Rais wa Brazil Inacio Lula da Silva ameliomba Bunge la nchi hiyo kutangaza uwepo wa janga kwenye jimbo la kusini la Rio Grande do Sul baada ya watu 85 kupoteza maisha kutokana na mafuriko makubwa yanalolikumba eneo hilo.
Hatua hiyo itaruhusu serikali kuu kuongeza matumizi ya ziada ili kutuma msaada unaohitajika kwenye jimbo hilo bila kukiuka masharti ya ukomo wa bajeti yaliyoidhinishwa mwaka uliopita.
Waziri wa Mipango wa Brazil Simone Tebet amewarai wabunge kuridhia pendekezo la rais Lula, akisema serikali bado haijafahamu gharama halisi zitakazohitajika kulisaidia jimbo hilo.
Kiwango kikubwa cha maji kimeharibu barabara, kusomba madaraja na kusababisha maporomoko ya udongo kwenye miji ya jimbo la Rio Grande. Hadi kufikia jana watu 130 bado hawajulikani waliko na zaidi ya wengine 150,000 wamepoteza maakazi.