Mwenyekiti mstaafu wa Simba ya jijini Dar es Salaam, Ismail Aden Rage, amesema kwamba michuano ya Ligi Kuu Bara msimu huu itakuwa ngumu kwa timu za Simba na Yanga.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Rage amesema kwamba ugumu huo utatokana na timu nyingi zinazoshiriki kuwa na ufadhili unaoziwezesha kuendesha timu na kushiriki vyema kwenye michuano.

Amesema kwamba ufadhili uliotolewa na wafanyabiashara na kampuni binafsi ni kichocheo cha timu nyingi kufanya vizuri na kutoa ushindani mkali wa kushika nafasi za juu katika ligi msimu huu.

Rage anaeleza kuwa, “Miaka ya nyuma ukiondoa Simba na Yanga ambazo zilikuwa na ufadhili mnono, timu zilizobaki zilikuwa zikiendesha shughuli zake kwa shida. Hata ushiriki wa timu nyingi haukuwa wa ushindani kutokana na ukosefu wa ufadhili wa kugharamia shughuli za uendeshaji wa timu hizo katika Ligi Kuu.”

“Tunapoelekea, Ligi Kuu itakuwa na ushindani mkali na ulio sawa. Uwezekano wa Simba na Yanga kupokezana ubingwa utatoweka kama hatua za kujizatiti za kushinda hazitachukuliwa,” anaeleza Rage.

Timu zilizokuwa zikionekana kuwa ndogo kwa sasa zimesajili wachezaji wazuri mbali ya kuwa na uhakika wa usafiri, malazi na chakula kwa timu wakati michuano ikiendelea.

Anasema kwamba kwa kiasi kikubwa klabu hizo ‘ndogo’ zimeweza kulipa vema makocha, hali inayofanya wachezaji kuwa na ari ya mchezo.

Timu zinazofanya vema kwa sasa ni pamoja na Azam FC inayomilikiwa na kufadhiliwa na mfanyabiashara maarufu wa jijini Dar es Salaam, Said Salim Bakhressa. Timu hiyo kwa sasa ndiyo bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara.

Msimamo wa Ligi ya msimu huu unaonesha timu hizo za Simba na Yanga zimeporomoka kutoka katika nafasi zilizozoeleka kushikwa na timu hizo. Simba kwa sasa inashika nafasi ya tisa. Yanga yenyewe inashika nafasi ya nne.

Timu zilizopo kileleni ni Azam FC, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar, nafasi ya tatu inashikwa na Coastal Union huku ya tano ikidhibitiwa na Kagera Sugar, Mbeya City inashikilia nafasi ya sita, nafasi ya saba imekamatwa na Stand United na nafasi ya nane imetwaliwa na Prison.

Hadi sasa Simba imecheza mechi nne. Haijashinda mechi hata moja kati ya mechi hizo ilizocheza. Imeambulia sare katika mechi zote ilizocheza hadi sasa. Yanga imecheza mechi nne. Kati ya hizo imeshindwa moja, imesare moja na kushinda moja.

JAMHURI ilipohoji kulikoni sababu zinazoifanya Simba kusuasua katika Ligi, Rage alisema kwa sasa yeye si msemaji rasmi wa timu hiyo ila bado ana imani na matarajio mema na timu hiyo. Suala la kusuasua kwa timu ana imani linatafutiwa ufumbuzi na uongozi uliopo wa timu.

Rage anasema; “Jitihada za kocha wa timu hiyo kutoka Zambia, Patrick Phiri, la kuwatia moyo wachezaji wadogo ni suala la kupongezwa. Kwani zoezi hilo la kuwahamasisha wachezaji wadogo likiendelea litawezesha timu kuwa na wachezaji wengi bora katika siku zijazo.