Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya

Watu watano wa familia moja katika kitongoji cha Nkangi, wilayani Chunya, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi kwenye kambi ya kuchunga ng’ombe wakiwa wamelala, huku wengine watano wakijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, alithibitisha kutokea kwa vifo hivyo, akisema tukio hilo lilitokea saa 8:30 usiku wa kuamkia jana.

Kamanda Kuzaga alisema tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Nkangi, watu hao watano wa familia moja ya mfugaji Masiganya Scania (39) wakifariki dunia.

Aliwataja waliofariki dunia katika tukio hilo ni Balaa Scania (28), Kulwa Luweja (17), Masele Masaganya (16), Hema Tati (10) na Manangu Ngwisu (18), wote wakazi wa kijiji cha Nkangi. 

“Katika tukio hilo, watu wengine watano walijeruhiwa ambao ni Gulu Scania (30), Manyenge Masaganya (13), Seni Solo (13), Paskali Kalezi (16) na Huzuni Kalezi (19),” alisema Kamanda Kuzaga.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana iliyoambatana na radi na kusababisha vifo vya watu hao na kujeruhi kadhaa.

Kamanda Kuzaga alisema majeruhi walikimbizwa katika Kituo cha Afya Isangawana kwa ajili ya matibabu na baadaye waliruhusiwa kurejea nyumbani baada ya hali zao kuimarika.