Raia watatu wa China wametiwa mbaroni wakiwa na vipande 12 vya dhahabu na dola 800,000 za Kimarekani katika sehemu ya mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kwa mujibu wa Gavana wa Mkoa wa Kivu kusini Jean Jacques Purusi.

Dhahabu na fedha hizo zinadaiwa kuwa walizificha chini ya viti vya gari walilokuwa wakisafiria.

Gavana Jean alisema operesheni ya kuwakamata watu hao ilifanywa kIsiri baada ya kuachiwa kwa kikundi kingine cha raia wa China waliokamatwa kwa tuhuma za kuendesha mgodi haramu wa dhahabu katika eneo hilo.

Sehemu ya mashariki ya DRC ina hifadhi kubwa ya dhahabu, almasi, na madini yanayotumika kutengeneza betri za simu na magari ya umeme.

Utajiri huu wa madini umekuwa ukinyakuliwa na makundi ya kigeni tangu enzi za ukoloni na ni moja ya sababu kuu za mzozo unaokumba eneo hilo kwa zaidi ya miaka 30.

Makundi ya waasi yanadhibiti migodi mingi katika mashariki ya DRC na viongozi wao wanapata utajiri kwa kuuza madini hayo kwa wafanyabiashara wa kati.

Mwezi uliopita, Gavana Jean aliiambia vyombo vya habari kwamba alishangazwa kusikia kwamba raia 17 wa China, waliokamatwa kwa tuhuma za kuendesha mgodi haramu wa dhahabu, walikuwa wameachiliwa na kuruhusiwa kurejea China.

Hata hivyo, ubalozi wa China haujatoa maoni kuhusu tuhuma hizo.