Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Ikiwa ni siku chache zimepita tangu aliyekuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt Faustine Ndugulile afariki dunia, jana Desemba 10, 2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza kumpendekeza Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi kugombea nafasi hiyo.
Rais Samia ambaye amemteua Profesa Janabi kuwa mshauri wa Rais wa masuala ya tiba na afya, ametoa taarifa hiyo katika hafla ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua iliyofanyika jana katika Ikulu ya Zanzibar.
Kwa sasa Profesa Janabi anashikilia nyadhifa za mshauri wa Rais, masuala ya tiba na afya, mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili pamoja na mteule wa Rais kuiwakilisha Tanzania katika kinyang’anyiro cha Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.
Jina lake kamili ni Mohamed Yakub Janabi, ana uwezo wa kuzungumza lugha nne ambazo ni Kiswahili, Kiingereza, Kijapan na Kirusi.
Alipata shahada ya kwanza ya udaktari wa binadamu mwaka (1989 ) katika Chuo cha Kharkov Medical Institute kilichopo nchini Ukraine.
Mwaka 1994, alipata Masters ya Tropical Medicine kutoka Chuo Kikuu cha Queensland, nchini Australia.
Profesa janabi ana PhD ya Cardiology (magonjwa ya moyo) na Postdoctoral Fellowship ya Cardiology aliyoipata nchini Japan katika chuo kikuu cha Osaka.
Baada ya kuhitimu masomo yake, Profesa Janabi amehudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo mtafiti mkuu wa majaribio ya chanjo ya VVU (HIV Trial vaccine), daktari bingwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Country Director wa Madaktari Afrika.
Amekua Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) tangu mwaka 2014 mpaka mwaka 2022, kisha akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) tangu Oktoba 2022 mpaka sasa na juzi ameteuliwa kama mshauri wa Raisi katika masuala ya afya.
Aidha Profesa Janabi ni daktari binafsi wa Rais Mstaafu wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuanzia 2005 mpaka sasa.
Profesa Janabi ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo tangu mwaka 2003 mpaka sasa, ni Mwenyekiti wa bodi ya THPS tangu 2022, mjumbe wa bodi ya chuo kikuu cha afya Muhimbili tangu 2022, Mjumbe wa bodi ya JKCI tangu 2022, mjumbe wa bodi SUA tangu mwaka 2016, mlezi wa Taasisi ya lishe na kisukari Tanzania, mjumbe wa baraza la madaktari Tanzania, mjumbe wa TPHA, mjumbe wa Royal society of tropical medicine and hygiene, mjumbe wa Japanese society of vascular medicine, mjumbe wa American Heart Association na Mjumbe wa Japanese society of echocardiography.
Katika kuitumikia sekta ya afya, Profesa Janabi amepata tuzo za heshima kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na chuo cha American College of Cardiology (FACC).
Pia ni mwanachama wa Kudumu wa Medical University of South Carolina, Marekani.
Profesa Janabi ameanzisha na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na mashirika makubwa kama Mending Kids (USA), Open Heart International (Australia), Save the Child’s Heart (Israel), Sharjah Children’s Charity (UAE).