhiwa bunduki zao ambazo awali zilidaiwa kutumika kwenye mauaji ya wanyamapori, wakiwamo tembo 86.
Waliofutiwa mashitaka ni Mikidadi Mwazembe (55), Shahgol Mulla (42), Pirmohamed Mulla (25) na Fahad Pirmohamed (31).
Wengine ni Sylvester Lugolo (28), Mazar Gamdust (50), Abdulsamad Abdala (22), Shahdad Mulla (42) na Juma Msagati (23). Wote ni wakazi wa Mbarali mkoani Mbeya.
Hivi karibuni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Pirmohamed Mulla alikamatwa na nyara za Serikali zikiwamo pembe za tembo na kupandishwa kizimbani.
Alitiwa hatiani na kuhukumiwa kwenda jela miaka 20 au kulipa faini ya Sh milioni 138.390. Mshitakiwa huyo alilipa kiasi hicho cha fedha na kuachiwa huru. Katika mashitaka mengine, jangili Pirmohamed Mulla na wenzake wanane, walifunguliwa mashitaka mengine ya uhujumu uchumi, lakini Ofisi ya DPP kwa kushirikiana na Polisi, wakaamua kufuta mashitaka hayo.
Habari kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na kikosi kazi kilichoundwa kupambana na ujangili, zinasema hatua hiyo imewavunja moyo watu waliojitoa uhai wao kuwalinda wanyamapori.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani. Upande wa mashitaka ambao ni Jamhuri uliamua kuondoa mashitaka dhidi ya washitakiwa wote.
Awali, washitakiwa hao walisomewa mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, wakituhumiwa kuua wanyamapori bila kuwa na vibali halali vya Serikali.
Katika uamuzi wa Mahakama Kuu, Jaji Dk. Adam Mambi aliwaachia huru, akisema kesi yao isingeendelea kwa kuwa upande wa mashitaka uliamua kuondoa shauri hilo mahakamani.
Alisema washitakiwa hao katika kesi yao iliyokuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa, walikuwa wakishitakiwa kwa tuhuma za uhujumu uchumi, na kwamba wameachiwa kwa kutekeleza matakwa ya kifungu 91 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
“Upande wa mashitaka ambao ni Jamhuri, ulifuta mashitaka yao katika Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, hivyo kutokana na kufutwa huko, Mahakama Kuu hatuwezi kuendelea kusikiliza mashitaka yaliyofutwa, hivyo na sisi tunayafuta kwa mujibu wa sheria,” alisema jaji huyo.
Mashitaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, yalifutwa na Hakimu Atughanile Ngwala baada ya upande wa mashitaka kuamua kufuta mashitaka.
Katika kesi hiyo namba 6/2016 iliyofunguliwa Novemba 10, mwaka huu, washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na kesi mbili za uhujumu uchumi kupitia uwindaji haramu wa wanyamapori.
Waendesha Mashitaka wa Serikali – Basil Namkambe na Hebel Kihaka – waliieleza Mahakama kuwa washitakiwa kwa pamoja walitenda kosa la kuwinda na kuua wanyamapori waliokatazwa.
Kihaka aliiambia Mahakama kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Agosti 2006 na Septemba 2014 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Morogoro na Iringa ambako wanadaiwa kuwinda na kuua tembo 86 na wanyama wengine.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, aliwataka washitakiwa wote kurudishwa rumande hadi Novemba 17 kesi itakapoanza kusikilizwa.
Novemba 17, mwaka huu kesi hiyo iliitwa tena mahakamani hapo na ndipo ilipofutwa kwa kile kilichoelezwa kuwa upande wa Jamhuri uliomba iondolewe kutokana na upelelezi wake kutokamilika na kwamba ungechukua muda mrefu.
Pia wanafamilia hao wanadaiwa kukutwa na bunduki 17 zinazosadikika kutumika katika matukio mbalimbali ya ujangili katika Hifadhi za Taifa. Bunduki hizo zilikamatwa katika makazi ya wanaukoo wa Mulla.
Mapya yaibuka
Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii waliozungumza na JAMHURI kwa masharti ya kutotajwa majina, wamesema mtuhumiwa mmoja kati ya hao anamiliki bunduki saba.
“Bunduki kadhaa walizokutwa nazo zipo zilizonunuliwa madukani, lakini kuna nyingine zimetoka katika vituo vya polisi nchini,” anasema mtoa taarifa wetu.
Hadi sasa mtu mmoja aliyesaidia kikosi kazi kupata taarifa za ujangili za watuhumiwa hao hajulikani aliko, akidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
“Huyu mtu ndiye aliyewezesha kukamatwa kwa hawa watuhumiwa, ametoa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kueleza idadi ya wanyama waliouawa kwani naye alikuwa akihusika. Alikisaidia kikosi kazi, akiwa njiani kwenda Dar es Salaam ametoweka na hajulikani alipo. Ingawa zipo taarifa kwamba ndugu yake mmoja amehusika katika njama za kumpoteza,” anasema mtoa taarifa.
Maofisa kadhaa wa Jeshi la Polisi walio kazini na wengine waliostaafu, wanadaiwa kuwa kwenye mpango madhubuti uliofanikisha kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao.
Mmoja wa wasiri wa JAMHURI amesema kitendo cha kuwaachia watuhumiwa hao wa ujangili, ni mkakati wa kukwamisha juhudi za kupambana na ujangili ambazo zimeanza kuonesha mafanikio.
Amesema haiwezekani kesi za aina hiyo zifutwe katika mazingira yasiyoeleweka kwa kisingizio cha kutokamilika kwa ushahidi, huku watuhumiwa wakiwa wamekamatwa na ushahidi ukionesha wazi kuhusika kwao.
“Rais awe mkali, la sivyo atajikuta hawezi kupambana katika vita hii. Mtandao huu ni mkubwa unaohitaji mapambano ya kweli kwani watu wa aina hii wana pesa na wapo tayari kwa lolote,” anasema mtoa taarifa wetu.
Taarifa za uhakika ambazo JAMHURI imezipata zinaonesha kuwa kuachiwa kwa watuhumiwa wa ujangili ni matokeo ya kufanikiwa kwa mtandao mkubwa unaowahusisha baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi, maofisa katika ofisi ya DPP, wanasiasa na watu mbalimbali wenye ushawishi.
Mmoja wa watu wanaotajwa ni aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC) ambaye alihamishiwa katika moja ya miji mikubwa nchini, na kwa sasa amestaafu.
“Huyu anajua mtandao wa ujangili unavyofanya kazi. Alikuwa karibu na majangili wengi, na hata alipoondoka Mbeya alihakikisha anarithisha uhusiano huo kwa waliompokea ofisi.
“Majangili wakikamatwa wanampigia simu, na yeye anatumia nafasi yake kama mmoja wa wastaafu kuzungumza na ‘vijana’ wake kuweka mambo sawa. Kufutwa kwa kesi nyingi za ujangili na dawa za kulevya ni matokeo ya mtandao huo kuanzia Polisi Makao Mkuu, Ofisi ya DPP na hata kwenye ngazi ya wale walio na nguvu au ushawishi kwenye kikosi kazi,” kimesema chanzo chetu.
JAMHURI imepewa majina ya maofisa hao wanaotajwa kushirikiana na majangili, na kwa sasa inaendelea kuhifadhi majina hayo.
JAMHURI imewasiliana na Mwanasheria Ofisi ya DPP, aliyekuwa katika kikosi kazi mkoani Mbeya, Paul Kadushe, ili kuweza kupata ufafanuzi kuhusu kufutwa kwa kesi hiyo.
Amethibitisha kuwa ni kweli kesi imefutwa, lakini mwenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni Mwanasheria wa Mkoa.
“Mimi nilikuwapo awamu wa kwanza alipokamatwa Pirmohamed ambaye ni mtoto wa mbunge, tukamfungulia mashitaka, Mahakama ikamuamuru kwenda jela au kulipa faini ya Sh milioni 138 akalipa na kuachiwa huru.
“Baada ya hapo nilipangiwa majukumu mengine, nilienda mkoani Arusha kwenye kesi ya Lema, hivyo kesi hiyo nyingine ilikuwa na wanasheria wa mkoa. Ila nimesikia kuwa imefutwa, siwezi ongea zaidi ya hapo, Mbeya wanaweza kukusaidia nini kilitokea mpaka ikawa hivyo,” amesema Kadushe.
Mwakilishi wa Ofisi ya DPP Mkoa wa Mbeya, Joseph Pamde, ameulizwa juu ya kufutwa kwa kesi hiyo, lakini akaruka kwa madai kwamba si msemaji.
“Ofisi yetu ina taratibu, na taratibu ni kwamba anayepaswa kuongelea mambo ya kesi mahakamani ni Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP); ukimpata yeye atakwambia kila kitu kuhusu hiyo kesi unayoiulizia,” anasema Pamde.
DPP Biswaro Mganga hakupata kutokana na maelezo kwamba yuko nje ya nchi. Anatarajiwa kurejea nchini leo.