Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete, Salaam. Mei 30, 2012, madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, walimwandikia Mkurugenzi Mtendaji barua wakimtaka aitishe kikao maalumu cha Baraza la Madiwani, kujadili tuhuma mbalimbali za ufisadi walizozielekeza kwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Kashunju Runyogote.
Tuhuma hizo ziliandikwa kwenye gazeti la JAMHURI toleo la No. 29 la Juni 19-25, 2012. Baadhi ya tuhuma hizo ni pamoja na kupokea malipo ya posho ya kukagua miradi wakati huo huo akapokea fedha za kwenda Rwanda ambako ziara hiyo iligharimiwa pia na Serikali ya Rwanda. Ukaguzi wa miradi ulifanyika wakati Mwenyekiti akiwa Rwanda.
Hata hivyo, pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Ernest Kahabi, kulipa fedha za ziara ya kwenda Rwanda kiasi cha Sh 7,132,320 alikuwa na barua ya mwaliko inayoeleza wazi kuwa gharama zote za ziara hiyo zitalipwa na Serikali ya Rwanda. Takriban mwezi mmoja tangu Mwenyekiti Runyogote apokee fedha za ukaguzi wa miradi na siku mbili baada ya madiwani kupeleka tuhuma kwa Mkurugenzi, Runyogote alirejesha Sh 270,000 na kukatiwa risiti rasmi.
Tuhuma nyingine ni za malipo ya Sh 3,591,000 (kwa hati ya malipo namba 0080134 na hundi namba 000293 ya Oktoba 2011) yaliyofanywa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Kahabi kwa Runyogote, ikiwa ni posho ya siku tano kwenda Rwanda kwenye sherehe za kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere wakati sherehe zilikuwa za siku moja! Ikumbukwe kuwa kutoka Karagwe kwenda Rwanda ni safari ya saa nne tu.
Malipo mengine yenye utata ni ya posho ya siku saba (siku mbili kulala Mwanza na siku tano kukaa Kisumu) Sh 9,319,730 aliyoidhinisha Kaimu Mkurugenzi, Kahabi kwa ajili ya Runyogote, kwenda Kisumu, Kenya kwenye kikao cha mwaliko wa siku moja ya Julai 29, 2011.
Haya ni baadhi tu ya maamuzi waliyofanya wakitumia madaraka yao vibaya na kusaini mikataba yenye utata. Juni 6, 2012, kilifanyika kikao cha CCM ngazi ya mkoa kilichohudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa, Pius Msekwa. Kikao hicho kiliunda timu kuja Karagwe na kushinikiza madiwani wote wa CCM wamsamehe Mwenyekiti Runyogote.
“Wakati hayo yote yanafanyika madiwani wote wa CCM hatujaridhishwa na kitendo cha wabadhirifu wa mali ya wananchi wanaolia umaskini kila kukicha. Vilevile, kitendo hicho kinatufunga midomo wananchi na madiwani kwa sababu hata watumishi wengine wakifanya maovu tutashindwa kuwakemea maana wakubwa wao tayari wameonesha njia ya kuwasamehe na wao watadai wasamehewe ilhali mali ya umma iendelee kupotea.
“Fedha hizi zilizotafunwa zinatokana na vyanzo mbalimbali vya Halmashauri ukiwamo ushuru wa kahawa, ambao wananchi maskini wamechangia hivyo wanaona uchungu kuona fedha hizi badala ya kufanya maendeleo zinatafunwa na mtu mmoja au wawili na msamaha wa kutochukuliwa hatua za kisheria unatolewa.
“Hivi majuzi huko Dodoma, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua awamu ya tatu ya TASAF (Mfuko wa Taifa wa Jamii), alikemea na kusisitiza wabadhirifu wa fedha za umma wafichuliwe na kuchukuliwa hatua, kinyume chake Makamu Mwenyekiti wake wa chama, Msekwa, anaamuru Runyogote asamehewe eti kwa sababu amekiri kufanya ubadhirifu.
“Kauli ya juzi ya Mheshimiwa Rais inatia moyo, lakini inashangaza kuona baadhi ya viongozi wa juu wanatunyamazisha tunapoibuka na tuhuma za ubadhirifu kama za Runyogote na watendaji. Hawa wanatuharibia chama. Badala ya kushughulikia tuhuma inashangaza kuona Runyogote amesamehewa na Kahabi amehamishiwa Sikonge.”
Tunajua Runyogote alikwishazungumza na Gazeti la JAMHURI akakanusha karibu haya yote na mengine anayotuhumiwa nayo. Msekwa pia alieleza kupitia Gazeti la JAMHURI kuwa haikuwa nia yake kuzuia Runyogote asichunguzwe bali alitaka wakaangalie chama kina tatizo lipi. Ombil letu kwako Mheshimiwa Rais ni wewe kuingilia mgogoro huu.
Tunakuomba kwa nguvu uliyonayo kama Mwenyekiti wa CCM na Amiri Jeshi Mkuu uiokoe Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambayo maendeleo yote yamesimama. Tunatanguliza shukrani kwako Mheshimiwa Rais, tukitarajia msaada wako wa haraka katika hili. Wako, Kamukulu Mussa wa Karagwe, mkoani Kagera.
Wako, Kamukulu Mussa wa Karagwe, mkoani Kagera.