Na Englibert Kayombo,JamhuriMedia,Iringa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi katika Mkoa wa Iringa kuongeza usimamizi katika masuala ya lishe bora kwa watoto ili kuwa na watoto wenye afya bora pamoja na rasilimali endelevu kwa manufaa ya taifa.

Rais Samia amesema hayo leo akiwa Isimani Iringa akihitimisha Ziara yake ya kikazi katika mkoa huo kurejea Dodoma.

Rais Samia amesema wazazi wamekuwa hawajishughulishi na suala la lishe bora kwa watoto hivyo kupelekea Mkoa huo kuwa na takwimu kubwa za watoto wasio na lishe bora.

“Hapa kuna watu wanakwenda shambani asubuhi, wanampa mtoto uji kisha wanampa Ulanzi mtoto ili alale, kufanya hivyo unamkosesha milo mitatu ya lishe akiwa amelala” amesema Rais Samia akiwa anatolea mifano ya vitendo vinavyofanywa na wazazi ambavyo vinawakosesha watoto lishe bora.

Rais Samia ameitaka jamii kubadilika na kuweka msisitizo zaidi kwenye suala la lishe kwa watoto ili kuweka msingi wa kuwa na afya bora kwa watoto.

Aidha, Rais Samia amewataka wataalam wa lishe kuweka mkazo zaidi kwenye kutoa elimu ya lishe ili kuweza kuwa na watoto ndani ya jamii walio na afya bora.

Awali alizungumza Waziri wa Afya amesema kuwa Mkoa huo una tatizo kubwa la udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano.

Waziri Ummy amesema kiwango cha udumavu Iringa ni asilimia 47 ambapo katika kila watoto 100 wa Iringa wenye umri wa chini ya miaka mitano watoto 47 wamedumaa.

“Kwahiyo niwaombe sana ndugu zangu, tunazungumzia elimu bure, tunazungumzia maji, kilimo lakini kama watoto wetu wamedumaa maana yake hawatoweza kufundishika, hatutokuwa na rasilimali yenye ujuzi” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

“Tuna kila aina ya vyakula pamoja na maziwa katika mkoa wa Iringa, niwaombe sana wazazi tutoe kipaumbele kwenye suala la lishe bora” Waziri ummy akiwasihi wazazi.