Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa hai na kuandika makala hii, pili kushuhudia wewe ukiwa Mbunge wa jimbo la Kigoma Mjini, kwani sikutarajia kuwa ipo siku utakuwa mwakilishi wa wananchi wa mji huo.
Ni imani yangu kuwa ushindi wa jimbo la Kigoma Mjini kwako ni wa kihistoria, kwani umeweza kumgaragaza mwalimu wako wa siasa, Dk. Amani Walid Kabourou, aliyekuwa mbunge katika jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya kuangushwa hapo mwaka 2005 na Peter Serukamba wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Ndugu yangu Zitto, anuani yangu inasema leo tumsome Dk Kabourou, bila shaka huyu hujamfahamu mwaka huu. Kumbukumbu zangu zinaniambia kuwa mwaka 2005 pale katika uwanja wa Cine Atlas Ujiji Kigoma wakati Kabourou akizungumzia kushindwa kwake ubunge wa jimbo hilo, wewe ulisikitika sana na hata kuonekana kulia ukisema huko bungeni ungekuwa mgeni wa nani wakati mwalimu wako hakufanikiwa kurudi bungeni.Hukuamini kuwa alikuwa ameshindwa ubunge.
Hii ni ishara tosha kuwa unamfahamu Dk kwa ukaribu na miaka mingi tu.
Rafiki yangu Zitto, tumshukuru tena Jalali kwa kurejea kwako bungeni, safari hii kupitia Jimbo la Kigoma Mijni ambalo nathubutu kusema siasa ndio kwao.
Nasema hivyo kwa sababu sehemu kubwa ya wakazi wa mji huo – watoto kwa wakubwa – ni wanasiasa, nenda vijiwe vya kahawa, pale Ujiji, Gungu, Mwanga Urusi, wao ni siasa tu, bila shaka hili unalifahamu vema.
Mheshimiwa Zitto, natumai unazifahamu vema siasa za mji wa Kigoma Ujiji, siasa zao ni tofauti na sehemu kubwa ya nchi hii, zinafanana kidogo na zile za Kisiwa cha Pemba huko Zanzibar, ni siasa za mtu na si chama, na ndiyo maana licha ya uchanga wa chama chako, wamekupatia kura wewe ili uwe mbunge wao.
Mbunge wangu Zitto, fahamu kuwa wana-Kigoma Mjini hawafanyi siasa hizo kama kujifurahisha, au kwa uelewa mdogo, la hasha, wana-Kigoma wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na changamoto lukuki zinazowakabili ambazo, kutokana na usugu wake kuwapo mkoani hapo wamekuwa wakibadilisha wabunge kila uchao.
Wewe kwa sasa ni mbunge wa tatu kutoka vyama vitatu tofauti tangu kurejeshwa kwa mara ya pili kwa mfumo wa vyama vingi hapo mwaka 1992 nchini kwetu.
Utakumbuka vizuri Jimbo la Kigoma Mjini ni miongoni mwa majimbo ya mwanzoni hapa nchini kufanya mageuzi ya kivyama katika siasa, hawa walimchagua mtu waliomwamini sana Dk. Kabourou wakitarajia atawasaidia unafuu katika kero zao, ila haikuwa hivyo. Tuanze sasa kumsoma.
Ndugu yangu Zitto Kabwe, Dk Kabourou ni miongoni mwa waliowahi kuwa wabunge katika nchi hii wenye historia ya kipekee, huyu alipendwa sana zaidi ya kupendwa, huyu alibebwa kwenye kiti kama mfalme kutoka kituo cha gari moshi (treni) cha Kigoma Mjini hadi Ujiji japo Polisi walitibua msafara wake, na hicho kiti kilichongwa maalum kwa ajili yake.
Kutokana na watu kuwa na mahaba makubwa kwake, ilifikia mahala wakagawanyika kisiasa, hadi kidini, watu waligawana misikiti, masheikh nao wakaitwa huyu wa Dk. Kabourou, huyu wa Azim Suleyman Premji wa CCM enzi hizo.
Nakumbuka mwaka 2000 nikiwa bado nipo madrasa pale SwadaqatulJaria Ujiji, ustadhi wetu kinyume na utaratibu wa kutoka darasani saa 11 jioni alitufungia darasani hadi saa moja ya usiku eti akitwambia hataki kutuona tukienda kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea wa urais wa CCM wakati huo, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, pale kwenye Uwanja wa Kawawa Ujiji kwa sababu ya uvyama.
Siasa za enzi za Dk. Kabourou ziliwagawa sana wana-Kigoma, watu waligombana kwa ajili yake, wakanuniana, wakasusiana baadhi ya shughuli muhimu zikiwamo za dini, ilifikia hata hatua mtu ukionekana wewe ni CCM ilikuwa ni kama ni najisi, watu hata kuombana maji ilikuwa haiwezekani. Kisa upendo tu.
Lakini pamoja na mapenzi yote hayo, wana-Kigoma hawakuzisahau changamoto zao za mji wao, baada ya kumuona mtu waliyempenda akishindwa kuyatimiza ipasavyo matarajio yao, taratibu wakaanza kumchoka,ilipofika mwaka 2005 wakamuweka pembeni Dk. Kabourou, badala yake wakamchukua mtu ambaye hakujulina sana – Serukamba, mji ukashtuka tukaambiwa mende kaangusha kabati. Watu hawakuamini kushindwa kwa Dk Kabourou.
Waswahili wanasema: “Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.” Ni ukweli uliodhahiri kuwa Dk. Kabourou alisaidia kukua kwa kiwango kikubwa cha uelewa kwa wana-Kigoma kuhusu haki zao na mambo ya kisiasa, jambo ambalo liliwafanya kuanza kuwaona viongozi wa Serikali kumbe na wao hawakuwa juu ya sharia.
Itakumbukwa miaka ya nyuma, askari polisi kwa kutolea mfano, walionekana kama miungu-watu.
Pamoja na hayo yote kosa kubwa la Dk Kabourou ni kujisahau, akalewa umaarufu na mahaba, akashindwa kuwasemea wana-Kigoma Mjini ipasavyo huko bungeni kuhusiana na matatizo yao ya kimsingi, kazi yake ilikuwa mipasho tu, mara utamsikia anamsema huyu fulani haujui mwenyewe, mara hawa wamekuja kuvalia mikanda ya suruali hapa mjini, yaani alijaa kejeli za kila aina, na watu wakamshabikia kweli.
Wakati yeye akilewa sifa kwa mahaba, kipindi chote hicho cha ubunge wake mji wa Kigoma ulikuwa na matatizo lukuki, umeme wa mgawo wa kiwango cha kutisha, ilikuwa leo Ujiji, kesho Mwanga, licha ya uwepo wa Ziwa Tanganyika ambalo tulikuwa tukishinda tukiogelea kule forodhani, Aifola na kadhalika, wana-Kigoma kwao maji ya bomba ilikuwa anasa, barabara nyingi za vumbi tu. Haya hayakumhusu.
Mheshimiwa Zitto, hayo nilikuwa nakukumbusha mahaba ya wana-Kigoma kwa Dk. Kabourou na anguko lake, zama zake zimekwisha, sasa hivi yale mahaba wamekupa wewe, ikumbukwe kuwa hadi unachaguliwa hakuna jambo kubwa umelifanya katika Jimbo la Kigoma Mjini, isipokuwa ni imani kubwa walionayo juu yako tu.
Ndugu yangu Zitto, sasa ni wakati wako kuitafsiri imani waliokupa wanajimbo lako kivitendo, moja ya eneo la kufanya hivyo ni kupigania suala la viwanda, kwani wana-Kigoma wana kiu kubwa ya kuuona mkoa wao unapata viwanda ambavyo vitawapatia ajira vijana wengi waliokuwa wakiukimbia kutokana na ukosefu wa ajira, licha ya uwezo wa zao la michikichi kwa wingi, pia samaki aina ya migebuka na dagaa wake wengi tu, rasilimali muhimu kwa sekta hiyo.
Mheshimiwa Zitto, kwa kuwa suala la viwanda ndiyo ajenda kuu ya Rais Dk. John Pombe Magufuli na amekusifu sana pale bungeni kwa kitendo chako cha kutotoka nje kupinga uwepo wa Dk. Mohamed Shein wa Zanzibar, basi mdokeze akupe na viwanda pia pale Kigoma. Asikusifu tu bure, mbane.
Pili, huyu mdudu anayeitwa rushwa, huyu kaota mizizi sana katika ofisi zetu nyingi za Kigoma, huduma nyingi hutolewa mpaka uweke jiwe ili barua yako isipeperushwe na upepo (hela), suala hili limekuwa kero, pambana na huu uozo ndugu yangu Zitto, uzuri wa awamu hii tunaye Rais wa wanyonge – Dk. Magufuli, ungana naye.
Ubabaishaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji umekithiri. Imekuwa ikiahidi kuwasomesha watoto wa sekondari ila ulipaji wa hizo hela kwa shule kama inavyoahidi ni masikitiko matupu, ushahidi wa hili upo, kuna mwanafunzi alipewa barua na halmashauri hiyo ya kusomeshwa kidato cha tano na sita mwaka 2010 huko Arusha ila hadi anamaliza kidato cha sita mwaka 2012, hakuna kilicholipwa kwa mujibu wa mhasibu wa shule hiyo, mpaka sasa sina hakika kama hizo fedha zilishawahi hata kulipwa na hiyo halmashauri.
Mheshimiwa Zitto, halmashauri hiyo kwa sasa iko mikononi mwa chama chako cha ACT-Wazalendo, hebu fuatilia hili kwa undani, iweje halmashauri hiyo imuandikie mtu kuwa itamsomesha ila hela hizo ufikaji wake huko unakizungumkuti, na kama zinafika kwa nini inachukua miaka mingi hadi inafikia hatua mtu anajiandaa kulipa mwenyewe, hili si jambo jema hata kidogo.
Ndugu Zitto, kero nyingine zana wana-Kigoma ni suala la upatikanaji wa tiketi za treni kwa abiria, pamoja na kwamba siku hizi tiketi hizo hutolewa siku husika ya safari ili kudhibiti vitendo vya ulanguzi, lakini ili mtu kuipata hiyo tiketi kwa wepesi huna budi kulala kituoni.
Wapo wanaolala na watoto wadogo mno katika mbu na baridi kali hadi wanatia huruma, hii hali si afya kwa Taifa lenye ziadi ya miaka 50 ya Uhuru, ni kutowatendea haki wasafiri hao.
Huo ni mwanzo tu wa mchoko, subiri safari iianze ya hiyo treni ndiyo utaijua kero yake kiundani, badala ya siku mbili za safari, wakati mwingine huchukua hadi siku tatu, nne mtu hujafika mwisho wa safari yako, mara utaambiwa injini imeharibika, mara utasikia kuna sehemu reli imeharibika, ndani ya treni sasa kukanyagana, kusongamana ni suala la kawaida, hakuna staha ya ubinadamu kabisa.
Hili nalo ni suala la kulipigania kwa nguvu zako zote kwani huo ndiyo usafiri unaotumiwa na wana-Kigoma wengi, hasa katika suala la usalama na pia kulingana na nauli za basi ambazo ni ghali mno, na ukizingatia kipato cha wana-Kigoma wengi bado ni duni, hivyo hakuna budi kupambana na hili suala zima la usafiri wa treni.
Mheshimiwa Zitto, nafasi hainiruhusu kukuorodheshea matatizo yote kwa kina ila yapo mengi mno kama ya maji, umeme wa kutosha na kadhalika, hivyo basi ni wakati wako wa kuhakikisha sehemu kubwa ya matatizo haya yanatatuliwa ipasavyo, kiigizo unacho ni aliyekuwa rafiki yako, Deo Filikunjombe.
Nimalizie kwa msemo wa wazee wetu kuwa “wema huanzia nyumbani”, hivyo natumai nawe utautekeleza msemo huo kivitendo kwa wana-jimbo lako, hawatarajii kukuona upo kitaifa tu kutafuta umaarufu huku wao wakiugulia matatizo yao.
Mheshimiwa Zitto, tofauti na hivyo, wana-Kigoma Mjini hawatasita ‘kukufurusha’ kwenye sanduku la kura, kama ilivyokuwa kwa Dk. Kabourou, watu hawa huwa hawana mahaba ya kudumu na mtu, mwenzako Peter Serukamba anawajua vizuri.
Nakutakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yako.
Simu: 0658 010594