Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam

Waziri Ofisi ya Raisi Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amepongeza uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na kampuni ya kimataifa ya uwekezaji ya DP World katika bandari ya Dar Es Salaam na kuangalia ni namna gani Serikali itaendelea na maboresho zaidi katika bandari hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo makusanyo ya kodi kupitia Dira ya Taifa ya miaka 25 ijayo (2050).

Akiongea wakati wa ziara yake ya kikazi bandari hapo, Waziri Mkumbo amesema uwekezaji uliofanyika katika bandari ya Dar es Salaam ni mkubwa na una tija sana katika taifa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ukusanyaji wa mapato na ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma na kuvutia wafanyabiashara zaidi kutumia bandari hiyo.

Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo (kulia) akipewa maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA ) Bw. Plasduce Mbossa (wapili kushoto) juu ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika bandari ya Dar es salaam, wakwanza kushoto ni Afisa Fedha Mkuu wa kampuni ya DP WORLD Dar es Salaam Bw. Mathew Cliff na wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus Abed wakisikiliza kwa makini.

“Nikiwa kama Waziri mwenye dhamana katika sekta ya uwekezaji na mipango, nimeamua kuitembelea bandari ya Dar es Salaam ili kujionea utendaji wake kazi kupitia uwekezaji mkubwa uliofanyika,”

“Kiukweli nimefurahishwa sana na maboresho ya kimiundombinu na kiutendaji yaliyofanyika na haya ni matunda ya uwekezaji huu,”

“Naipongeza sana menejimenti na uongozi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kwa usimamizi mzuri na mipango mbalimbali inayoendelea katika upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine ili kukuza uchumi wa nchi,” amesema Waziri Mkumbo.

Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo (wakwanza kulia) akipewa maelezo kutoka kwa Afisa Fedha Mkuu wa kampuni ya DP WORLD Bw. Mathew Cliff juu ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika bandari ya Dar es Salaam. Wengine pichani wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA ) Bw. Plasduce Mbossa pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus Abed (wapili kulia).

Amesema kupitia mipango ya Dira ya Taifa , Serikali inapenda kuona ni namna gani uwekezaji huu utazidi kuwa na tija katika miaka 25 ijayo kupitia mipango na mikakati mbalimbali ambayo Serikali imeipanga.

Amesema maboresho yanayoendelea kufanyika katika bandari hiyo kupitia uwekezaji uliofanyika yanachochea uwekezaji katika sekta mbalimbali hapa nchini kama vile sekta ya viwanda mbalimbali, sekta ya kilimo na sekta ya elimu, ambazo zote zitasaidia kuleta tija kwa nchi ikiwemo kutoa ajira na kukuza uchumi wa taifa.

“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu uwekezaji huu mkubwa na wa kihistoria kwa nchi yetu, kwani hivi sasa tumeanza kuona matunda yake” alisema Mkumbo.

Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo (kulia) akipewa maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA ) Bw. Plasduce Mbossa (kushoto) juu ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika bandari ya Dar es Salaam, katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus Abed.

Katika ziara hiyo Mkumbo alibainisha namna uwekezaji huo utakavyoweza kukuza uchumi hasa katika mipango ya nchi ya muda mfupi na mipango ya muda mrefu na kuona kuwa yana tija kwa pande zote mbili, akimaanisha upande wa serikali na upande wa muwekezaji.

Kampuni ya kimataifa ya DP World imepewa dhamana ya kuwekeza kwenye gati namba 4 mpaka 7, hivyo kupelekea kuongezeka kwa mapato baada ya maboresho mbalimbali ikiwemo meli kuweka gati na kupakua mizigo kwa muda mfupi sana tofauti na ilivyokuwa zamani.