W

iki iliyopita, familia ya mpira wa miguu katika Bara la Afrika ilipata msiba mzito kwa kumpoteza nguli wa soka wa Nigeria, Stephen Keshi, ambaye ana historia ndefu nchini humo.

Keshi alikuwa mchezaji katika miaka ya 1990 pamoja na Kocha wa kikosi cha ‘Super Eagles’ ambacho kilichukua Kombe la Afrika (AFCON) 2013.

Ni majonzi kwa wanafamilia yote barani Afrka. Unaweza usiamini lakini huna budi kuamini baada ya mitandao mbalimbali kuelezea kifo chake kutoka Nigeria.

Ilikuwa Jumatano iliyopita asubuhi, mitandao mbalimbali nchini Nigeria imeripoti kuwa Keshi amefariki kutokana na maradhi ya shambulio la moyo na umauti ulimkuta nchini Benin katika mji wa Edo State.

Nahodha huyo umemkuta umauti akiwa na miaka 54 katika uhai wake ambao aliishi hapa duniani.

Keshi alizaliwa Januari 23, 1962 katika kitongoji cha Azare, Bauchi State nchini Nigeria, na aliitumikia timu ya taifa kama beki wa kati kuanzia mwaka 1981 hadi 1995.

Lakini, Keshi hakuacha kujikita katika soka. Alianza harakati za soka kwa kuanza kufundisha soka ndipo alipokuja kubahatika kuifundisha Nigeria, ambayo iliingia kwenye historia.

Kwenye maisha yake ya soka, Keshi alitumikia kwa ngazi ya klabu akiwa Ubelgiji, kabla ya kuamua kuishi Marekani na kujikita katika ukocha.

Timu ambazo Keshi amewahi kuzichezea ni Lokeren, Anderlecht, RC Strasbourg, RWDM, CCV Hydra, Sacramento, Scorpions na Perlis FA, lakini pia alitumia muda akiwa Anderlecht ya Ubegiji.

Keshi aliandika historia kuwa kocha wa kwanza mzawa kuipa Nigeria Kombe la Afrika, na wa pili kutwaa Kombe la Afrika akiwa kama kocha na mchezaji pia.

Mtu wa kwanza kufanya hivyo kwa hapa Afrika, alikuwa ni Mahmoud El-Gohary wa Misri mwaka 1998.

Mbali na kufundisha timu kubwa ya taifa, ‘The Big Boss’ aliwahi kuinoa timu ya vijana ya Nigeria mwaka 2001 katika michuano ya vijana Afrika, vilevile kufuzu kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana mwaka 2001, lakini hakufanikiwa kufuzu.

Mwaka 2004 hadi 2006, Keshi aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Togo, na kufanikiwa kuipeleka michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 kwa mara ya kwanza kabisa.

Licha ya kuiwezesha Togo kufikia hatua hiyo, lakini alitimuliwa kabla ya michuano hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Otto Pfister.

Mbali na Togo na Nigeria, amewahi kuifundisha Mali mwaka 2008 kwa mkataba wa miaka miwili, lakini alitimuliwa mwaka 2010 baada ya timu hiyo kufanya vibaya katika hatua ya makundi kufuzu michuano ya Afrika.

Mwaka 2011, Keshi aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Nigeria na ilifanikiwa kufuzu michuano ya Afrika mwaka 2013 na kuchukua taji kwa kuwafunga Burkina Faso bao 1-0. Lakini, baada ya michuano hiyo kumalizika Keshi alijiuzulu na akarejeshwa tena.

Aliiongiza tena Nigeria katika michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka 2013 na akapata ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Haiti, akapoteza 2-1 dhidi ya Uruguay kabla ya kufungwa tena na Hispania mabao 3-0 na kutupwa nje kwenye mashindano hayo.

Novemba 16, 2013  Keshi alifanikiwa kuipeleka Nigeria kwenye michuanio ya Kombe la Dunia baada ya kuiondosha Ethiopia kwa wastani wa mabao 4-1 kwenye mtoano.

Hivyo basi, Keshi aliweka rekodi katika soka la Afrika kwa kuwa kocha pekee wa Kiafrika kufanikiwa kuzipekeka timu mbili za Afrika – Nigeria na Togo – kwenye Kombe la Dunia.

Nahodha huyo ambaye aliitumikia Nigeria kwa kiwango bora, aliweza kuipeleka Nigeria hatua ya mtoano kwenye Kombe la Dunia mwaka 2014 ambapo walitolewa na Ufaransa kwa kufungwa mabao 2-0.

Keshi alikuwa katika wakati mgumu baada ya kushindwa kuipa matokeo mazuri Nigeria kwenye kufuzu michuano ya Afrika mwaka 2015.

Baada ya matokeo hayo mabovu, alitishia kujiuzulu endapo wangeendelea kumpa mashinikizo kutoka kwa watu ambao aliwashutumu kuwa wanamhujumu.

Keshi aliachana rasmi na Nigeria Julai 2015 baada ya mkataba wake kwisha na waajiri wake (Chama cha kabunbu Nigeria-NFF) kutokuwa na mpango wa kumpa mkataba mpya.

Baada ya kuacha kufundisha timu hiyo, Keshi alijikita katika mambo yake binafsi na mwaka 2015 alifiwa na mkewe aliyekuwa na maradhi ya kansa. Alidumu naye kwa miaka 33. 

Ni nyota wa tano kuiaga dunia kutoka katika kikosi cha Nigeria

kilichotingisha sana mwaka 1994, akiungana akina Thompson Oliha, Radhid Yekini, Uche Okafor na Wilfred Agbonavbare.

Kikosi hicho kilikuwa moto na ndicho kilicholeta chachu ya soka la Nigeria na vijana wengi kuanza kupenda mpira wa miguu kutokana na kuona fursa za kutoka zilikuwa wazi.

Nigeria kwa sasa ina vijana wengi wanaocheza soka barani Ulaya. Keshi ‘Big Boss’ ameacha watoto wanne pamoja na mama yake mzazi ambaye ni mzee sana.