Rais Jakaya Kikwete amesema Watanzania watakuwa na Katiba mpya ifikapo mwaka 2014. Alipoulizwa kama hilo litawezekana hasa ikizingatiwa kuwa Kenya iliwachukua miaka saba kuwa na Katiba mpya, alijibu kwa mkato, “Hao ni Kenya, sisi ni Tanzania.”
Wananchi wengi wamekunwa na uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uliofanywa na Rais Kikwete, kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
Rais Kikwete alitangaza wajumbe hao mwishoni mwa wiki iliyopita alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Wananchi wengi wamepiga simu katika chumba cha habari cha JAMHURI wakipongeza uteuzi huo. Miongoni mwao ni Charles Nyamwasha aliyesema, “Tumepata watu makini, huu ni mwanzo mzuri wa kuelekea kupata Katiba ya Watanzania. Ukiacha dosari ya Tume yote kuongozwa na wanaume, lakini kwa kweli viongozi wetu wakuu wamefanya uteuzi wa maana sana.”
Pongezi kama hizo zimetoka kwa watu wa kada mbalimbali, hasa wanaofuatilia kwa karibu suala zima la marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kutangazwa kwa Tume hiyo ni utekelezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83, Toleo la 2012, Vifungu 5, 6 na 7.
Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Jaji Joseph Sinde Warioba. Jaji huyo alishaongoza Tume ya Kuchunguza Mianya ya Rushwa iliyoundwa na Rais Benjamin Mkapa mwaka 1996. Ripoti ya Tume hiyo maarufu kwa jina la “Tume ya Warioba”, inatajwa kama miongoni mwa ripoti nzuri kuwahi kutolewa nchini. Hata hivyo, wananchi wengi hawajaridhishwa na namna Serikali ilivyotekeleza mapendekezo yake.
Makamu Mwenyekiti ni Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani. Huyu ameshapata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi na ni miongoni mwa wanasheria nguli wanaoheshimika duniani. Pia ni mwanajeshi aliyestaafu akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali.