Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ametangaza kuipandisha hadhi Manispaa ya Mji wa Dodoma kuwa Jiji kuanzia leo Aprili 26, 2018.

Rais Dkt Magufuli ameyasema hayo leo, katika shotuba yake aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Nilifanikiwa kuiona Dodoma ilivyokuwa. Imejengwa kila mahali, na Dodoma kweli ni Makao Makuu. Tulizoea Dar es Salam ndiyo yalikuwa majao makuu kwa wakati ule, na paliitwa Jiji.Nikaona niangalie katika nchi yetu tuna Halmashauri ngapi, tuna manispaa ngapi na mimi nina mamlaka gani katika kutengeneza majiji au manispaa au kadhalika,” amesema Rais Magufuli.

“Nikakuta Arusha ni jiji, Tanga ni jiji, nikaambiwa Dodoma ni Manispaa, nikasema haiwezekani. Kwahivyo kuanzia leo Dodoma linakuwa Jiji,” amesema Rais Magufuli.

Vile vile Rais Magufuli amempandisha hadhi Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kutokana na kupanda hadhi yake.

Hatua hiyo inaifanya idadi ya majiji hapa nchi kufikia sita ambapo tuna jiji la Dar es Salaam, Jiji la Tanga, Jiji la Arusha, Jiji la Mwanza, Jiji la Mbeya na Jiji jipya la Dodoma.