Nashawishika kuamini kuwa kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, angekuwa hai, jambo moja kubwa ambalo angelipinga kwenye
Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba ni la muundo wa Muungano.
Sidhani kama angekubali muundo wa Serikali Tatu.
Sina hakika kama Mwalimu angepinga mambo mengi mazuri ambayo Tume ya
Jaji Warioba iliyaweka kwenye Rasimu, lakini yamefyekwa kana kwamba
hayana maana kwa Tanzania ya leo na ijayo.
Alipoingia Ikulu mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa kazi yake kubwa ya
kwanza ilikuwa kuteketeza maelfu ya ngano ya tajiri mmoja. Kazi hiyo
ilifanywa na makamanda wa JWTZ. Naamini Rais ajaye mwakani, kazi ya
kwanza itakuwa kutupa mbali kabisa hii ‘Rasimu ya Sitta’.
Ibara 28 kwenye Rasimu ya Warioba zimefutwa kwa sababu pengine
kutokana na kupanguliwa kwa suala la kuwa na muundo wa Serikali Tatu.
Kwa maneno mengine, kukwazwa kwa mfumo au aina hiyo ya muundo wa
Muungano kumezifanya ibara nyingine zife kifo cha kawaida.
Hata hivyo, kuna ibara zilizofutwa na wabunge hawa katika mazingira
yanayotia shaka. Na hapa ndipo inapokuja hoja ya kwamba Katiba yetu
haikupaswa kutungwa na watu wenye maslahi nayo. Kwa mfano, tumeona
wabunge wakipigia upatu kuendelea kwa sifa ya ‘kujua kusoma na
kuandika’ kama sifa mama ya kuchaguliwa kuwa mbunge. Hapa hakuna shaka
kwamba mbunge ambaye ana aina hiyo ya elimu, hawezi kukubali kuona
sifa ya kuwa mbunge ikibadilishwa. Kuikubali maana yake ni kumwambia
akose ubunge.
Jaji Warioba na timu yake wamemaliza kazi yao. Najua wajumbe wengi
kwenye Tume hiyo wanasikitika. Wanasikitika kwa sababu wanaona kazi
waliyofanya imetupwa. Imeonekana haina maana. Kwa maneno mengine,
wajumbe hao wanaona wamefanya kazi iliyoshusha au kupoteza heshima
yao. Hili linawauma hasa miongoni mwao wanapoona namna jamii na
jumuiya ya kimataifa inavyowaheshimu.
Nawaomba Jaji Warioba na timu yake watulie kwa sababu sisi tulio huku
mitaani tunasikia maneno ya wananchi — maneno ya hasira. Wananchi
wanajiandaa kuiadhibu Rasimu ya Sitta. Kinachofanywa na waheshimiwa
hawa ni kuendeleza hila za kushika madaraka, basi. Wiki mbili zilizopita nilihoji weledi wa baadhi ya wabunge wetu katika kufikia mwafaka wa kupitisha rasimu hii ambayo sioni soni kuitambua kama rasimu mbovu kabisa.
Nitajaribu kueleza kwa uchache. Baadhi ya ibara zilizofutwa kwenye
Rasimu ya Warioba ni ya 15 iliyohusu zawadi wanazopewa viongozi wakuu
wakati wa utekelezaji dhima zao. Rasimu ilitaka zawadi anazopewa
kiongozi ziwe mali ya umma. Wabunge wamelikataa jambo hilo. Wanataka
mali ziwe za huyo aliyepewa. Rais akienda mgodini akapewa rushwa ya
kilo 10 za dhahabu, hiyo iwe mali yake kwa sababu ni ‘zawadi’ halali
aliyopewa! Hatari ya uamuzi huu ni kwamba rushwa sasa itatolewa kwa
mgongo wa ‘zawadi’. Haina tofauti na ile rushwa iliyoletwa kwa
msamiati wa ‘takrima’.
Ibara ya 17 ilitaka kiongozi wa umma pamoja na mke/mume na watoto wake,
aorodheshe mali na madeni yake kwa muda utakaopangwa kisheria, kwa
maana wakati wa kuingia na wakati wa kutoka tujue kavuna au kapoteza
nini. Hilo limepingwa. Kwa maneno mengine wanataka tuwe na waziri
anayeingia madarakani akiwa lofa wa mali, lakini baada ya kutoka
madarakani awe na ukwasi ambao hauhojiwi! Hawa ni wabunge walio karne
ya 21!
Ibara ya 20(1) ilipendekeza mali za kiongozi ambazo kazipata kwa
kukiuka sheria zitwaliwe ili ziwe za umma. Hilo wabunge hawa
wamelikataa. Hawataki kuliona katika Katiba. Kwa maneno mengine,
kiongozi anayekuwa madarakani aibe kadri anavyoweza kwa sababu hakuna
breki ya kumzuia iliyowekwa kikatiba.
Katika Ibara ya 103 kulikuwa na hoja njema ya kuona mawaziri na naibu
wao hawahudhurii vikao vya Bunge. Kwa maneno mengine mawaziri wasiwe
wabunge ili uwajibikaji wao uwe mkubwa na wenye tija kwa nchi. Hilo
waheshimiwa hawa wamelikataa. Wanataka mawaziri waendelee kutoka
miongoni mwa wabunge. Hili wamelikomalia kwa sababu ubunge wanautaka
na uwaziri wanautaka. Kwa hiyo, kusema wawe wabunge tu ilhali na
uwaziri wanautaka, hawawezi. Na uwaziri wanapoutaka, na kama
ilivyokuwa kwenye Rasimu ya Warioba, ilibidi wabaki nje ya Bunge ili
pengine kwa dua na ndumba, waweze kuteuliwa kuwa mawaziri.
Lakini hapo hapo hakuna mwenye hakika asipogombea ubunge atateuliwa
kuwa waziri. Kwa hiyo, njia rahisi waliofanya ni kuona waziri anatoka
miongoni mwa wabunge; na kwa njia hiyo akikosa uwaziri, basi walau awe
mbunge. Wametega kote kote. Huu ni ubinafsi. Kama kweli tulidhamiria kupata Katiba nzuri, ilikuwa hawa wanaotunga hii Katiba wazuiwe kisheria kuwa kwa miaka walau mitano ijayo wasigombee ubunge. Bila shaka wangekuja na Rasimu ya maana.
Ibara ya 107 ilihusu Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu chini ya Katibu
Mkuu Kiongozi ambayo ingekuwa na dhima ya kuchambua na kulishauri
Baraza la Mawaziri juu ya masuala mbalimbali kabla ya kuwasilishwa na
kutolewa uamuzi na Baraza hilo. Hili nalo wamelikataa. Ibara hii
ilikuwa muhimu kwa sababu makatibu wakuu ni wataalamu; tofauti na
mawaziri ambao ni wanasiasa tu.
Kituko kingine kilichofanywa na Bunge hili ni kuifuta Ibara ya 129
iliyokuwa ikipendekeza kuwapo nguvu za kikatiba kwa wananchi kumwondoa
mbunge madarakani. Mambo ambayo yangeweza kuwafanya wananchi wachukue
hatua hiyo ni kama mbunge angeunga mkono sera zinazoenda kinyume cha
maslahi ya wapigakura, au maslahi ya Taifa; kushindwa kuwasilisha kero
za wapigakura, kuacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la
Jimbo la Uchaguzi kwa miezi zaidi ya sita bila sababu za msingi; na
kadhalika.
Ibara hii ingesaidia kuondoa vilio vya wapigakura kwa sasa ambao
hulalamika kuwa hawaoni wabunge wao uchaguzi unapomalizika. Wabunge wengi wamekuwa wakiishi mijini kwa kisingizio kwamba huko ndiko wanakosaka misaada kwa ajili ya wapigakura wao. Hili wabunge wamelikataa kwa sababu wanajua ni hao hao watakaokuwa wabunge mwakani, kwa hiyo kutunga sheria ya kuwaondoa ni kuwaondolea uhondo wanaoufaidi bungeni. Haihitaji akili nyingi kubaini kuwa huwezi kumpa mlamba asali ajipangie muda anaotaka kuacha kulamba asali!
Ibara ya 253 ilikuwa na orodha ndefu ya watumishi ambao wasingekuwa na
haki ya kugombea, kuchaguliwa au kuteuliwa kushika nafasi za kisiasa
hadi unapopita muda wa miaka mitatu tangu kuacha au kustaafu madaraka
au nafasi aliyokuwa akishikilia. Humo wamo majaji, wakuu wa vyombo vya
ulinzi na usalama, makatibu wakuu, Msajili wa Vyama vya Siasa, na
kadhalika. Ibara hii, na nyingine, zimefafanuliwa vizuri sana kwenye
Bango Kitita. Hawa wakubwa wameliweka kando na sasa linaletwa kwa
staili tofauti kabisa. Wanataka hawa wanaosimamia wananchi kupigwa chini,
waking’atuka tu kwenye upolisi, waingie katika siasa. Ndiyo maana kuna
matendo mengi ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kujipendekeza
kwa wanasiasa kwa sababu wana malengo mapana ya kuingia kwenye siasa
au bodi za mashirika ya umma, au kuteuliwa kuwa mabalozi!
Wabunge hawa hawa walipinga muundo wa Serikali Tatu kwa nguvu kubwa
sana kwa kigezo kwamba zingeongeza gharama za uendeshaji, lakini ni
wabunge hawa hawa ambao sasa wanapendekeza Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania liwe na wabunge 360 na wasiozidi 420! Wanapendekeza kuwapo kwa marais wanne — kwa maana ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais watatu.
Wameondoa Mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ingefanya kazi
kubwa ya kumpendekeza kwa rais majina ya watumishi wa nafasi mbalimbali. Badala ya kupunguza madaraka ya rais, wao wameongeza. Katiba ya majirani zetu Kenya imejitahidi sana kupunguza madaraka ya rais. Leo hii Rais Uhuru Kenyatta hawezi kuamka na kumtangaza Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, na kadhalika.
Wenzetu wamefikia hatua ambayo kazi hizo zinaombwa na watu wenye sifa. Wanafanyiwa usaili hadharani huku vyombo vya habari vikirusha mahojiano hayo moja kwa moja. Sisi hapa hata uteuzi wa makatibu wakuu bado tunaiacha kazi hiyo ifanywe na rais mwenyewe. Bado tunataka hata mkuu wa Shirika la Masoko
Kariakoo ateuliwe na rais. Huyu rais atafanya kazi ngapi?
Lakini jingine linalotia hasira ni hili la kuwapo wagombea binafsi. Suala hili wameliruhusu, lakini kuna kila dalili kuwa fursa ya kuwapata wagombea binafsi itakuwa ngumu mno kutokana na masharti yanayoandaliwa. Moja ya mambo hayo ni kama lile la kuwapo muda maalum kwa anayetaka kugombea, wa kuwa amejitoa katika chama cha siasa.
Ndani ya mpango huu kuna hila za Chama Cha Mapinduzi (CCM) za
kuhakikisha wanachama wake wengi hawakihami chama hicho na kwenda
kugombea endapo majina yao yatakatwa kwa mizengwe kwenye vikao vya
vyama. Kwanini mgombea binafsi isiwe fursa huru kwa kila mwenye sifa.
Ndiyo, sheria na vigezo vinapaswa kuwapo, lakini havipaswi kuwakwaza
watu.
Kwa haya na mengine, ndiyo maana namsihi Jaji Warioba akae kimya. Sauti
zinazotolewa na wapinzani wake hawezi kuzikabili maana zimejaa kiburi na jazba. Kitu pekee kitakachopigana vita hii kwa niaba yake, ni historia. Na hiyo historia imo mwenye mioyo na bongo za Watanzania. Mijadala inayoendelea mitaani na katika mitandao ya kijamii inadhihirisha pasi na shaka kuwa wananchi, kwa idadi ya kutosha; wapo nyuma ya Jaji Warioba.
Tulidhani kupinga mfumo wa Serikali Tatu, kama kweli kulikuwa na hoja
ya kufanya hivyo, ndiko kungekuwa jambo kuu la wanaompinga Jaji Warioba, na si kufuta hata mambo kama ya uadilifu yaliyokuwa kwenye Rasimu yake. Rasimu ya Sitta imeandaliwa na wabunge kwa misingi ya ndoto za Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuitawala nchi hii. Huo ni ubinafsi unaoweza kuliangamiza Taifa.
Kama wengine wamejipachika jukumu la kutaka Watanzania Rasimu hii kura ya ‘ndiyo’; kwanini iwe nongwa kwa wanaosema ipigiwe kura ya ‘hapana’? Sina kigugumizi kuwasihi Watanzania kwa kuwaambia; “Ikataeni Rasimu ya
Sitta”. Bado naamini rais ajaye baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani, kama
kweli kwake Tanzania ni zaidi ya CCM au Chadema au CUF, ataitupilia
mbali rasimu hii iliyojaa ubinafsi.