Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Wananchi wa mkoa wa Pwani wamejitokeza kwa wingi kwenye vituo vya uandikishaji na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hali inayohofiwa kwamba baadhi ya watu huenda wasifikiwe kutokana na mwamko mkubwa ulioonekana.
Idadi hiyo kubwa ya watu imeanza kujitokeza tangu tarehe 17, 18, na 19 Februari, jambo ambalo limesababisha waandishi wasaidizi katika baadhi ya vituo kuhemewa.
Katika kituo cha uandikishaji cha Shule ya Msingi Mloganzila, imeshuhudiea watu wengi wakiwa katika foleni kutimiza haki yao ya kikatiba ya kujiandikisha kuwa wapiga kura.

Wananchi waliokuwa katika foleni, akiwemo Wahida Jamal, alieleza kuwa alifika kituoni hapo tarehe 18 Februari tangu saa 5 asubuhi, lakini alishindwa kujiandikisha hadi saa 12 ambapo kituo kilifungwa kwa mujibu wa utaratibu wa nchi. Wale waliobaki, zaidi ya 30, walilazimika kupokea namba na kurudi tena tarehe 19 Februari.
Hofu yake ni kwamba ana shughuli za kibiashara na ameshapoteza muda mwingi, hivyo anahofia endapo kutakuwa na ongezeko kubwa la watu siku ya mwisho, litakuwaje.
Juma Rashid na Reuben walisema, wanafunzi wengi wamejitokeza, na ingawa ni haki yao kwa wale wanaofikia umri wa miaka 18, idadi ya watu imeongezeka.
Hata hivyo, imeshuhudiwa kwamba mmoja wa madereva wa bodaboda kutoka Kibamba alifika kituoni hapo kujiandikisha, lakini alipotoka kubadili shati na kurudi tena, alibainika na kukatiliwa kujiandikisha kwa mara ya pili, jambo ambalo ni kosa la kisheria.
Katika baadhi ya vituo vya kata ya Mailmoja na Tangini, mkazi wa eneo hilo, Hassan Abdallah, alieleza kwamba hatua za dharura za kuziba mapungufu kwenye vituo vya uandikishaji zingechukuliwa mapema tangu ilipobainika ongezeko kubwa la watu na changamoto za mtandao na vifaa ili kudhibiti wingi wa watu.
“Watu wanagombania foleni, inafikia hatua utu unaondoka. Wanashindwa kupisha wazee na wenye watoto kwa sababu kila mmoja anataka kuwahi,” alisema Hassan.

Hassan aliongeza kuwa, kiukweli mwaka huu vituo vya uandikishaji ni vichache na waandishi wasaidizi ni wachache, Hali inasababisha watendaji wa vituo kuhemewa kwani kuna mpiga picha mmoja na muandikaji maelezo mmoja ama wawili.
Kwa upande wake, mratibu wa zoezi hili mkoani Pwani, Gerald Mbosoli, alifafanua kuwa zoezi limeenda vizuri .
Alisema penye mafanikio hakukosi changamoto, katika changamoto kubwa iliyojitokeza ni Watanzania wengi kuwa na tamaduni za kuchelewa kujitokeza na kutegemea kujiandikisha mwishoni mwa zoezi kama hili.
Mbosoli alisema ,anatembelea vituo kwa kushirikiana na watendaji wengine , na wameona mwamko mkubwa hivyo wanalifanyia kazi kwa kushirikiana na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
“Katika maeneo ambapo kuna wingi wa watu, tunaangalia uwezekano wa kuongeza mashine za ziada ili kuondoa tatizo hili,” alisema.
Mbosoli alieleza pia kuwa changamoto nyingine ni kwamba mkoa wa Pwani uko jirani na Dar es Salaam, ambapo watu wengine wanakuja kujiandikisha wakati zoezi katika Dar es Salaam bado halijaanza.
Kuhusu ombi la kuongeza muda, Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Suleiman Mtibora, hivi karibuni alieleza kuwa zoezi hilo linapangwa kufanyika kwa siku saba na hakuna mpango wa kuongeza muda.
Kwa upande wa vituo vya uandikishaji, Mtibora alieleza kuwa mkoani Pwani kuna vituo 1,913, ikiwa ni ongezeko la vituo 179 ikilinganishwa na 1,734 vilivyokuwepo mwaka 2019/2020.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulianza tarehe 13 Februari hadi 19 Februari 2025 katika mikoa ya Tanga na Pwani kwa siku saba.
Zoesi hili linatarajiwa kuandikisha wapiga kura wapya 431,016 na baada ya kumalizika, mikoa hiyo itakuwa na wapiga kura 2,727,318.