Polisi mkoani Kigoma kwa kushirikiana Idara ya Uhamiaji imewakamata watu 86 kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo wakiwa wanaishi na kufanya kazi nchini bila vibali.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema watu hao walikamatwa katika operesheni maalum iliyoendeshwa baina ya polisi na uhamiaji katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Kamanda Makungu alisema wahamiaji hao waliamatwa katika maeneo ya stendi kuu ya mabasi mjini Kigoma na vizuizi mbalimbali vya barabarani ambavyo polisi na uhamiaji huvitumia kukagua masuala ya ulinzi na usalama ikiwemo masuala ya uhamiaji.
Aidha kamanda huyo alisema kuwa baadhi ya wahamiaji hao wanatuhumiwa kufanya kazi za vibarua kwenye mashamba ya watu bila kuwa na vibali huku wakiwa wameingia nchini kupitia katika njia zisizo halali.
Katika tukio lingine kamanda Makungu alisema kuwa polisi imekamata bunduki moja aina ya Gobole iliyotengenezwa kienyeji ikiwa imetelekezwa baada ya aliyekuwa akimiliki kukimbia baada ya kuhisi polisi wanafuatilia nyendo zake.
Akieleza tukio hilo Kamanda huyo wa polisi alisema kuwa gobole hilo lilikamatwa katika eneo la Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na askari waliokuwa kwenye operesheni ya kuzuia uhalifu.