Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa miezi mitatu kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na watendaji wake kuhakikisha mradi wa maji wa Mtyangimbole unaanza kufanya kazi.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Septemba 24, 2024 wakati akiweka jiwe la Msingi katika mradi wa maji wa Mtyangimbole Songea mkoani Ruvuma unaoimarisha upatikanaji wa maji Madaba.

“Nimeona mradi, nimeona maendeleo, nimemwambia Waziri na Katibu Mkuu wake ambao ni wachapakazi wazuri sana pamoja na watendaji wao, ninawapa miezi mitatu tu, maji yatoke kwa wananchi hawa, kwasababu leo tumekuja kuweka jiwe la msingi tayari tumeshajenga matumaini kwao kwahiyo baada ya miezi mitatu, mwezi wa kumi na mbili, Krismass ikiingia maji yawe Mwaaa mwaaa mwaaaa ndani ya eneo hili,” amesema.

Aidha Rais Dkt. Samia amewaondoa hofu wananchi kuwa yeyote atakayepitia na mradi wa serikali atalipwa fidia.

“Niwashukuru wananchi kwa kupisha miradi iendelee kwa kusubiri fidia zao. Nataka niwahakikishie kwa kila anayepaswa kulipwa fidia atapata fidia yake, hakuna mradi utakaopita serikali ikachukua ardhi bila kulipa fidia. Tunaweza tukachelewa kulipa, kwasababu fedha zinakwenda kwenye mradi kwanza, lakini tutalipa fidia zote,” amesema.

Ametoa wito kwa Watanzania kufanya kazi kwa bidi, kulima mazao mengi na kuyauza kwa wingi ili kupata fedha nyingi zitakazosaidia kwa mambo mbalimbali.

“Miradi mingi tunayofanya ni ya fedha za kukopa nje, kwahiyo tunashindwa kwa mapato ya ndani jinsi ya kulipa fidia, lakini kwa jinsi tunavyokusanya ndivyo tunavyolipa fidia

“Kwahiyo tukizalisha kwa wingi, tukifanya kazi kwa wingi, fedha ikipatikana kwa wingi fidia hizi zitalipwa kwa mara moja. Lakini niwahakikishie kila mwenye haki yake atakwenda kupata haki yake,” amesema.