Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika sekta ya madini mwaka 2024 utakaofanyika kuanzia Novemba 19 hadi 21, mwaka huu.

Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi Tanzania huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii’.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam, kuhusu maandalizi ya mkutano huo Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema zaidi ya wadau 1500 kutoka mataifa mbalimbali duniani wanatarajia kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa kwa lengo la kujadiliana namna nzuri ya kuendeleza sekta hiyo hasa kwenye masuala ya teknolojia na uongezaji thamani madini.

Amesema miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni mawaziri wa madini kutoka nchi nyingine za Afrika, watendaji wakuu wa kampuni kubwa za madini duniani zilizowekeza na zinazotarajia kuwekeza nchini, watafiti na mabalozi 31wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

“Serikali ya Tanzania inafanya mkutano huu wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini kila mwaka ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kuendelea kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

“Mkutano huo ni jukwaa la kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana maarifa, ujuzi na kuangazia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hiyo inayokua kwa kasi,” amesema.

Ameongeza kuwa mkutano huo unatoa nafasi kwa washiriki kujifunza kuhusu sera na mikakati mipya ya serikali, kujadili masuala ya kisheria na kiuchumi yanayohusiana na madini, na kushuhudia teknolojia mpya na ubunifu unaoweza kuleta thamani zaidi katika utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini kupitia mawasilisho na maonesho kwenye mabanda yanayoenda sambamba na mkutano,” amesema Mavunde

Amesisitiza kuwa mkutano huo unalenga si tu kuvutia uwekezaji, bali pia kuweka msingi thabiti wa ushirikiano baina ya wadau, kuimarisha uzalishaji wa madini, na kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinawanufaisha watanzania kiuchumi na kijamii.

Aidha amesema kuwa mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano mingine iliyotangulia tangu kuanza kwake mwaka 2019 ambapo Serikali ilitenga zaidi ya saa sita kusikiliza kero, changamoto na maoni kutoka kwa wadau wa madini.

Amesema kutokana na matokeo ya mkutano wa Mwaka 2019, Serikali iliona umuhimu wa kuwa na mikutano hiyo yenye sura ya Kimataifa na hivi sasa, imevuka mipaka ya nchi ikihusisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania wanaohusika katika mnyororo mzima wa shughuli za madini.

Hata hivyo amesema mkutano huo utaambatana na hafla ya usiku wa madini, tukio maalum la kutambua mchango wa wadau waliofanya vizuri katika sekta ya madini kupitia makundi mbalimbali.

Amesema hafla hiyo inalenga kutambua mchango wa wadau hao katika maendeleo na ukuaji wa sekta, huku ikihamasisha wadau wengine kuongeza juhudi, kuziona fursa zilizopo na kuchangia katika mafanikio ya sekta ya madini nchini.

“Kutokana na mustakabali wa sekta ya madini nchini na duniani, mkutano huu unatarajia kuwa na jumla ya mada 8 zitakazojadiliwa kutoka kwa watoa mada wapatao 20 kutoka nje ya nchi na 35 kutoka nchini waliobobea kwenye sekta ya madini. Mada zitakazojadiliwa zitagusia maeneo mengi ikiwemo changamoto zinazokabili masuala ya uongezaji thamani madini; fursa za uwekezaji na mitaji kwenye sekta ya madini,

“Mada zingine ni mikakati ya uendelezaji madini mkakati kwa ajili ya kuongeza manufaa ya mnyororo wa thamani; matumizi ya teknolojia katika uchimbaji mdogo wa madini; ushiriki wa wanawake na vijana katika Sekta ya madini; kuendelea kutangaza madini adimu ya Tanzanite, na masuala mengine yakiwemo uchimbaji bora na uhifadhi wa mazingira,” amesema Mavunge

Ameongeza kuwa mkutano huo utafungwa Novemba 21, mwaka huu na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi