Kama ilivyo kwa nchi nyingine nyingi duniani, sekta ya usafiri wa reli ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Miundombinu ya usafiri wa reli huunganisha vituo vya uzalishaji mali na masoko katika sekta za kiuchumi kama vile kilimo, viwanda, madini na utalii.
Serikali imekuwa ikifanya juhudi katika kutekeleza mikakati inayolenga kufufua mtandao wa usafiri nchini ukiwemo wa reli.
Moja ya mikakati hiyo ni kufufua usafiri wa reli katika Mkoa wa Dar es Salam kupunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa jiji hilo baada ya Shirika la Usafiri (UDA) na watu binafsi kuelemewa na mahitaji ya wakazi wa hao.
Oktoba 30, mwaka huu, serikali ilitekeleza mpango wake wa siku nyingi kwa kuzindua treni ya abiria kwa ajili ya wakazi wa Dar es Salaam.
Tukio hilo la kihistoria lilizinduliwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, katika Kituo cha Ubungo Maziwa.
Historia ya Usafiri Dar es Salaam
Kabla na mara baada ya uhuru, huduma ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam ilitolewa na kampuni binafsi iliyojulikana kama Dar es Salaam Motors Transport (DMT).
Baadaye huduma ya usafiri katika jiji hilo ilitolewa na kampuni umma inayojulikana kama Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
UDA ilitoa huduma hiyo kwa kiwango cha kuridhisha hadi 1980 na baadaye ilianza kuzorota kutokana na matatizo ya kiutendaji.
Kushindwa kwa UDA kulisababishwa na usimamizi mbovu wa usafiri huo, hali iliyosababisha huduma hiyo kuzorota huku idadi ya watu na makazi ikiongezeka.
Watu binafsi waliingia kutoa huduma hiyo kwa kutumia magari madogo ya mizigo yaliyojulikana kama Chai-Maharage na baadaye Haice (vipanya) na yale ya saizi ya kati (Coasters) lakini hayakuziba pengo hilo pengo la ugumu wa usafiri.
Makundi maalumu, hasa wazee, wanafunzi, na watu wenye ulemavu wamekuwa wakishindwa kumudu adha za usafiri huo wakati wa asubuhi na jioni. Hali hiyo ilishawishi haja ya kuwa na mfumo mpya wa usafiri jijini.
Ujio wa usafiri wa Garimoshi
Usafiri wa Garimoshi ulianza kutolewa, Oktoba 30, mwaka huu na kuwafurahisha wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam. Furaha ya wakazi hao inatokana na jinsi linavyookoa muda wa kukaa katika msongamano barabarani na kuwahi kazini na nyumbani.
Mkazi wa Kimara-Baruti, Juma Hamisi, anasema kuwa tangu aanze kupanda garimoshi hilo amekuwa akitumia dakika 40 kufika kazini kwake tofauti na siku za nyumba ambako amekuwa akitumia zaidi ya saa mbili.
Anasema hata muda wa kulala umeongezeka kwania alikuwa kiamka saa 10:00 alfajiri lakini kwa sasa anaamka saa 12:30 asubuhi na kuliwahi garomoshi hilo.
“Usafiri huu umeturahisishia sana usafiri, tunawahi ofisini kwa wakati tumepunguza muda wa kuamka asubuhi, kama ulilazimika kuamka saa 10:00 alfajiri, sasa unamka saa 12:30 na unawahi kwenye mihangaiko yako.
“Unaona hapo unakuwa umepumzika kwa saa mbili na pia unatumia muda mfupi kufika kazini, ni kama dakika 35 hadi 40 wakati daladala kutoka Ubungo hadi Kariakoo au Posta ni zaidi ya saa mbili. Hiyo inaondoa uchovu na usingizi na inaoongeza ufanisi katika kazi,” anasema abiria mmoja.
Kila kwenye jambo zuri hapakosi kasoro wapo wanaolalamika kuwa kuna upungufu katika usafiri huo, hususan katika Kituo cha Stesheni.
“Usafiri huu ni mzuri, lakini mabehewa hayatoshi watu ni wengi na garimoshi linasubiriwa kwa muda mrefu vituoni.
“Tunatoa ombi kwa serikali kuongeza treni lingine au waongezee mabehewa watakuwa wafanikiwa kupunguza kero ya usafiri katika jiji hili kwa kuacha hilo wataendelea kututesa,” anasema Julius Mwangi Makazi wa Tabata.
Kwa upande wao, wamiliki, madereva wa daladala na makodakta, wanasema ujio wa treni hiyo kwao inawapunguzia ‘ulaji’ kutokana na usafiri huo kuwapunguzia soko.
Mmoja wa makodakta wa daladala aliyejitambulisha kwa jina moja la Abdalah, anasema ujio wa treni hiyo umefanya hali kuwa ngumu kwao sasa, kwa kuwa wanashindwa kutimiza kiwango cha fedha wanazoagizwa na wamiliki wa daladala.
Anasema treni hiyo imeathiri kwa kiwango fulani biashara ya daladala zinazofanya safari kati ya Ubungo na Mnazi Mmoja kupitia barabara ya Mandela, Ubungo-Posta, Ubungo-Kariakoo, Mabibo-Posta na Mabibo-Kariakoo kupitia barabara ya Morogoro.
Anasema kila safari moja ya treni hiyo inakadiriwa kuchukua nafasi ya daladala 20 nyakati za asubuhi, hali inayosababisha biashara yao kuwa ngumu.
“Unajua kuwa treni inafanya kazi asubuhi wakati ambao kwetu ndio muda wa biashara na kupumzika saa 5:00 asubuhi, ambapo hakuna biashara na kuanza kazi saa 9:00, muda ambao watu wanaanza kutoka ofisini na huu ndio ulikuwa muda wetu wa kuvuna,” anasema Abdalah.
Watu wengine wanaouona ujio wa usafiri huo wa treni ni mchungu ni waliojenga jirani barabara kwa kuwa watabomolewa nyumba zao siku si nyingi zijazo.
Tayari Kampuni Miliki ya Rasilimali za Reli (RAHCO) imeweka alama za X katika nyumba zote zilizojengwa ndani ya hifadhi ya reli na kuwataka wamiliki wa nyumba hizo kubomoa wenyewe kabla ya zoezi la kuzibomoa kuanza.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), Midladjy Maez, anasema huduma ya usafiri huo itaendelea kuboreshwa.
Anasema treni ya pili itaanza kutoa huduma mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya kugeuza kichwa cha treni katika Kituo cha Ubungo. Sehemu ya pili ni kukamilisha njia ya kupishana treni katika vituo vya Buguruni na Buguruni kwa Mnyamani.
Anasema kwa sasa mabehewa sita yanatumika kusafirisha abiria na kila behewa moja halitakiwi kubeba abiria zaidi ya 160 kwa wakati mmoja.
Kampuni ya Selcom Wireless inayotoa huduma ya tiketi katika vituo vya treni hiyo imeuthibitishia uongozi wa TRL kuwa imejipanga kuweka maduka maalumu katika vituo vyote saba.
0713393393