Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar wamefanya mazungumzo yenye lengo la kuanzisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kubadilishana uzoefu.

Akizungumza na ujumbe kutoka Tanzania Qatar , Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa nchini Qatar, AbdulAziz Ahmad Abdullah Al-Mahmoud alisema majukumu ya kisheria ya Wizara yake ya mazingira yanafanana na majukumu ya NEMC.

Alisema kutokana na hali hiyo kuna kila sababu ya kushirikiana hasa katika suala la usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Habibu Awesi Mohammed aliishukuru NEMC na Mamlaka za maji kutoka Dar es Salaam, Dodoma na Mtwara kwa kuonesha utayari wa kujifunza na kushirikiana na Qatar katika suala zima la uhifadhi wa mazingira na usimamizi bora wa mifumo ya maji safi na taka kwa ajili ya maendeleo ya sasa na ya vizazi vijavyo.

Wengine walioshiriki katika mikutano hiyo ni Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira kutoka katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mtwara kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kusimamia mifumo ya maji taka kwa ajili ya kulinda mazingira na viumbe kwa ujumla.

Vile vile ujumbe huo wa Tanzania uliweza kufanya mikutano na Taasisi nyingine ikiwemo Public Works Authority waliokuwa wanahusika na miundombinu na mifumo ya maji taka, Qatar General Electric and Water Cooperation wanaohusika na uzalishaji na usambazaji wa maji safi na umeme.

Mikutano mingine ambayo NEMC imeshiriki ni pamoja na Qatar Foundation ambao wameonyesha utayari wa kufanya ushirikiano nchini hasa katika eneo la uhifadhi wa Ziwa Victoria hususani katika kufanya tafiti kuhusu uondoshwaji wa gugu maji vamizi lililoshamiri kwa sasa linalosababishwa na ongezeko la virutubisho majini vinavyotokana na shughuli za kibinadamu.