Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Mhashamu Stephano Musomba ametoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi na kuhakikisha wanajiandikisha kushiriki Pugu Marathon 2025 itakayofanyika Mei 31, 2025 katika viwanja vya Hija Pugu Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Ameyasema hayo leo Januari 21, 2025 wakati wa Mkutano na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, kuelekea Uzinduzi wa Pugu Marathon awamu ya tatu, uliofanyika katika Ukumbi wa Kardinali Pengo uliopo Kanisa kuu la Mtakatifu Joseph Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Amesema kuwa miongoni mwa malengo ya Pugu Marathon awamu hii 2025 ni pamoja na kuendeleza kituo cha Hija Pugu pamoja na kujenga Afya ya kila mmoja kupitia mazoezi.

Amefafanua kuwa kupitia mbio hizo kutakuwepo na shughuli mbalimbali zikiendelea ikiwemo utoaji wa huduma za Afya na majitoleo ya matendo ya huruma kwa kutoa Damu kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu.
Ameongeza kuwa, mbio hizo za msimu zitakuwa za umbali wa kilometer 2.5km, 5km, 10km na 21 Km,malengo ya mbio hizo ni pamoja Kuendeleza kitua cha hija Pugu,Kuendeleza shule ya sekondari Pugu kwa kuboresha maktaba na nyumba aliyoishi Hayati Mwalimu Julius Nyerere,Kufanya matendo ya huruma katika hospitali zetu za Mkoa wa Dar es Salaam na Kujenga afya zetu kupitia michezo.
Mhashamu Askofu Musomba, amesema mbio hizo ni za msimu wa tatu ambapo msimu wa pili mwaka 2024 waliweza kufanikiwa kupata kiasi cha sh.Milion 160 kutoka kwa wakimbiaji na wafadhili mbalimbali.
”Mtakumbuka kwamba Pugu Marathon imefanyika kwa misimu miwili yaani mwaka 2023 na 2024,huku mwaka huu 2025 itakua ni msimu wa tatu wa mbio hizo,tunawashukuru sana kwa majitoleo yenu.
”Katika majitoleo haya fedha hizi zitatumika katika maandalizi ya msimu wa tatu 2025 na akiba iliyobaki leo tunakabidhi Milioni 2 kwa ajili ya kununua vitabu kwa ajili ya shule ya sekondari Pugu,Milioni 3 tutatoa kwa ajill ya matendo ya huruma katika kituo cha afya Pugu Kajiungeni kwa ajili ya ununuzi wa mashuka na Milioni 10 zitatolewa kwa ajili ya kuendeleza kituo cha hija Pugu,” amesema.
Amesema gharama ya mbio hizo ni kiasi cha sh. 30,000 kwa mbio zote kwa maana ya umbali wa Kilomita 2.5,5,10 na 21km ambapo washiriki watapatiwa Tshirt ya kukimbilia,Namba ya kukimbilia na pini za kubandikia pamoja na maji na matunda kwa wakimbiaji.
“Ninawaalika waumini na watu wote wenye mema kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizi kwani pamoja na kujenga afya pia itasaidia kuendeleza Kituo cha Hija,” amesema.
Hata hivyo katika kuhakikisha kila mmoja analinda Afya yake, ametoa wito kwa jamii kuwa na Utamaduni wa kufanya mazoezi ili waweze kulinda afya zao na jamii inayowazunguka.
“Kila mtu katika Jamii anapofanya mazoezi inamsaidia kujiimarisha katika Uhai na inaongeza weledi katika utendaji kazi wake,” amesema Askofu Musomba.
Pugu Marathon ni mbio ambazo ni za hisani na zinafanyika kila mwaka katika kuhakisha wanawezesha kituo cha Hija cha Pugu na kukiendeleza na kuwa kituo kikubwa kwa siku zinazokuja ili kukuza imani ya kizazi kijacho.