Watu wengi wameshtushwa na habari kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imetumia Sh bilioni tisa kwa ajili ya posho kwa kikao cha wafanyakazi wa Mamlaka hiyo.
Taarifa za matumizi hayo zimetokana na uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikaloi (PAC).
Tofauti na wananchi walioonesha mshangao wa matumizi hayo ya fedha za umma, kwetu sisi hatuna cha kushangaa. Hatushangai kwa sababu kwa miezi kadhaa Gazeti la JAMHURI tumeandika habari na makala nyingi mno zinazohusu ufisadi ndani ya TPA.
Kama ilivyo ada, wapo waliodhani tumeandika habari hizo kwa sababu ya chuki binafsi kwa menejimenti ya TPA. Lakini wapo waliokwenda mbali zaidi na kudai kwamba kuandikwa kwa habari hizo kunatokana na msukumo wa kisiasa kutoka kwenye kambi hasimu za kuwania urais mwakani.
Madai yote tuliyapuuza kwa sababu tuliamini kile tulichokuwa tukikiandika kilikuwa cha kweli, tena kweli tupu. Tunashukuru kuona na kusikia sasa umma ukianza kufahamu kile tulichokuwa tukiueleza kwa muda mrefu.
Tanzania si nchi maskini, ingawa watu wake wengi ni maskini kweli kweli. Umaskini wa Watanzania si wa bahati mbaya, bali ni wa kutengenezwa. Fedha nyingi sana za umma zinafujwa bila wahusika kuhojiwa wala kutiwa msukosuko wa kisheria. Haya ya TPA ni kama tone la maji tu katika bahari ya ufisadi ndani ya nchi yetu. Ulaji ni huo huo katika mashirika na taasisi zote za umma.
Kinachosikitisha zaidi ni kuona kuwa pamoja na tuhuma zote hizi kuibuliwa, bado kasi ya vyombo vya dola na mamlaka za uteuzi imekuwa ndogo mno katika kuwashughulikia watuhumiwa hawa.
Kinachosikitisha zaidi ni kuona kuwa wakati mabilioni ya shilingi yakiishia katika matumbo na mifuko ya wachache, makakwela wanakamuliwa ili waweze kufanikisha baadhi ya miradi muhimu katika jamii. Kwa mfano, hivi sasa kuna kazi inayoendelea nchini kote ya utekelezaji amri ya Rais Jakaya Kikwete ya kuhakikisha kila shule ya sekondari inakuwa na maabara.
Inauma kuona wananchi maskini wakichangishwa fedha, tena wakati mwingine kwa nguvu, huku mabilioni ambayo yangeweza kufanya kazi hiyo yakiishia kwa wachache. Mara zote tumesema hatutoi shinikizo kwa mamlaka za uteuzi kuchukua hatua, lakini ni wajibu wetu kuzisihi mara kwa mara kuchukua hatua ili kujenga imani kwa wananchi na Serikali yao.
Ilivyo sasa ni kama ruhusa imetolewa kwa kila mwenye uwezo wa kuiba au kufuja — aibe au afuje. Wananchi nao, kwa kuwa wanaona na kusikia haya ya TPA au Maliasili yakiendelea, nao wanamalizia hasira zao katika kuhujumu miradi kama ile ya mabasi yaendayo kasi. Nchi inamalizwa. Tunamuomba Rais Kikwete achukue hatua.