Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kongwa

Wasichana 194 waliorejeshwa shuleni kutokana na kupata ujauzito wameendelea na masomo kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP-AEP) mkoani Dodoma.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Mayeka wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo rasmi yaliyofanyika wilayani Kongwa.

Mayeka ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati wa maadhimisho hayo alisema kuwa kurejeshwa shuleni kwa wanafunzi hao ni kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuwajali wasichana waliokatisha masomo.

“Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kuwajali wasichana ambao hawakuweza kupata elimu ya sekondari kwenye mfumo rasmi kwa sababu mbalimbali ameamua kuwarejesha kupitia mpango wa SEQUIP-AEP,” alisema.

Aliongeza, “Mkoa wa Dodoma tumefanikiwa kuwarejesha shule wanafunzi wa kike 194 kupitia programu hii na tunaendelea kuwabaini na kuwasajili”.

Aidha, aliwaasa mabinti wote ambao kwa bahati mbaya walikatiza au kukatizwa masomo kwa sababu mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo iliyotolewa na Rais Samia kujiendeleza kwani elimu ndiyo silaha kuu ya ukombozi wa binadamu, hivyo jamii isaidie kuwaibua wanafunzi walioacha shule.

Naye Ofisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi Mkoa wa Dodoma, Borase Chibura alisema kupitia utekelezaji wa Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) wananchi hawafundishwi tu Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) bali pia stadi za maisha ili kuwawezesha kujikwamua kimaisha.

“Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa miwili nchini inayotekeleza programu ya MUKEJA kupitia vituo viwili vilivyopo katika halmashauri mbili za Kongwa na Kondoa Mji hali inayoongeza fursa ya upatikanaji wa elimu kwa watu wazima,” alisema Chibura.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dk Omar Nkullo, Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kongwa, Sudi Abdul aliwaomba wanavikundi vya ujasiriamali kutumia mikopo ya halmashauri kuomba fedha kwa ajili ya kuboresha shughuli zao na pia jamii idumishe elimu ya watu wazima ikiwa ni pamoja na kujifunza stadi mbalimbali za ufundi na uzalishaji mali.

Kwa upande wake, Mshauri wa Maendeleo ya Uwezo, Matteo Mwita alitoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza ili kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu.