Rais Vladimir Putin amekataa usitishaji vita wa mara moja na kamili nchini Ukraine, akikubali tu kusitisha mashambulizi kwenye miundombinu ya nishati, kufuatia mazungumzo yake na Rais wa Marekani Donald Trump.

Kiongozi huyo wa Urusi alikataa kutia saini usitishaji vita wa mwezi mzima ambao timu ya Trump iliafikia hivi majuzi na Ukraine nchini Saudi Arabia.

Amesema mapatano ya kina yanaweza tu kufanya kazi ikiwa msaada wa kijeshi wa kigeni na ushirikiano wa kijasusi na Ukraine utasitishwa.

Washirika wa Ukraine wa Ulaya hapo awali walikataa masharti hayo. Mazungumzo ya Marekani na Urusi yanatarajiwa kuendelea Jumapili huko Jeddah, Saudi Arabia, mjumbe wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, amesema.

Katika vita hivyo vilivyodumu kwa miaka mitatu, Urusi hivi karibuni imekuwa ikilikomboa eneo lake la Kursk ambalo lilichukuliwa na uvamizi wa Ukraine miezi sita iliyopita.

Matokeo hayo ya wito wa Jumanne wa makubaliano ya Trump-na Putin ni sawa na kujiondoa katika nafasi ya Marekani kutoka pale iliposimama wiki moja iliyopita, ingawa viongozi hao wawili walikubaliana kwamba mazungumzo zaidi ya amani yatafanyika mara moja katika Mashariki ya Kati.

Wakati wajumbe wa Marekani walipokutana na wenzao wa Ukraine mjini Jeddah Jumanne iliyopita, waliishawishi Kyiv kukubaliana na pendekezo lao la usitishaji vita wa “haraka” wa siku 30, ardhini, angani na baharini.

Rais Volodymyr Zelensky, ambaye aliwasili Helsinki, Finland, kwa ziara rasmi siku ya Jumanne muda mfupi baada ya mazungumzo ya Trump na Putin kukamilika, alisema Ukraine iko tayari kwa wazo la makubaliano ya kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati, lakini anataka maelezo zaidi kwanza.

Baadaye alimshutumu Putin kwa kukataa usitishaji mapigano kufuatia msururu wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi. Miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni hospitali ya Sumy, na vifaa vya umeme huko Sloyansk, alisema kiongozi huyo wa Ukraine.