Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amezindua bodi mpya ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ambapo ameitaka kusimamia kwa umakini ufadhili wa masomo ya elimu ya juu ya teknolojia ya nyuklia ‘Samia Scholarship Extended Program’.
Akizungumza wakati akizindua bodi hiyo leo Februari 19, jijini Dar es Salaam, Profesa Mkenda ameisisitiza TAEC kuzidi kutenga fedha kwa ajili ya ufadhili huo ambao huwawezesha watanzania kusoma nje ya nchi fani mbalimbali zinazohusu mambo ya Atomu na nguvu za nyuklia.
“Tunawapongeza kwa kutenga bajeti, hivyo naomba hili jambo liendelee na mlisimamie. Niwashauri kuimarisha uhusiano wenu na vyuo vikuu vinavyojihusisha na masuala ya sayansi hasa katika utafiti ili kuweza kupata wanafunzi bora watakaopata ufadhili.

“Tunawapa Mamlaka ya kuchagua na kuwapeleka kulingana na miongozo iliyopo na kipaumbele cha kwanza ni watumishi wa ndani ya tume, vyuo vyetu vikuu kama kule hamna tuangalie mtanzania yeyote mwenye pasipoti na tumpeleke akasome,” amesema Profesa Mkenda.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya TAEC, Profesa Joseph Msambichaka amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua aendelee kushikilia jukumu hilo na kuahidi kutekeleza kama inavyotakiwa.
“Hii ni heshima kubwa sana kwangu na naahidi nitatekeleza majukumu yangu kadri nitakavyoweza,” amesema Profesa Msambichaka.
Amesema katika kipindi chote atakachoendelea kushika nafasi hiyo atatoa ushirikiano kuhakikisha Taasisi hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Najat Mohammed TAEC inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kudhibiti na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini kwa mujibu wa Sheria.
“Ili kuhakikisha bodi inatekeleza majukumu yake, kwa kushirikiana na Uongozi Institute tumeandaa mafunzo maalum kwa wajumbe wa bodi ambayo yameanza Februari 17 hadi 20, mwaka huu,” amesema Profesa Najat.
