Rais wa Namibia Hage Geingob amefariki dunia wakati akipata matibabu hospitalini katika mji mkuu, Windhoek.
Makamu wa Rais Nangolo Mbumba ametangaza kuwa Geingob amefariki Jumapili alfajiri.
“Mkewe Monica Geingos na wanawe walikuwa karibu naye,” Mbumba amesema katika taarifa yake.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 aligunduliwa kuugua saratani na alitangaza hali yake mbele ya umma mwezi uliopita.
Ofisi yake ilitangaza kwamba atasafiri kuelekea Marekani kupata matibabu, lakini kwamba atarudi Namibia Februari 2.
Geingob aliapishwa kuwa rais mnamo 2015 na alikuwa anatumikia awamu yake ya pili na ya mwisho ya uongozi.
Alifanyiwa upasuaji wa moyo mwaka jana, na mnamo 2014 alifichua kuwa amepona saratani ya tezi dume.
Namibia inatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu Novemba.
Chama tawala cha Swapo ambacho kimekuwa madarakani tangu 1990, kimemteua Nandi-Ndaitwah kama mgombea urais.
Yeye ndiye Waziri mkuu wa sasa na iwapo atashinda, atakuwa rais wa kwanza mwanamke nchini humo