Profesa Issa Shivji, hivi karibuni alihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Azam, kuhusu siku 50 za uongozi wa Rais John Magufuli. Ufuatao ni mtazamo na ushauri wake kwa Serikali ya Awamu ya Tano
Ni kweli kwamba ni siku 50 tangu Rais Magufuli aingie madarakani. Kuna mambo alifanya kwa vitendo bila shaka yamegusa sana nafsi za wananchi hasa kuonyesha kwamba anawajali wananchi wa hali ya chini na pia kwamba atahakikisha watendaji wanawajibika kwa vitendo vyao.
Nafikiri hili lilikuwa na umuhimu wake kuonyesha kwamba mambo hayataenda kama ilivyozoeleka katika awamu yake; na kwamba awamu yake ya tano ni kitabu kipya tofauti na awamu tatu zilizopita. Sitaki kulinganisha na awamu ya Mwalimu Nyerere, lakini baada ya Mwalimu. Kwa hiyo hatua alizochukua nafikiri ina-symbolize ukweli huo.
Lakini pia katika kipindi hiki ametoa hotuba mbili. Hotuba moja aliyotoa pale bungeni alipokuwa anazindua Bunge. Katika hotuba ile ingawa ilikuwa nzuri tu, alichofanya aliorodhesha maovu ya jamii yetu na utawala wetu na jinsi atakavyokabiliana na maovu haya na matatizo. Aliyaita malalamiko ya wananchi.
Lakini hotuba ambayo ilinifanya mimi kama mwanazuoni msomi, ambayo ilikuwa inaonyesha mwelekeo wake hasa anadhamiria kwenda wapi na anaongozwa na dira gani nafikiri ilikuwa ni hotuba aliyotoa kwa wafanyabiashara tarehe 3 Desemba.
Hotuba ile inaelekea haikuandikwa na mimi niliona gazeti moja limechapisha. Gazeti la JAMHURI. Kwangu mimi kama msomi, hotuba ile ina umuhimu wa kipekee, na kwa kiasi fulani inanishangaza kwamba haijajadiliwa sana kwa sababu nadhani bado watu wapo kwenye jazba (mshangao) wa vitendo alivyofanya.
Mimi kwa upande wangu ningependa kuchukua nafasi hii kuangalia kwa undani kidogo hotuba hiyo aliyotoa kwa wafanyabiashara kwa sababu mimi naona hotuba hii inatupatia mwelekeo wake na mtazamo wake.
Bado haijaiva, inawezekana bado inapikwa, lakini kwa kiasi fulani nafikiri tunaweza tukaainisha anakotaka kuelekea katika awamu yake. Na hapa baada ya ufanya uchambuzi wa hotuba ile mimi naona kuna mambo matatu muhimu amegusia.
Kwanza, ninavyoona mimi kwa uchambuzi wangu ana mwelekeo wa kujenga uchumi wa kitaifa-National Economy. Baadaye nitaeleza sifa za national economy.
Ya pili, anataka kudhibiti uporaji wa rasilimali na mtaji wa nchi, hasa rasilimali zinazoporwa na kusafirishwa kwenda nje bila wananchi kufaidika.
Na tatu, ameonyesha haridhiki na sekta ya fedha. Haya mambo matatu mimi nimeona kwenye hotuba yake.
Ningependa kueleza. Kwanza tujikumbushe kwamba alikuwa anazungumza na wafanyabiashara. Alikuwa anazungumza na sekta binafsi, alikuwa anazungumza na wawekezaji wa ndani.
Kwanza amesisitiza kwamba uwekezaji wa ndani au wafanyabiashara wa ndani wana nafasi yake katika kujenga uchumi wetu na nchi yetu na yeye Serikali yake itashirikiana nao. Lakini hakumalizia hapa tu; alipokuwa anazungumza na hawa wawekezaji nafikiri aliainisha sifa za hao wawekezaji wa ndani maana yake nini kutoka kwa hao wawekezaji wa ndani au tuite kwa jina lake-mabepari wa ndani.
Yeye nimeona katika hotuba yake amerudia rudia kusisitiza kwamba angalau bepari yeyote popote pale duniani anaongozwa na kuchuma faida. Hii ni kweli yenyewe, lakini yeye angependa kuona hao mabepari pia wanakuwa mabepari wazalendo- wa kitaifa. Watakuwa wanatanguliza maslahi ya Watanzania mbele.
Kwanini nasema yeye alikuwa anasisitiza kwamba angependa kuona tabaka hili liwe tabaka la mabepari wa kitaifa; mabepari wa kitaifa wana sifa tatu au nne hivi na yeye ingawa hakuweka katika maneno haya, amegusia.
Moja ni kwamba hao wanajikita kwenye uzalishaji, siyo uchuuzi tu, yaani kununua bidhaa na kuuza kwa bei zaidi. Siyo wachuuzi hao. Hao ni wazalishaji. Wanawekeza kwenye sekta ya uzalishaji. Hii ni moja. Na hii ni muhimu kwa sababu wengi ambao tunawaita wawekezaji hasa wa ndani –wafanyabiashara hawajajikita kwenye uzalishaji. Wamejikita zaidi kwenye kuchuuza au kuuza bidhaa. Mwalimu Nyerere aliongea vizuri sana jambo hili mwaka 1989. Mwalimu alikuwa anazungumza wakati ule na wafanyabiashara na watendaji wakuu wa Serikali. Ninavyoona hotuba hii ya Rais Magufuli kuna mambo ambayo unaweza kuyalinganisha na yale aliyozungumza Mwalimu mwaka 1989 pamoja na yale alikuwa anazungumza sana Marehemu Sokoine (Edward) mwanzoni mwa mwaka 1980. Haya yote yamejitokeza katika hotuba ya Rais Magufuli.
Kuhusu wazalishaji na wachuuzi, Mwalimu alisema, na ningependa kumnukuu hapa kwa sababu ameeleza vizuri tu. Alikuwa anazungumzia kwamba sisi nchi zetu uchumi wetu tegemezi tunauza tu bidhaa za wakubwa. Anasema: “Kwa Coca Cola kwa sababu Wamarekani wao wana nguvu sana kwa Coca Cola, Marekani sasa wanataka wote tuwe tunakunywa Coca Cola. Ndugu Mengi (Reginald), mkipenda msipende mtatuuzia Cola Cola, basi Coca Cola inauzwa tu.” Mwalimu anasema. Anaendelea: “Kwa hiyo tunajivunia ule ugonjwa. Tunajivunia ule ugonjwa wala hatuoni haya. Unaparedi silaha za wakubwa, unaparedi madege ya wakubwa, unaparedi bidhaa za wakubwa, unaparedi ma-Coca Cola ya wakubwa, na unajivuna tu unasema ‘sisi tumeendelea’.” Mwalimu huyo mwaka 1989.
Na Rais Magufuli, kwa maneno yake pia anasisitiza uzalishaji wa bidhaa. Hii ni sifa mojawapo na amegusia. Sifa nyingine ya tabaka hili ni nini? Anatumia malighafi ya nchi ili kutengeneza bidhaa kwa ajili ya mahitaji ya soko la ndani. Ni hili tabaka tunalozungumzia. Anatumia malighafi, anawekeza kwa mfano kwenye viwanda, anatengeneza bidhaa ili kukidhi mahitaji/soko la ndani. Ndiyo maana hasa ya kiini cha kujenga uchumi wa kitaifa. Hii ni sifa ya pili.
Kwanini nasema Rais Magufuli ana mwelekeo huu; ametoa mifano mitatu au mine hivi. Kwanza, ametoa mfano wa ngozi kwamba nchi ya Tanzania ina mifugo mingi katika Bara la Afrika, nafikiri ni nchi ya pili baada ya Ethiopia kuwa na mifugo mingi, lakini hatuna viwanda vya ngozi. Hatutumii mifugo yetu kuwa na ngozi na kutengeneza viatu kadri ya soko letu la ndani. Kama unavyokumbuka inawezekana vijana wamesahau-tulianza hiyo. Tulikuwa na viwanda vya ngozi huko Morogoro, lakini baada ya kuingia kwenye mfumo huu wa ubepari mamboleo na kufungua milango, viwanda vyote vilikufa na vingine ambavyo vilibinafsishwa sasa ni ma-godown (maghala). Rais Magufuli amegusia hilo.
Mfano wa pili anaotoa ni kwamba yale yanayotokana na mifugo, kwa mfano maziwa na mengine…samli, siagi, na kadhalika hatutengenezi sisi hapa hapa kwetu kwa ajili ya soko letu.
Mfano mwingine aliotoa ni wa mbao. Magogo tuna mapori hapa, lakini magogo yanasafirishwa kwenda nje. Sisi hatutumii magogo haya kutengeneza furniture (samani) kwa ajili ya soko la ndani. Furniture yetu tunanunua kutoka nje, na utakumbuka kwamba amepiga marufuku. Furniture katika ofisi za Serikali zote lazima zinunuliwe hapa hapa. Unaona!
Mfano wa tatu anaotoa ni ule wa samaki. Ameelezea vizuri tu kwanini sisi tusiweze ku-process (kusindika) samaki zetu kwa ajili ya soko letu. Ameeleza hapa na ningependa kunukuu kwa sababu ameweka vizuri tu faida ya kuwa na mwelekeo kama huu.
Anasema: “Mtu yule anayevua samaki kwenye maji marefu kule baharini na kuleta hapa ndani akawa anawa-process mwenyewe kwenye viwanda vyake, anasafirisha hao samaki, anapeleka hata Ulaya watu wetu wa hapa wakapata ajira, Serikali ikapata mapato yake na mabaki ya samaki yakatumika hata kutengeneza chakula cha kuku, huku naye akijipatia fedha zake na maisha yakaendelea.”
Hiyo anawambia wawekezaji wa ndani hawa ‘kwanini nyie msiweze kufanya kazi hiyo badala ya kuachia watu wa nje wavue samaki wetu na kupeleka nje?’ Unaona hapo kuna mwelekeo wa zile sifa za mabepari wa ndani- anazungumza kujenga uchumi wa kitaifa.
Kutokana na mifano hii anayotoa, ninavyoona mimi mwelekeo wake juu ya mfumo wa uchumi ni kujaribu kuchukua hatua za makusudi kabisa kujenga uchumi wa kitaifa. Na katika hili anasisitiza kwamba nia ya wawekezaji wa ndani ni kuwa na sifa hizo za mabepari wa kitaifa, ndiyo maana yake kusema kwamba wekeni maslahi ya Watanzania mbele, ndiyo maana yake. Msiwe wachuuzi tu-kuchuma faida haraka haraka.
Siku 50 ni chache sana kuwa na mwelekeo kwa vitendo kwa sababu ndiyo maana nimejikita kwenye hotuba yake. Hotuba hii ndiyo inaonyesha mwelekeo. Lakini sasa atafanyaje? Atachukua hatua gani katika mfumo wenyewe ili kuelekea huko-kujenga uchumi wa kitaifa; na baadaye mimi nitazungumzia. Kama kweli tuna dhamira ya kujenga uchumi wa kitaifa kunakuwa na masharti yake. Hii nitaizungumza baadaye.
Lakini kwanza inaonyesha kwamba nia yake ni kujenga uchumi wa kitaifa na katika hili ndiyo alikuwa anawambia wawekezaji wa ndani kwamba muwe na sifa ya kusaidia kujenga uchumi wa kitaifa, na mkifanya hivyo, sisi Serikali tutawasaidia, tutawawekea mazingira.
Hotuba yake amesema atafanyaje. Kwa mfano amezungumzia suala zima la kuweka mazimgira, kupunguza kodi za kero hasa kwa wafanyabiashara wa kati na wafanyabiashara wadogo. Naye pia ameweka masharti mengine na ndiyo sifa mojawapo kwamba huwezi ukakwepa kulipa kodi. Hicho ndicho nitazungumza baadaye kidogo.
Sehemu ya pili, ameonyesha pia kwamba anakasirishwa na uporaji. Na katika hili pia kwa kiasi fulani ameonyesha kwamba wako mabepari wazawa ambao siyo mabepari wa kitaifa. Kwa Kiingereza tunawaita Comprador, isipokuwa yeye mwenyewe hakutumia neno hili wala hakupanua sana, lakini kulikuwa na jambo moja amezungumzia na ningependa kwa kiasi fulani inaonyesha kwamba yeye anasisitiza tabaka la mabepari wa kitaifa lisilo tabaka la mabepari wachuuzi wanaotaka kupora rasilimali na kutengeneza faida haraka haraka kwa kushirikiana na waporaji wa nje.
Kwa mfano, anasema: “Nafahamu Mwanyika alikuwa hapa (Mwanyika ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Accacia), nafahamu Mwanyika yuko hapa, kwenye madini kule kuna ndege zinatua kila siku. Sina uhakika vile vyote vinavyobebwa na ndege hizo tunavijua, lakini kwa kuwa nafahamu wewe ni Mbena au Mhehe mna tabia ya kujinyonga kila mambo yanapoharibika, basi simamia haya mambo vizuri.”
Hii nayo naona ni ishara kwamba ‘mimi sitaki mabepari comprador ambao watashirikiana na waporaji wa nje na kufaidika wao wenyewe.’
Kwa mfano wale ambao wameng’ang’ania sana kwamba wazawa wapewe vitalu vya gesi ili wao sasa watakuwa na ubia na watu wa nje. Sasa kama ni hivyo kwa nini Serikali yenyewe isiwe na ubia na watu wa nje ambao itaweza kudhibiti. Badala ya kuwekeza kwenye viwanda, kujenga ajira, kama nilivyosema-kutumia malighafi ya ndani, ukidhi mahitaji ya ndani kwanini huyu mwekezaji ang’ang’anie sana apate kitalu kwa sababu yeye ni mzalendo wakati yeye hazalishi chochote, atafunga ubia na watu wa nje ambao watakuja kupora rasilimali zetu.
Na hii pia amezungumzia kwa sababu sifa mojawapo amesisitiza sana Mheshimiwa Magufuli, ni kwamba uwekezaji katika sekta ya uzalishaji hasa viwanda viweze kujenga ajira. Kwa hiyo sifa mojwapo kwamba wewe ni mwekezaji utaweka mitambo ya aina gani, kwa mfano, ili kuhakikisha kwamba unaweza ukapanua ajira. Na hilo amezungumzia Mheshimiwa akizungumza na Mwenyekiti Mengi. Alizungumza suala la ajira na wakati anatoa mfano huu: “Meshimiwa Mengi alikuwa anajisifia kwamba sekta ya viwanda nchini kwa sasa imetoa mchango mkubwa wa ajira kwa Taifa hili kwa kuajiri watu hao laki moja.” Sasa Rais Magufuli anasema ‘katika idara niliyokuwa mie, Idara ya Ujenzi kulikuwa na ajira watu milioni 1.3. Idara moja tu ya Serikali, sasa yeye kwenye viwanda 400 mmesema mmejenga ajira 100,000 tu kwa kweli anasema hiyo ajira ya aina gani hiyo. Na ukweli ndivyo ulivyo.
Yaani tulikuwa na wafanyakazi walioajiriwa katika sekta ya viwanda zaidi ya 300,000 kabla ya ubinafsishaji, leo hii tunajisifia kwa kuwa na ajira 100,000. Hata wafanyakazi nyumbani ni zaidi ya mara nne ya hawa; sasa hapo hujafanya chochote ukijisifia kuwa umetengeneza ajira watu 100,000 tu. Kwa hili pia amesisitiza sana kwamba uwekezaji katika sekta ya uzalishaji hasa viwanda ujenge ajira kwa ajili ya vijana wetu.
Jambo la tatu: Sekta ya fedha. Yeye hakupanua sana, lakini nimekuta hapa jambo moja amezungumzia ambalo lilikuwa wazi lakini halizungumziwi. Kasema tusisahau wakati ule tunabinafsisha, tulibinafsisha sekta ya fedha pia. Mabenki, bima tukabinafsisha, na anasema hapa Mheshimiwa Magufuli: “Sekta ya benki kwa mfano, Dk. Kimei (Charles), anafahamu tunazo benki kubwa karibu 54 na zote zinafanya biashara na Serikali, lakini zote hizi hazijakita chini kwenda kwa wananchi. Juzi hapa tumejaribu kufanya uchambuzi tukakuta karibu Sh bilioni 550 zinazozunguka katika benki hizi ni fedha za umma ambazo kiukweli ni fedha za Serikali zinazotokana na mfumo wa hati fungani. Kwa hiyo kwa maana nyingine Serikali inafanya biashara na mabenki haya kwa kutumia fedha zake yenyewe”.
Miaka michache iliyopita mfanyakazi mmoja wa Benki Kuu aliwahi kuniambia kwa sababu baada ya kubinafsisha mabenki hela zote za mishahara ya wafanyakazi wa Serikali, na wafanyakazi wa Serikali wako nchi nzima, zinawekwa kwenye mabenki ya watu binafsi. Mishahara inalipwa mwisho wa mwezi, sasa katika kipindi hiki cha mwezi mmoja mabenki wanatumia hela hizo kununua treasury bond na kupata riba. Hela hizo hizo za Serikali. Ndiyo mabenki. Mabenki haya ndiyo katika hesabu zao wanaonyesha wana deposit kubwa sana. Hela zimewekwa. Visenti vyetu, lakini Watanzania hawakopesheki. Hawapati mikopo. Hela hizo zinaenda wapi? Tunasema nchi hii ni maskini, mimi nimerudia rudia sana kusema hilo kama nchi ni maskini hayo mabenki yooote hayo wanafanya nini hapa? Hela zinatoka wapi?
Kwa hiyo sekta ya fedha kwenye mabenki, pia kuna bima. Bima siku hizi ulimwenguni ni taasisi kubwa sana ya kulimbikiza mtaji. Alitaka kumaanisha kuwa kuna kitu ambacho hakiko sawa, ingawa katika mawazo yake bado anafikiria. Katika kutoa mfano huu, nafikiri anaonyesha kwamba sekta yetu ya fedha kuna walakini. Inatubidi tufikirie upya. Na mimi ningeongeza, siyo mabenki tu- kama nilivyosema taasisi nyingine za fedha kama bima, akiba za uzeeni – taasisi hizi zinalimbikiza mtaji mkubwa sana, na ungetusaidia sana. Kama tungeweza kutumia mtaji huu tungewekeza mfano kwenye viwanda, kwenye kilimo, lakini sasa huwezi ukafanya hivyo kama hudhibiti haya mabenki na bima kama umeweka dhana ya soko huria ndani ya mikono ya watu binafsi.
Akiba za uzeeni zinalimbikia hela nyingi sana, lakini kama sasa hatuna mpango wa uwekezaji wa dhati kabisa, hasa katika uzalishaji, mtaji huo unaondoka tu au unawekwa kwenye sekta ambazo hazizalishi ajira wala haziendelezi uchumi.
Mimi ningesema kwamba ukitaka kujenga uchumi wa kitaifa bila shaka jambo la kwanza kabisa huwezi ukaachia uchumi wako katika soko huria moja kwa moja. Lazima uwe na mpango kuelekeza uchumi ule kwenye uchumi wa kitaifa. Kwa hivyo kuna sekta muhimu na nyeti tatu ambazo lazima uzidhibiti au kwa kuzimiliki na Serikali moja kwa moja, au kudhibiti kwa karibu sana.
Sekta ya kwanza ni sekta ya fedha kwa sababu ukitaka kujenga uchumi wa kitaifa lazima udhibiti sera ya kifedha. Kwa hiyo sekta ya fedha huwezi ukawaachia watu binafsi ama shirika binafsi. Sekta nyeti sana. Hii ni moja.
Sekta nyingine nyeti lazima iwe mikononi mwa Serikali ni nishati- umeme, maji, rasilimali, mapori. Sekta ya nishati lazima iwe mikononi mwa Serikali. Huwezi kuachia watu binafsi.
Sekta ya tatu ni ardhi. Rasilimali zote zinazopatikana chini ya ardhi na juu ya ardhi. Huwezi ukaachia watu binafsi. Kwa hiyo sekta hizo nyeti unazidhibiti kwa karibu sana, au moja kwa moja zinakuwa mikononi mwa Serikali.
Sasa ndiyo unawaachia mabepari wa ndani kuwekeza kwenye viwanda kwa mfano. Na hapa kuna viwanda ambavyo ni vikubwa sana kwamba Serikali inaweza ikashiriki, viwanda vya hali ya kati na viwanda vya hali ya chini. Hao unawawekea mazingira mazuri ili wawekeze, wakidhi soko la ndani, watumie malighafi ya ndani –matunda, pamba.
Hotuba yake inaelekea kukidhi mahitaji hayo, lakini kama nilivyosema sina uhakika kwa sababu hotuba hiyo ilikuwa ni hotuba ya kwanza kabisa, lakini jinsi alivyokuwa anazungumza, yale aliyogusia kwa upande wangu kama mchambuzi ninavyoona hii ni kana kwamba ana dhamira ya kujenga uchumi wa kitaifa. Kwa sababu haya unayozungumzia hayawezekani kama huna lengo hili na hukidhi masharti yake.
Kwa mfano, ukijengea mazingira tabaka lako la ndani, la kitaifa; kuna mambo mawili kutoka juu. Moja, walipe kodi, hili amezungumzia sana. Ya pili, wawekeze kwa malengo yanayowekwa na Serikali. Unapokuja serikalini kuomba kibali kutakuwa na vigezo. Je, utatumia malighafi ya ndani? Je, utatoa bidhaa ambayo ni mahitaji ya watu walio wengi nchini? Je, utatumia mitambo ambayo itaongeza ajira? Ingawa Serikali haimiliki kiwanda, lakini Serikali ina vigezo kabla ya kumruhusu huyu aende kuwekeza, na siyo jambo geni. Ndivyo walivyofanya nchi za South Korea na Thailand- ndivyo walivyokuwa wanafanya. Wanakuwa na mpango kabisa ingawa uchumi siyo mikononi mwa Serikali, lakini wana mpango. Haya ni masharti mawili kutoka juu.
Masharti mengine ni kutoka chini kwamba uwe na vyama huru vya wafanyakazi ili hawa mabepari wa ndani kwa kisingizio cha uwekezaji wasije wakanyonya wafanyakazi kupita kiasi. Wanadhibitiwa kutoka chini kutokana na vyama vya wafanyakazi. Haya ni masharti ninavyoona mimi kama unadhamiria kujenga uchumi wa kitaifa.
Hii la kodi ni muhimu kwa sababu suala la kodi ni Serikali kuweza kukusanya mapato yake na mapato haya kutumika kutoa huduma kwa jamii. Huwezi ukajenga uchumi imara kama huna watu wenye afya imara, wenye elimu- huwezi. Kulikuwa na wakati ambao sekta kama elimu na afya na maji zilichukuliwa kama sekta za huduma, siyo za uzalishaji, lakini sasa dhana imebadilika kabisa.
Dhana ya kimaendeleo ni kwamba elimu, afya, maji safi hizo siyo sekta za huduma, ni sekta za uzalishaji kwa sababu wazalishaji ni nani? Wazalishaji ni wananchi wenyewe. Kama hukuwekeza kwa wazalishaji hao huwezi ukaendeleza uchumi wako. Ni muhimu hiyo. Kwa hiyo dhana ni tofauti kabisa sasa. Unavyowekeza kwenye elimu, unapowekeza kwenye afya na hii ni jukumu la Serikali, siyo mambo ya kuachia soko huria. Huwezi ukaachia soko huria. Kwa kweli unawekeza kwenye uchumi wako. Unafanya uchumi wao uwe endelevu, hii ni muhimu sana na katika hili inahitaji mapato.
Hotuba zake (Rais Magufuli) amezungumzia, na hii amesimamia sana kwamba ‘sitakubali kwamba wafanyabiashara wanakwepa kodi’, sawa, sasa swali litakuja je, baada ya kukusanya kodi una mpango-jinsi ya kutumia hiyo kodi na kuhakikisha kwamba watendaji wako wanawajibika kutoa zile huduma zinazohitajika kwa wananchi, na wananchi wa hali ya chini? Ni muhimu sana hiyo.
Katika siku 50 huwezi ukasema, lakini hapa na pale kuna dalili, lakini huwezi ukasema katika siku 50 na huwezi ukafanya mambo hayo…kama nilivyosema ilikuwa muhimu pale mwanzoni lazima ujenge mfumo uwe na dira kabisa kwamba unataka kuelekea wapi. Hufanyi maamuzi yanayogongana. Maamuzi yote yanalenga kwenye kujenga uchumi wa kitaifa, kwa hiyo hata pale unapowekeza kwenye huduma ni kwa dhamira, nia, lengo la kuwekeza kwenye hali ya watu wako ili uweze kujenga uchumi unaotaka.
Mambo mengine haya sana siyo suala la maadili ya mtu. Tumezoea sana kuzungumza maadili, maadili, maadili. Mara nyingine tunapotosha watu. Hakuna mtu anazaliwa ana maadili. Maadili yanatokana na mfumo uliopo. Wakati wa Mwalimu tulikuwa na Miiko ya Viongozi. Miiko ile haikubuniwa tu. Haikuelea juu juu tu. Ilikuwa na mizizi yake katika mfumo wenyewe. Wewe kiongozi, wewe unaongoza ujenzi wa nchi ya Kijamaa. Sasa wewe kama kiongozi unajenga nchi ya kijamaa huwezi ukahubiri ujamaa wakati wewe siyo mjamaa. Wakati wewe unapora mali ya wananchi-huwezi ukawa mjamaa. Kwa hiyo chagua-kama unataka kuwa kiongozi wa jamii na unataka kujenga ujamaa lazima ukidhi miiko ile; kama hutaki sawa. Uko huru.
Ndiyo ilikuwa maana ya miiko. Kwa hiyo halikuwa suala la maadili. Ulikuwa unabanwa-chagua sifa zilizopo. Sasa leo hatuna miiko. Tunazungumzia maadili, maadili yatatoka wapi? Wewe kama kiongozi wa Serikali katika mfumo tulionao, mfumo wa kibepari, tena ubepari wenyewe siyo ubepari imara; ubepari uchwara wewe utafundisha nini watoto wako. Utawaambia kwamba wasitafute biashara, wasichume faida, utawaambia? Watakusikiliza kweli? Hawawezi. Sasa mfumo wenyewe ni tofauti. Kwa siku 50 huwezi ukaona, lakini kama amedhamiria itambidi huko mbele ya safari awambie viongozi wake ‘chagua moja’.
Na tusijiingize, kwa maoni yangu, inawezekana mimi nimekosea, kwa maoni yangu tusiingize kwenye mdajala wa mgongano wa maslahi. Wewe ulikuwa waziri, ulikuwa na biashara yako, lakini uweke kwenye trust-hapana. Chagua moja, ama uwe mfanyabiashara au uwe kiongozi. Hapo suala siyo mgongano wa maslahi. Kama kiongozi anakimbia uongozi kwa sababu hawezi kufanya biashara yake, basi hatumhitaji kiongozi huyo.
Kuna mambo mawili ningependa kusema. Moja ni kuhusu Bandari. Kwa kweli tumejaliwa na nafasi kijiografia nzuri sana. Tumezingirwa na nchi kama nane hivi. Tungeweza kutumia bandari yetu kwa kweli kukusanya na kulimbikiza mtaji mkubwa sana. Tungekuwa tunapata mapato makubwa sana. Tungeweza kutumia mapato haya kuwekeza, kuendeleza sekta nyingine.
Bahati mbaya mapato yote ya bandari yamepotea mifukoni mwa watu. Hatujaweza kutumia bandari zetu vizuri. Leo tuna tatizo la usafiri nchini, sawa tunajenga barabara, lakini nchi kubwa kama Tanzania haiwezi ikategemea barabara na magari tu. Kipaumbele ilikuwa kwenye kujenga njia za treni- reli ndiyo ingekuwa hasa njia yetu ya kusafiri. Reli na maji-meli. Ingekuwa kipaumbele, lakini hata ile reli tuliyorithi tumeharibu kabisa. TAZARA pia.
Umeniuliza kama Bunge limefanya kazi yake. Katika mfumo tulio nao wa vyama vingi na upinzani, ningesema kwa dhati kabisa hakuna chama hata kimoja ambacho kina programu au dira. Hayo ndiyo ninayozungumzia mimi.
Ni mara ya kwanza baada ya miaka 30; karibu miongo mitatu tunampata Rais, tunampata kiongozi angalau anaonyesha mwelekeo wa kujenga aina ya uchumi anayotaka. Ebu nieleze katika miaka hii 30 ulimsikia nani akizungumzia mwelekeo wake kuhusu aina ya uchumi anaotaka kujenga, aina ya nchi anayotaka kuijenga. Nani? Wapi? Hakuna.
Watu wanatumia neno ‘mfumo’ siku hizi. Mfumo wanaozungumzia hawaeleweki-eleweki. Kwangu mimi ukisema mfumo, kwanza kabisa maana yake mfumo wa uzalishaji –mfumo wa uchumi ndiyo hasa kitovu cha kila kitu. Tunataka mfumo wa uzalishaji uweje, wa aina gani. Lazima uainishe hilo.
Ndiyo maana nimesema kwamba kuweza kuangalia hizi kashfa hapa na pale, sawa lakini hatimaye lazima ujiulize swali hili kashfa zinatokana na nini? Chanzo chake ni kipi? Kwanini mtu anaweza kufanya mambo kama yale? Nini kinamruhusu afanye hivyo? Ana uhuru wa kujilimbikizia mali. Kwa hiyo unatumia cheo chako cha kisiasa kama nafasi ya kujilimbikizia mtaji. Sasa mfumo wa soko huria. Hatuna haja ya kwenda mbali mimi naona kwa kiasi fulani mambo mengine yanaelekea-elekea kama ya Sokoine (Edward). Lakini kuna haja mimi naona kwa upande wake (Rais Magufuli) kuangalia mambo kwa upana na undani zaidi. Nafikiri yeye mwenyewe anajua kwamba siyo rahisi kukabili mfumo tulionao ambao umejengeka kwa sababu unajua makundi na matabaka yanayofaidika na mfumo wanakuwa na njia zao za kuhujumu na mara nyingi sana hawahujumu wazi wazi au kwa vitendo vinavyojulikana.
Siyo kwamba wanafanya chini chini, lakini wanafanya kwa jazba kuonyesha kwamba wewe ni zaidi kuliko yule. Katika hili sasa unadhalilisha kiongozi wako. Unamdhalilisha. Hiyo ni njia mojawapo ya kumhujumu mtu ili aonekane ni upuuzi tu. Hao pia wanakuhujumu. Yule ambaye anajipendekeza kwa kukuiga, lakini kwenda mbali zaidi.
Thomas Sankara (Rais wa Burka Faso) alikuwa kijana, alikuwa na dhamira, alikuwa na mwelekeo. Alikuwa anaelewa anachotaka. Ni muhimu sana, lakini pia kama kuna kitu cha kujifunza kutoka kwa Thomas Sankara aliuliwa na nani – mwenzake mwenyewe waliyefanya mapinduzi pamoja. Wale waliomuunga mkono katika mapinduzi hawakutaka kwenda mbali kiasi chake yeye. Wakamuua.
Ndiyo maana kila mara nasema siyo kwamba hatuna viongozi katika Afrika. Tunao, lakini viongozi kama hawa lazima waelewe kitu kimoja wawe na imani kubwa sana na watu wao. Wajikite kwa watu wao, washirikishe watu wao, wasitegemee tu viongozi wenzao, au mfumo. Ndiyo maana nimesema yale aliyofanya pale mwanzoni (Rais Magufuli) tu yalikuwa na umuhimu wake. Wananchi wakiwa upande wako, siyo kwa kushangilia tu, lakini pia kushirikishwa-wao watakulinda.
Naona kuna dalili ambayo inanipa matumaini na ndiyo maana mimi nimekubali kuwa na mahojiano haya kama nilivyoeleza-kuna dalili. Hatuwezi tukawa na hakika. Dalili zipo. Sasa tuangalie zinaenda wapi, mwelekeo wake, viongozi anaochagua, jinsi anavyotatua mambo mbalimbali, lakini mimi binafsi ningependa kusema tu kwamba aweke imani kwa wananchi wake.
Pili, awasirikishe. Kwa hilo aangalie suala zima la demokrasia kwa jicho la kuwashirikisha wananchi. Hakuna siri kwa wananchi. Wananchi waambiwe. Wananchi wawe mobilized tuwe pamoja. Tunataka kujenga nchi ambayo itajali watu wa hali ya chini. Na wao washirikishwe.
Tuanze kufikiria muundo wa demokrasia utakaowashirikisha wananchi moja kwa moja, na bahati nzuri tunao. Kwa mfano, leo vijijini kuna vyombo kama mkutano mkuu wa wanakijiji, tuna serikali za kijiji. Ninavyoona mimi, kijiji ndicho kitovu cha demokrasia. Kwa hiyo tunapozungumza demokrasia tusifikirie mambo ya uchaguzi na Bunge. Tufikirie vijiji.