Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol, ametangaza hali ya hatari muda mfupi uliopita, katika hotuba ya usiku wa manane.

Amesema hatua hiyo ni muhimu ili kuilinda nchi kutokana na vikundi vya kikomunisti vya Korea Kaskazini na kuwaondoa watu wanaoipinga serikali. “Uamuzi huo umefanywa ili kuviondoa vikundi vinavyoiunga mkono Korea Kaskazini na kuilinda katiba.”

Ripoti kutoka vyombo vya habari vya Korea Kusini, vinasema jeshi la nchi hiyo limetangaza kusimamisha shughuli zote za bunge. Shirika la Habari la Yonhap linasema wajumbe wa Bunge la Kitaifa wamepigwa marufuku kuingia kwenye jengo hilo.

Kanda za video zimeanza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaonyesha uwepo wa maafisa wengi wa usalama nje ya bunge. Shirika la Habari la Yonhap linaripoti kwamba kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Party cha Korea Kusini, Lee Jae-myung, amesema kutangazwa hali ya hatari ni kinyume cha katiba.

Yonhap pia limeripoti kwamba Han Dong-hoon, mkuu wa chama tawala cha People Power Party – ambacho Rais Yoon Suk Yeol ni mwanachama – pia ameapa kulizuia tamko hilo, akielezea ni “makosa.”

Yoon amekuwa rais aliyekosa nguvu tangu uchaguzi mkuu wa hivi karibuni baada ya upinzani kushinda kwa kishindo na hakuwa na uwezo wa kupitisha sheria alizotaka.

Yoon pia amekumbwa na kashfa kadhaa, moja ikimuhusu mkewe, ambaye anatuhumiwa kwa ufisadi. Upinzani umekuwa ukijaribu kuanzisha uchunguzi maalum dhidi yake. Wiki hii, upinzani ulizuia bajeti ambayo serikali na chama tawala ilipendekeza.

Pia upinzani, unapanga kuwashtaki wajumbe wa baraza la mawaziri, hasa mkuu wa wakala wakaguzi wa serikali, kwa kushindwa kumchunguza mke wa rais.