Na: Hughes Dugilo, JamhuriMedia, Kibaha
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Raisi, Mipango na Uwekezaji, Professa Kitila Mkumbo, ameagiza Bodi zinazowakilisha Serikali kwenye mashirika zenye hisa chache kusimamia kwa ukamilifu mashirika hayo kwa maslahi mapana ya taifa.
Prof. Mkumbo ametoa maelekezo hayo Machi 15,2024 Kibaha mkoani Pwani, alipokuwa akifunga kikao kazi cha siku tatu, kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na wajumbe wa Bodi na wakurugenzi wa Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 50.
Amesema kuwa yapo mambo ambayo serikali inawataka viongozi hao kuhakikisha wanayasimamia ili kuleta tija kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
Waziri huyo alieleza kuwa moja ya mambo ambayo Serikali inatamani kuona yanafanyika kwa kampuni hizo, ni kuona zinawekeza nchini kwani zipo hapahapa.
“Mna nafasi ya kuhakikisha kwamba Makampuni haya yanawekeza Tanzania na kuendana na mazingira ya hapa nchini.
“Utakuta mampuni kubwa Kllutoka nje imewekeza nchini, lakini mazingira yao na namna wanavyoendesha Kampuni kama wapo kwao” amesema Prof. Mkumbo.
Amewataka viongozi hao kuwa na tabia njema na kuona ujuzi na mbinu ambazo zinazotumika kuhakikisha Kampuni zao zinafanikiwa.
Professa Mkumbo amewataka viongozi hao kutoa mrejesho kwa Serikali ambayo wanaiwakilisha kwa tutoka taarifa za mambo mbalimbali katika makampuni yao.
“Serikali imeamua kuijenga na kuikuza Sekta binafsi katika nchi yetu ili itusaidie, na ukiangalia makampuni mnayofanyia kazi mengi ni Sekta Binafsi, hivyo kusimamia na kufanya kazi kwa weledi ili kuisaidia Serikali kufikia malengo yake” amesema Prof. Mkumbo.
Ofisi ya Msajili wa Hazina iliwaketisha pamoja wajumbe wa Bodi na wakurugenzi wa Mashirika ambayo Serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 50 katika kikao kazi cha siku tatu, Kibaha, Pwani kwa lengo la kuzungumza nao na kuwakumbusha matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kusimamia masilahi ya Taifa.