Na Mwamvua Mwinyi, JahuriMedia, Pwani
Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, ameweka wazi kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia Halmashauri ya Mji wa Kibaha kupandishwa hadhi na kuwa Manispaa.
Mchengerwa ameeleza kuwa taratibu za mwisho zinafanywa, na kutatangazwa rasmi kuwa Manispaa hivi karibuni.
Ameeleza hayo katika mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani uliofanyika Mailmoja, Kibaha, mkutano ulioandaliwa kupongeza na kuunga mkono azimio la mkutano Mkuu maalum wa CCM uliofanyika Dodoma, kumchagua Mwenyekiti CCM Taifa Dkt Samia Suluhu Hassan kugombea kiti cha Urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mchengerwa alisema kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani, tayari ameunganisha vitongoji kuwa vijiji na vijiji kuwa miji kulingana na vigezo na utaratibu ulio wazi.
“Kwa namna mji wa Kibaha ulivyokuwa, hakuna sababu mji huu usiwe Manispaa. Rais Samia kwa kushirikiana na viongozi wa mkoa, wilaya, na jimbo, ameleta maendeleo makubwa Kibaha na Mkoani Pwani, na hayo ni manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Mchengerwa.
Alifafanua zaidi kuwa hakuna anayekataa kwa macho kwamba Rais Samia amefanya kazi inayoonekana na ameacha alama katika sekta zote, huku wananchi wakiwa mashahidi wa maendeleo hayo.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani (MNEC), Mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kura, na tutaakikisha hakuna kura inayopotea wakati wa uchaguzi.
MNEC huyo aliwataka madiwani, wabunge, na wanachama wa CCM kuendelea kukisemea chama kwa kueleza utekelezaji wa ilani na miradi iliyotekelezwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, alifurahi na kuishukuru Serikali kwa uamuzi huu baada ya maombi yao ya muda mrefu ya kuhakikisha mji wa Kibaha unakuwa Manispaa.
“Katika mji wetu, yaliyofanyika ni mengi kama maajabu, lakini Rais Samia anafanya maajabu zaidi. Mfano, mwaka 2010 wakati naingia madarakani, lami pekee ilikuwa kuanzia Tamco – Hospitali ya Tumbi hadi Pichandege. Leo hii, karibu kila kata ina barabara ya lami na ambazo hazijakamilika zinakwenda kutandazwa lami katika kata zote,” alibainisha Koka.
Koka alieleza kuwa kwa sasa Kibaha ina hospitali ya wilaya Lulanzi, vituo vya afya, umeme kila kona, miundombinu ya barabara, na ujio wa barabara sita katika barabara kuu ya Morogoro. Pia, nishati ya umeme, maboresho katika sekta ya elimu, na maji safi vimeendelea kutekelezwa, ambapo imebakia kata ya Pangani ambayo kuna mradi unaendelea, na ukikamilika kero hiyo itakuwa historia.
“Maendeleo haya yote ni matunda ya jitihada zilizofanywa na Serikali, madiwani, jimbo, na usimamizi wa CCM, na ndio sababu ya kupanda hadhi Halmashauri yetu kuwa Manispaa,” aliongeza Koka.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, alitoa tamko la Mkoa wa Pwani kuunga mkono Mkutano Mkuu maalum wa CCM kumchagua Mwenyekiti wa CCM Taifa kugombea nafasi ya Rais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Pia, walimpongeza Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza kupitia CCM katika uchaguzi huo.
Kadhalika, Mlao amempongeza Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, kuwa mgombea wa nafasi ya Rais kupitia CCM Zanzibar.