Na Fresha Kinasa,JamhuriMedia,Musoma
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara,Prof.Sospeter Muhongo ameendelea na zoezi la kampeni la kutoa elimu na hamasa kwa wananchi wa Kisiwani cha Rukuba ili washiriki kwa ufanisi kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, mwaka huu.
Prof.Muhongo ameambatana na Diwani wa Kata ya Etaro, Mhe Emmanuel Kigwa. Ambapo Kisiwa cha Rukuba ni moja ya vijiji vinne vya Kata ya Etaro katika Wilaya ya Musoma.
Huo ni mwendelezo wa ziara ya kitongoji kwa kitongoji, nyumba baada ya nyumba, kijiji baada ya kijiji na kata baada ya kata ambayo aliianza muda mrefu kuhamasisha wananchi kushiriki sensa ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya jimbo hilo na wananchi kwa ujumla.
Wananchi wa Rukuba, wamemhakikishia Mheshimwa Mbunge Prof.Muhongo watashiriki kwa asilimia 100 katika Sensa ya Watu na Wakazi kwani wamepata elimu kwa kina juu ya umuhimu wa sensa katika kuifanya Serikali ipate takwimu sahihi iweze kuendelea kutekeleza Mipango yake kwa ufanisi ya kuwaletea Maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Kabla ya kufanya Mkutano wa Uhamasishaji wa ushiriki kwenye sensa ambayo itafanyika Agosti 23, 2022, Mbunge huyo alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kisiwa hicho.
Ambapo Serikali imeishatoa jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho kitawahudumia wananchi. Na kwamba, ujenzi unaendelea vizuri na majengo yaliyokamilishwa kwa zaidi ya asilimia 80 ni maabara na Wodi ya Mama na Mtoto.
Aidha, Wana-Rukuba wamedhamiria kukamilisha ujenzi wa Kituo chao cha Afya ifikapo mwishoni mwa Oktoba 2022.
Wananchi hao, wametoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mheshimiwa Mbunge Prof. Muhongo kwa kuendelea kuwaletea maendeleo chini ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha mapinduzi.
Jafari Kibasa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Rukuba ambapo amesema kuwa ujenzi wa Kituo hicho utaimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wa kijiji hicho kupata matibabu kwa ufanisi.
“Tunamshukuru Mheshimwa Rais Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi za kutuletea kituo hiki cha afya kitatupa uhakika wa huduma za matibabu na kuondokana na Changamoto za kufuata matibabu mbali Mungu azidi kumbariki Mheshimiwa Rais na kumpa maisha marefu kwa Jambo hili jema,” amesema Naomy Peter.
Hussein Nalinga ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Rukuba ambapo amesema kuwa, ujenzi wa Kituo hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa kina mama wanaojifungua kwani kwa sasa wakati mwingine hulazimika kutumia boti kuwapeleka Musoma kujifungua na wakati ziwa linapokuwa limechafuka inakuwa ni changamoto kubwa.