Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi wa Umwagiliaji Mkomazi unaofekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) mkoani Tanga.

Amesema, mradi huo umezungumzwa kwa miaka zaidi ya 50 sasa Serikali inajenga.

Akizungumza katika uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkomazi, Dk. Samia alisema ni mradi uliozungumzwa kwa miaka mingi bila ya kufanyiwa kazi, lakini sasa Serikali imeamua kuujenga. Alisema ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa mradi huo.

“Ni matarajio yangu kuwa itakapokamilika miradi hiyo kero ya maji itakuwa ni historia huku Lushoto, bwawa hili likikamilika litakuwa na uwezo wa kuingiza maji zaidi ya lita bilioni 70 kwa ajili ya kilimo,”
alisema.

Alisema lengo la ujenzi wa bwawa hilo ni kutumika katika shughuli za kilimo na mambo mengine lakini kubwa ni uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Alisema, Tanzania sasa inajitegemea kwa mazao ya chakula kwa asilimia 128 lakini ni Tanzania pekee, wenzetu wanaotuzunguka bado hawajajitosheleza, kuna soko kubwa katika kilimo na huko ndio wanataka kuelekeza vijana.

“Mabwawa tunayojenga yanakwenda kuongeza eneo la kilimo na kuvuna maradufu ndani ya mwaka mmoja, tunakwenda kufanya Tanzania iwe nchi ya kilimo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema kilimo ndio uti wa mgongo tunakwenda kulithibitisha hilo, ombi langu kwenu wananchi ni kushirikiana na wajenzi wa hii miradi,” alisema.

Alisema mradi huo utawanufaisha wananchi zaidi ya 20,000 katika kata saba na vijiji 28.

“Nilimpa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, sh. bilioni 18.2 kwa ajili ya mradi huu ambao utawezesha kushiriki shughuli za kilimo, wakulima watalima sasa bila kutegemea mvua, ukivuna utasikiliza ushauri wa maofisa kilimo, unaendelea kulima kitu kingine, ili mradi ndani ya mwaka utavuna mara mbili au mara tatu,” alisema.

Alisisitiza kuwa uwepo wa mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa wakulima na amepata faraja, kutokana na kuona waliokuwa hawautaki mradi huo wamekunjua mioyo yao na mradi umeanza kutekelezwa ni matumaini yake utamalizika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Husein Bashe, amesema mradi huo unatekelezwa kwa kasi kubwa kama Rais Dkt Samia alivyoagiza na kamwe serikali haitakubali siasa ikatishe utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji.

“Tunaishukuru sana Wilaya ya Korogwe na mkoa kwa ujumla mradi huu ulikuwa na siasa wapo baadhi ya watu walitaka usitekelezwa, tulisimama serikali na kuhakikisha miradi ya maendeleo ambayo ni muhimu kwa jamii inatekelezwa,”alisema.

Alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi 100 ya vipaumbele ya Umwagiliaji ambayo Tume chini ya Wizara ya Kilimo inaendelea kuikamilisha.

Mradi wa Mkomazi ni wa kihistoria, uliobuniwa zaidi ya miaka 50 iliyopita lakini umekuwa ukisuasua kutekelezwa kwa muda mrefu. Serikali ya wamu ya sita (6) chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dr. SamiaSuluhu Hassan imetoa fedha kwa ajili ya kuutekeleza mradi huu ili kuwanufaisha wananchi zaidi ya 20,000 kutoka kata saba za Mkomazi, Mkumbara, Mazinde, Mombo, Chekelei, Makuyuni na Magila Gereza.

Mradi huo unagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 18 utahudumia vijiji 28 katika kata saba (7) katika wilaya ya Korogwe. Aidha, mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2025. Kazi zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa tuta la udongo la kuzuia maji, ujenzi wa barabara kuelekea eneo la mradi, na ujenzi wa ofisi ya meneja wa mradi.