Prince Rahim Al-Hussaini ametangazwa kuwa Aga Khan mpya, kiongozi wa kiroho wa mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ya Ismailia.
Atachukua nafasi hiyo kutoka kwa babake Prince Karim Aga Khan, aliyefariki Jumanne akiwa na umri wa miaka 88.
Uteuzi huo ulifanywa baada ya wasia wa Prince Karim kufichuliwa, imesema taarifa ya Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan.
Prince Rahim Al-Hussaini Aga Khan V atakuwa Imamu wa 50 wa Waislamu wa Ismailia, ambao wanasema wao ni kizazi cha moja kwa moja cha Mtume Muhammad.
Ismaili ni madhehebu ya Waislamu wa Shia ambao ni wafuasi wa Maimamu kadhaa, akiwemo Imam Ismail, aliyefariki mwaka AD765.
Idadi yao duniani kote inafika milioni 15, wapatao 500,000 wakiwa nchini Pakistani. Pia kuna idadi kubwa ya wafuasi nchini India, Afghanistan na sehemu za Afrika.
Prince Karim Aga Khan alimrithi babu yake kama Imamu wa Waislamu wa Ismailia mwaka 1957 akiwa na umri wa miaka 20.
Alikufa akiwa amezungukwa na familia huko Lisbon, Ureno, ambako ndio makao ya Maimamu wa Ismailia. Mazishi yatafanyika huko siku zijazo.
Wakati akiwa kiongozi wa kiroho wa jumuiya ya Kiislamu ya Ismailia, marehemu Aga Khan alisaidia kuundwa shirika la hisani lenye jukumu la kuendesha mamia ya hospitali, miradi ya elimu na kitamaduni, haswa katika ulimwengu unaoendelea.
Aga Khan mpya ndiye mtoto wa kwanza wa babake marehemu na mamake Begum Salimah, mwanamitindo wa zamani wa Uingereza ambaye alisilimu na kubadili jina lake kutoka Sarah Croker Poole.
Prince Rahim ana watoto wawili wa kiume kupitia ndoa yake na mwanamitindo wa zamani wa Marekani Kendra Spears.