Kampuni kadhaa za uwakala wa utalii zinazotoa huduma kwa watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), zinatuhumiwa kuunda mtandao wa kuhujumu mapato ya hifadhi hiyo.

Kampuni hizo zinashirikiana na watumishi wasio waaminifu wa hifadhi hiyo, kuingiza wageni kwa kutumia ‘njia za panya’ bila nyaraka.

Hayo yamefichuliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alipokutana na wadau hao wa utalii mjini Moshi, wiki iliyopita.

Wadau hao ni wamiliki wa kampuni za uwakala wa utalii, viongozi wa vyama vya wapagazi na waongoza wageni.

Anasema zipo njia za panya zinazotumiwa na kampuni hizo kupeleka watalii mlimani, na kwamba hujuma hiyo inafanikishwa kwa msaada wa watumishi wa KINAPA, wakiwamo askari wa zamu kwenye milango (gates).

 Anasema hujuma hizo zimechangia kushusha mapato kutokana na idadi ya wageni wanaopanda mlima huo kushuka kutoka 50,000 hadi 45,000 kwa sasa.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Waziri Maghembe ametangaza mabadiliko ya watumishi wa hifadhi hiyo kwa kumwondoa Mhifadhi wake Mkuu, Erastus Lufugulo, na kumrejesha Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Nafasi yake imezibwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA), Betrita Loibooki.

Mhifadhi anayehusika na Idara ya Utalii, Eva Mallya, naye amepelekwa Hifadhi ya Taifa ya Manyara.

Waziri Maghembe ameagiza ufanyike ukaguzi wa nyaraka kwa kila kampuni inayopeleka watalii KINAPA, kwa lengo la kujiridhisha endapo malipo yaliyotolewa yanaendana na idadi halisi ya wageni. Ametaka ukaguzi huo uanzie kwenye milango na ndani ya hifadhi.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa mwaka juzi mapato ya KINAPA yenye uwezo wa kujiendesha yenyewe kutokana na kuongoza kwa mapato, yalishuka kwa Sh bilioni 1.5. Sababu kuu ya kushuka kwa mapato inaelezwa kuwa ni hujuma.

Mbinu zinazotumiwa kuhujumu mapato ya hifadhi hiyo ni pamoja na mawakala kulipia wageni wachache kuliko idadi halisi ya wageni, huku baadhi ya malipo ya wageni yakiingia mifukoni mwa watumishi kadhaa wasio waaminifu.

Kwa mbinu hiyo, watumishi hutoa nyaraka feki kwa mawakala wa utalii ambao huzitumia wakati wa kuwapandisha mlimani wageni wao kwa kuonesha kwenye vituo vyenye askari na maofisa wa KINAPA.

Mbinu nyingine inayotumiwa na mawakala hao ni kulipia siku chache za wageni kupanda Mlima Kilimanjaro, lakini wanapofika ndani ya hifadhi, huwahonga walinzi na maofisa wa zamu na kukaa siku zaidi ya walizolipia.

 

VIFO VYA WAPAGAZI 

Waziri Maghembe ameshtushwa na iadi ya vifo vya wapagazi (wagumu), na sababu kuu inayotolewa ni kwamba hawana mavazi yanayoweza kuwasaidia kuhimili baridi.

Kwa kukosa mavazi rasmi, wengi hulazimika kunywa pombe (viroba) kama njia ya kujikinga na baridi. Wapagazi 18 wamekufa katika kipindi cha miaka sita. Wapagazi sita kati ya hao walifariki mwishoni mwa mwaka jana.

Waziri Maghembe ameziagiza kampuni zinazotoa huduma kwa watalii ndani ya KINAPA kubeba jukumu la kuwapa mavazi yanastahili ili wahimili baridi.

Amesema kuanzia Machi mosi, mwaka huu ni marufuku mpagazi yeyote kupanda mlima bila kuwa na mavazi rasmi. Ameuagiza uongozi wa KINAPA kufanya ukaguzi kuanzia kwenye milango.

Kuhusu malalamiko ya wapagazi kupunjwa malipo, Waziri Maghembe ameagiza kuwa kuanzia sasa wenye kampuni lazima wawalipe vizuri wagapazi, waongozaji watalii na wapishi kulingana na viwango vilivyoidhinishwa na Bunge na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

Kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (GN) Namba 228 la mwaka 2008, Bunge liliidhinisha malipo ya dola 20 kwa siku kwa mwongoza watalii, dola 15 kwa siku kwa mpishi na dola 10 kwa siku kwa mpagazi.

Hata hivyo, Chama cha Waongozaji Watalii kimelalamika kuwa tangu GN hiyo itolewe, kampuni zaidi ya 700 za uwakala wa utalii zimekuwa hazilipi viwango hivyo.

Akiwasilisha malalamiko ya waongoza watalii na wapagazi kwa Waziri Maghembe, Katibu wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TTGA) Mkoa wa Kilimanjaro, James Mong’ateko, amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba kupatiwa mikataba ya ajira bila mafanikio.

Amesema vikao vingi vya kulipatia ufumbuzi tatizo hilo vimefanyika bila kutoa suluhu, na akazishutumu baadhi ya kampuni za uwakala kwa kushirikiana na watumishi wa Serikali kukwamisha mpango huo.

HUDUMA DUNI ZA CHAKULA

Waziri Maghembe pia ameagiza kampuni za uwakala wa utalii kuwahudumia vizuri wageni wanaopanda Mlima Kilimanjaro, na kusisitiza kuwa huduma hizo zilingane na thamani ya fedha wanazolipa. Anasema yapo malalamiko kwa baadhi ya wageni ya kupewa huduma duni pamoja na hali ya uchafu ndani ya KINAPA. Ameagiza uwepo mpango maalumu wa kufanya usafi kwenye hifadhi hiyo inayoongoza kwa mapato.

Ametoa muda wa hadi Mei, mwaka huu, kwa kampuni zote zinazotoa huduma kwa watalii KINAPA kurekebisha kasoro zote za huduma kwa wageni hao.

Waziri Meghembe amekwenda mbali zaidi kwa kutishia kuruhusu biashara ya ushindani kwa kampuni za nje kufanya biashara ya utalii hapa nchini, kama wazawa hawatajirekebisha haraka.