Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Uingereza, Prince Charles, ambaye pia ni mtoto wa Malkia wa nchi hiyo, Elizabeth, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua zake za dhati za kulinda wanyamapori na kupambana na ujangili dhidi ya tembo na faru, taarifa ya Ikulu imesema.
Prince Charles amesema yuko tayari kuunga mkono juhudi za Tanzania kwa kushirikiana na mtoto wake, Prince William, aliyechagua shughuli ya kulinda wanyamapori na kupambana na ujangili duniani kama moja ya shughuli zake kuu.
Moja ya hatua ambazo Prince Charles ameamua kuchukua ni kukabiliana na soko la bidhaa kuu za ujangili duniani, na hasa pembe za tembo na faru, na kufanya kampeni kubwa duniani dhidi ya biashara hiyo haramu.
Prince Charles ametoa pongezi hizo na msimamo wake wa kuunga mkono jitihada za Tanzania, wakati alipokutana kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Viongozi hao wamekutana kwenye Jumba la Tintagel mjini Colombo, Sri Lanka, ambako amefikia wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) ambao Prince Charles ameufungua rasmi Ijumaa, Novemba 15, 2013, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mahinda Rajapaksa.
Rais Kikwete naye yuko Sri Lanka kuhudhuria Mkutano huo.
Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Kikwete ametumia muda mrefu kumwelezea Prince Charles kuhusu hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa na Serikali yake, kupambana na ujangili dhidi ya tembo na faru ikiwamo Operesheni Maalum – Operesheni Tokomeza — ambayo ilifanyika hivi karibuni kuwasaka na kukabiliana na wafanyabiashara haramu ya pembe za tembo.
Rais Kikwete amemwambia Prince Charles kuwa pamoja na kuchunguza malalamiko yaliyotolewa na makundi mbali mbali ya watu kuhusu operesheni hiyo ya kwanza, bado operesheni hiyo itaendelea kwa sababu ni muhimu kulinda wanyamapori dhidi ya majangili.
“Imefika mahali ambako tunahitaji kuchukua hatua kali. Wakati wa Uhuru wetu kulikuwepo na tembo kiasi cha 350,000 lakini ilipofika mwaka 1989 idadi hiyo ilikuwa imepungua na kubakia 55,000. Hata hivyo, baada ya operesheni maalum na kubwa, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi kufikia 110,000 kabla ya kuanza wimbi jipya la ujangili mwaka 2010. Operesheni lazima iendelee,” Rais Kikwete amemwambia Prince Charles.
“Tusaidie kufunga na kuvuruga hili soko la bidhaa za wanyamapori. Operesheni ya sasa imethibitisha kuwa mtandao wa uwindaji haramu na biashara haramu ya pembe za tembo na faru ni mkubwa na watu wengi wanahusika, lakini kinachovuruga zaidi ni kwamba lipo soko la uhakika la pembe za tembo.”
Prince Charles amemweleza Rais Kikwete kuhusu hatua ambazo anakusudia kuzichukua kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano mkubwa wa wakuu wa nchi na Serikali, Februari 13, mwakani na kufanya mkutano mwingine mkubwa na vyombo vya habari kutoka pote duniani mwakani.
“Nakusudia pia kutumia wasanii nyota mbali mbali duniani kuendesha kampeni ya kuielimisha dunia kuhusu athari za biashara hiyo haramu, kwa sababu asilimia kubwa ya mapato ya ujangili inasaidia kugharimia vikundi vya kigaidi duniani.”