Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani
Kusoma Kuandika na Kuhesabu (KKK) vinategemeana na endapo hutojua Kusoma Kuandika ama Kuhesabu basi mwendo wa elimu huwezi kuufikia.
Kutokana na hilo, sekta ya elimu mkoa wa Pwani imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuongeza nguvu mwaka 2023-2024 kupunguza changamoto hiyo hasa kwa watoto wa awali,darasa la kwanza hadi la saba ili kujiandaa na elimu nyingine za juu.
Ofisa elimu Mkoani Pwani, Sara Mlaki alieleza, moja ya changamoto iliyosababisha ufaulu wa darasa la Saba mwaka uliopita kushuka ni pamoja na baadhi ya wanafunzi kushindwa Kusoma Kuandika na Kuhesabu.
Alielezea kuwa, kati ya mikakati hiyo ni pamoja na mradi wa shule bora unachagiza kuleta matokeo chanya kwa kuhamasisha jamii, kutoa elimu, mafunzo, kupata vitabu kutoka taasisi ya elimu Tanzania na kutoa vifaa vya kufundishia kwenye vituo vya Utayari.
Sara alielezea kuwa, hatua hizo zimezaa matunda kwani Mkoa huo umekuwa wa nne upimaji Kusoma Kuandika na Kuhesabu (KKK) Kitaifa darasa la kwanza.
“Ngazi ya Halmashauri bora,Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo imekuwa ya tatu Kitaifa, hatua ambayo ni nzuri na ni matokeo makubwa ya jitihada na mikakati tuliyojiwekea kupunguza changamoto hiyo kwa watoto.”
Pamoja na hayo ,Sara alieleza mkoa huo umejipanga kupimana katika ngazi zote ili kuleta matokeo mazuri ya semina ambazo tayari walimu, maofisa elimu walianza kutolewa pamoja na kuongeza ufaulu na kuhakikisha wanafunzi wote wanajua kusoma kuandika na kuhesabu.
“Walimu 120 kutoka shule 40 walipewa elimu kwa siku tano lengo likiwa kwenda kuondoa KKK mashuleni,na kupewa mbinu mbalimbali “
“Walimu hao walienda kufundisha walimu wenzao wote na kuandaa zana za kufundishia hesabu ili watoto wa shule za awali,darasa la kwanza na la pili wapate uelewa”
Vilevile kuondoa tatizo la wanafunzi kutomudu stadi za kujua Kusoma Kuandika na Kuhesabu Sanjali na kuboresha Ufundishaji na ufunzwaji kwa madarasa ya awali na I na II.
Hata hivyo ofisa elimu huyo aliiasa jamii kujenga tabia ya kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao ngazi ya shule za awali hadi msingi ,ili kuwajengea uwezo wa kujua Kusoma ,Kuandika na Kuhesabu .
Alielezea, itasaidia kupunguza changamoto ya watoto kufeli elimu ya msingi kwa kutojua KKK.
Kwa upande wake ofisa elimu awali na Msingi Chalinze, Miriam Kihiyo alieleza wameshatoa mafunzo mbalimbali kwa walimu,ambapo kwasasa walimu hao wametengeneza zana za kufundishia.
“Kuna walimu wametengeneza hadi zana za vibao vya kusoma katika mti ilihali tu watoto wapate uelewa kirahisi kujua kusoma ama Kuhesabu”
“Wengine wanatumia mbinu za kuimba,kucheza na watoto na katika hesabu kutumia vijiti,visoda na kufundishana kwa mbinu mbalimbali ili kuelewa”alisema Kihiyo.
Ofisa Elimu msingi Halmashauri ya Mji Kibaha,Bernadina Kahabuka aliishukuru Serikali kwani tatizo la utoro na kutokujua KKK linapungua mashuleni.
Anaeleza, awali wazazi walikuwa hawashirikishwi hivyo kusababisha mahudhurio Kuwa madogo kwa wanafunzi,kwasasa mahudhurio ni mazuri na watoto wanapenda Kusoma.