Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani
Mkoa wa Pwani umekuwa mkoa wa sita kati ya mikoa 26 katika masuala ya lishe, ikiwa ni hatua nzuri ya kupunguza tatizo la udumavu , utapiamlo hususan kwa watoto.
Akizungumza katika kikao Cha lishe kimkoa ,Mkuu wa Mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge ametoa rai kuwa Halmashauri za mkoa huo ziongeze juhudi zaidi kutekeleza viashiria vya lishe na wasidorore kuridhika na mafanikio hayo.
“Mkoa umekuwa wa sita , Halmashauri ya Bagamoyo imekuwa ya tisa kati ya halmashauri 184 nchini,na hii ni kutokana na suala la lishe tulivyolibeba kuwa la kimkakati ndani ya mkoa,ukizingatia huu ni mkoa wa uwekezaji na viwanda ni vyema kuimarisha lishe kwa jamii ili kuboresha afya za wananchi.
“Tuongeze nguvu katika suala la lishe,tuvuke na kupanda tufikie zaidi ya asilimia 80” amesema.
Hata hivyo Kunenge aliwaasa wananchi kutunza mazingira na vyanzo vya maji pamoja na kupanda miti ya matunda.
“Leo tunazungumzia lishe,lakini kuna miti ya lishe,matunda tupunguze kukata miti,tuitunze na kuiihifadhi na tuzuie ukataji miti”amesisitiza Kunenge.
Vilevile mkuu huyo wa mkoa, aliwataka viongozi wa dini kutoa elimu ya lishe kwa jamii na wakati wa ibada ili kuondoa tatizo la lishe .
Ofisa lishe Mkoani Pwani,Pamela Meena alieleza tatizo wanalokabiliana nalo ni fedha zinatumwa kwenye mfumo kuna kuwa na ucheleweshaji ,mifumo kutofanya kazi ipasavyo na Hali ya udumavu kimkoa hadi 2022 ni asilimia 23.3 .
Kufuatilia taarifa hiyo , Kunenge alitoa maelekezo kwamba ,wale wote wanaohusika kuingiza data kwenye mfumo kama wanachangamoto wapewe mafunzo huku akiwataka waganga wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasogeza huduma ya vipimo vya utapiamlo hadi kwenye vituo vya afya.