Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ametoa wito kwa watanzania kupenda kuandika kwa kuwa kinachoandikwa kinatoa funzo kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa Kitabu On my father’s wings kilichoandikwa na Mfanyabiashara na muasisi wa Shirika la Ndege la Precision Air Michael Shirima.
Amesema mambo mengi yaliyoandikwa kwenye kitabu hicho ni funzo na kwamba maktaba zinahitaji kuwa na vitabu kama hivi ili vijana waweze kujifunza.
“Kitabu hiki nitajitahidi kukiingiza kwenye maktaba za shule vijana wasome waelewe wajifunze, waende polepole wasidhani unaweza kushinda kwa siku moja inahitaji juhudi,”amesisitiza Prof. Mkenda
Amesema tunahitaji vitabu vingi vya aina hii vilivyoandikwa vyenye maudhui yanayochochea masuala ya maendeleo akitolea mfano vilivyoandikwa na Hayati Rais Benjamini Mkapa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi na hivi sasa Mhe Jakaya Kikwete anaandika cha kwake.
“Ninakupongeza kwa kuandika kitabu hiki kinatoa ari na ujasiri wa mtu kufikia malengo pamoja na kuwa wapo wengi walishaanza ni vizuri watu wakaendelea kuandika,” amesema.