Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho Juni 5, 2023 ameialika timu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) kwa chakula cha jioni Ikulu, Jijini Dar es Salaam kwa lengo kuipongeza kwa kufanya vizuri katika michuano ya soka ya kugombea Kombe la Shirikisho Barani Afrika iliyohitishwa jana Jijini Algers, Algeria.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia amewapongeza Yanga kwa kucheza vizuri katika mchezo wa pili wa fainali hapo jana kwa kuwafunga wenyeji wa mchezo huo bao 1-0 na hivyo kuwa na matokeo ya jumla ya mabao 2-2 japokuwa hawakufanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kutokana na kuruhusu kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa fainali uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam Tarehe 28 Mei, 2023.

Msigwa amebainisha kuwa pamoja na kutotwaa ubingwa, Mhe. Rais Samia anatambua kuwa Yanga wameipa heshima kubwa Tanzania na anawapongeza Wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo ambao ni Mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Timu ya Yanga, viongozi na mashabiki wanatarajiwa kurejea hapa nchini baadaye leo kwa ndege iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono timu hiyo iliyokuwa ikiiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kimataifa.