Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaji Abubakari Kunenge, ametangaza kuwa mkoa wa Pwani utazindua rasmi Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ‘Samia Legal Aid’, tarehe 24 Februari 2025.

Uzinduzi huo utafanyika katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Mailimoja, Kibaha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kunenge alisema kampeni hiyo itaanza rasmi tarehe 25,februari itakuwa kwa siku Tisa na itakamilika march 5 ,2025.

Alisisitiza , wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi siku hiyo mapema majira ya asubuhi.

Alitoa wito kwa wananchi wenye malalamiko mbalimbali kupeleka matatizo yao kwa ajili ya msaada wa kisheria.

“Wananchi wote wenye malalamiko wajitokeze kupeleka malalamiko yao yanayohitaji msaada wa kisheria, na nina imani watapata msaada,” alisema Kunenge.

Amesema huduma hii itahusu malalamiko ya masuala ya ndoa, mirathi, ardhi, na mengineyo, ambapo wananchi wote watapata nafasi ya kusikiliza na kushughulikiwa.

Huduma hii inatolewa na Wizara ya Katiba na Sheria, na inaimarisha juhudi za serikali kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia tayari imefanyika katika mikoa 19 ya Tanzania, na Pwani itakuwa mkoa wa 20.