Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es salaam

Ikiwa imesalia siku kadhaa kumaliza mwaka 2024 Chama Cha Wananchi (CUF) kimemshauri Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha uchaguzi mkuu unaoarajiwa kufanyika mwakani 2025 uwe wa uhuru na wa haki ili kuendelea kulinda na kukuza Demokrasia nchini.

Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 29,2024 Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti CUF Taifa Profesa Ibrahim Lipumba wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa tathmini ya baadhi ya mambo yaliyofanyika mwaka 2024 ikiwemo uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo amesema kuwa ulikua na dosari kubwa na kuharibu Demokrasia kwa ujumla licha ya jitihada zilizokuwa zikifanyika kuitwa na Msajili wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya pamoja na kutoa mapendekezo yao nmna gani wanahitaji siasa za kistaarabu zifanyike laki yale yote waliyokuwa wakizungumza hajafanyiwa kazi.

Hatua hiyo ya CUF imetokana na kile ilichodai kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 ulikua hauna uhuru na haki kwa wagombea wa vyama vya upinzani kutokana na Demokrasia kusiginwa na TAMISEMI iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi huo

Prof.Lipumba amesema kuwa uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na rais utakaofanyika mwishoni mwa mwaka 2025 unapaswa kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ( INEC) na sio TAMISEMI kama ilivyofanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mlmitaa ,huku akisisitiza kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anapaswa kusisitiza kuwepo kwa uhuru na haki katika uchaguzi huo.

“Tunamuomba Rais Samia asisitize kuwepo kwa uchaguzi wa uhuru nawa haki 2025, itafikia hatua wananchi uvumilivu kufikia kikomo na tutalitumbukiza Taifa letu kwenye machafuko ” amesema Prof Lipumba.

Nakuongeza kuwa “tukubali Rais Dkt.Samia ameteleza kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ,ajaribu kurekebisha mambo kwenye kwenye uchaguzi mkuu na iwepo tume huru ya Taifa ya uchaguzi ili itekeleze majukumu yake kwa uhuru nakwa haki.

Ikumbukwe kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vitongoji na Vlvijiji umefanyika Novemba 27,2024 ,na umeonekana kuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo kusambaa kwa karatasi bandia za kupigia kura,pia baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani kuenguliwa majina yao kwenye daftari la mpiga kura kwa sababu zisizo za msingi,hali ambayo imeelezwa iliipa ushindi CCM kwa asilimia zaidi ya 90, kufuatia mtokeo ya jumla yaliyotangazwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa Novemba 29,2024.

Katika hatua nyingine Profesa Lipumba ameishauri Serikali kuhakikisha inawekeza kwa tija katika sekta ya Elimu,Afya na Rasilimari watu ili kuhakikisha Taifa lina vizazi vyenye Elimu bora,Afya bora na Uchumi imara nakua na maendeleo endelevu kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo Profesa huyo wa uchumi ametumia fursa hiyo kuwatakia wananchi wote heri ya Mwaka mpya wa 2025 wenye mafanikio lukuki na kuweza Kutekeleza ipasavyo malengo yao waliyojiwekea.