Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

SERIKALI mkoani Pwani umeziagiza Halmashauri zote za Mkoa huo, kuhakikisha zinapanda miti angalau milioni 1.5 kila moja ili kufikia lengo la upandaji miti la mwaka 2024/2025 kwa asilimia 100.

Aidha kila shule iwe na kitalu cha matunda na kila taasisi kuwa na kitalu cha miche ya miti ili kutunza mazingira.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani,alhaj Abubakar Kunenge katika maadhimisho ya siku ya kupanda Miti Kimkoa yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Chalinze Mzee, halmashauri ya Chalinze.

Alieleza hadi sasa Mkoa umefanikiwa kupanda jumla ya miche 10,517,135, sawa na asilimia 77.9 ya lengo la miche milioni 13.5 kwa mwaka.

“Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Mkoa wa Pwani ulipanda miti 10,436,494 katika Halmashauri zote ikihusisha mashamba ya watu binafsi , vikundi na Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali sawa na asilimia 77.3 ” alifafanua Ndemanga.

“Hatuna sababu ya kushindwa kufikia asilimia 100,Tuhakikishe kila Halmashauri inapanda miti milioni 1.5 ili kufanikisha lengo letu la pamoja,” alisisitiza.

Vilevile Ndemanga alitoa wito kwa Maofisa Elimu wa Mkoa huo kuratibu kwa ufanisi zoezi la upandaji miti mashuleni.

Alieleza kwamba, kila mwanafunzi anapoanza shule ni lazima awe na mche wake wa mti, kama njia ya kuimarisha malezi ya mazingira na kuchangia lishe bora kupitia bustani za shule.

Katika maadhimisho hayo, miti 560 ilipandwa ikiwa sehemu ya juhudi za kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.

Pia aliwataka wataalamu wa mazingira kutoka ngazi za Mkoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ili kupata ushauri wa kitaalamu, hasa kuhusu changamoto ya mchwa inayoharibu miti baada ya kupandwa.

Nae, Katibu Tawala Msaidizi wa Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala, aliwaasa wananchi kuendeleza utamaduni wa kupanda na kutunza miti, na alipongeza ushiriki mkubwa wa wanafunzi katika shughuli hiyo, akisisitiza kuwa ni msingi wa kuwajenga kuwa mabalozi wa mazingira.

Kamanda wa TFS Kanda ya Mashariki, PCO Mathew Ntilicha, akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, alieleza jitihada hizo zinaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda mazingira na kuendeleza matumizi ya nishati safi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, ambaye pia ni Afisa Elimu Msingi, Miriam Kihiyo, aliwataka walimu wakuu kuhakikisha kila mwanafunzi anapanda na kutunza mti.

Alieleza kuwa Halmashauri hiyo ina zaidi ya wanafunzi 61,000 na aliomba TFS kutoa msaada wa dawa za kuzuia mchwa.

Afisa Misitu wa Mkoa wa Pwani, Pierre Protas Ntiyamagwa, alionya kuhusu uharibifu wa misitu unaofanywa na binadamu kupitia ukataji miti, uchomaji mkaa, uchimbaji mchanga na upasuaji mbao.

Maadhimisho ya Siku ya Kupanda Miti hufanyika kila mwaka tarehe 21 Machi, kwa mwaka 2025, yamebebwa na kaulimbiu:Ongeza Thamani ya Mazao ya Misitu kwa Uendelevu wa Rasilimali za Misitu kwa Kizazi cha Sasa na Kijacho.