Kama wahenga wetu wanavyonena katika moja ya hekima zao kwamba umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, ndivyo unavyoweza kuzielezea klabu za waandishi wa habari nchini (Press Clubs). Hizi ni klabu za waandishi wa habari zinazowaleta pamoja wanataaluma wa tasnia hiyo katika mkoa husika ili pamoja na mambo mengine mengi washikamane katika kusimamia maadili ya taaluma yao.
Vilabu hivi ambavyo viko katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Unguja na Pemba, vimekuwa mhimili mkubwa katika kuwaunganisha waandishi wa habari mikoani ili kuwapa sauti ya pamoja.
Katika mazigira ya uandishi wa habari hapa Tanzania, unaweza kusema kwa hakika kabisa kwamba klabu hizi kupitia Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (Union of Tanzania Press Clubs – UTPC) ni moja ya taasisi chache sana ambazo zimetoa mafunzo ya mbalimbali ya kunoa taaluma za waadishi wa habari hapa nchini.
Uzoefu unaonyesha kwamba siyo vyombo vingi vya habari hapa nchini vinavyotoa mafunzo ya kitaaluma kwa waandishi wao wa habari hasa wa mikoani, kwa hivyo waandishi wa habari wengi wamebaki kujitafutia namna ya kupata mafunzo ya kuboresha taaluma zao na kwenda na mahitaji ya wakati.
Katika hili la Mafunzo, Klabu hizi zimefanya kazi kubwa sana, wananchama wake wamefaidika na mafunzo mbalimbali yakiwemo ya uandishi wa habari za biashara, uandishi wa mtandao, mazingira, jinsia, makala, mahakamani, uchunguzi ambao hujikita katika mafunzo kwa vitendo.
Rais wa UTPC, Deo Nsokolo, anasema mafunzo haya hutolewa kila mwaka na kwa kila klabu ya waandishi ili kuwasaidia waandishi wa habari kuboresha ujuzi wao kwa kuwa mafunzo ya mara kwa mara ili hatimaye waweze kuutumikia vyema umma.
Anasema moja ya sababu za kuanzishwa klabu hizo ilikuwa ni kusimamia maadili ya waandishi katika mikoa husika, kwa kuwa hata kama mwandishi siyo mwanachama lakini walau kuna wanataaluma wenzake wanaweza kumwita na kumuonya au hata kuchukua hatua za ziada ikiwemo kumjulisha mhariri wake kuhusu mwenendo wa mwandishi husika usivyoendana na hadhi ya taaluma ili aweze kuchukua hatua zaidi.
Anasema suala hilo linahitaji ushirikiano wa kutosha na wa dhati kutoka kwa vyama na taasisi mbalimbali vya kitaaluma, likiwemo Jukwaa la Wahariri ili kuweza kurekebisha mienendo ya baadhi ya waandishi wanaokiuka maadili ya taaluma yao. Msingi wa hoja hii ni kwamba wakati mhariri yuko Dar es Salaam, ni vigumu kujua mienendo ya mwandishi wake aliyeko mkoani, lakini kama kukiwa na ushirikiano rasmi na makini na klabu za waandishi wa habari, mhariri anaweza kuwa na njia nyingine rasmi ya kujua hasa mwenendo na tabia za mwandishi wake. Mkurugenzi wa UPTC Abubakar Karsan, anasema katika eneo la mafunzo umoja huo umekuwa ukitoa mafunzo mbalimbali kila mwaka kwa kila klabu ya waandishi wa habari katika maeneo ambayo wanachama wanaona ni hitaji lao la msingi kwa wakati huo.
Kwa mujibu wa Karsan tangu mwaka 2003, waandishi wa habari wasiopungua 8,000 wamepewa mafunzo na UTPC. Mafunzo hayo yalihusisha uandishi wa habari za uchunguzi, uandishi wa makala, habari za afya, habari za haki za binadamu na utawala bora, habari mtandaoni, habari za walemavu, habari za biashara, namna ya kufuatilia matumizi na bajeti za serikali, habari za uchaguzi, utangazaji na mafunzo ya uongozi wa namna ya kuongoza klabu. Mafunzo haya yameboresha kwa kiasi kikubwa uandishi wa habari hapa nchi kwa kuwa yalikuwa yakitolewa kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.
Kwa upande wake Nsokolo anazungumzia manufaa zaidi ya klabu hizo, akisema zimewafanya waandishi wa habari kuwa wamoja kitu kilichowapa uwezo wa kuweza hata kujikwamua kiuchumi kupitia klabu za waandishi wa habari za mikoa.
“Ukiondoa masuala ya kitaaluma ambayo wamefaidika nayo sana na suala zima la usimamizi wa maadili, klabu hizi zimewasaidia waandishi wa habari kuwa na nguvu za kiuchumi kwa kuanzisha vyama kama Saccos kupitia umoja wao na shughuli zingine za kiuchumi ambazo zinawasadia kujiongezea kipato kama klabu na kama mtu binafsi,” anasema Nsokolo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kifoma Press Club ya mkoani Kigoma.
Aidha klabu za waandishi wa habari zimewasaidia wadau mbalimbali wa habari kuwafikia kwa urahisi waandishi wa habari kupitia umoja huo. Hili limewarahisishia wadau ambao wanahitaji wanahabari kwa sababu mbalimbali kuweza kuwafikia kupitia klabu hizo. “Mdau anaweza kuwa na malalamiko dhidi ya mwandishi fulani au ana habari badala ya kutafuta mwandishi mmoja mmoja, akifika ofisi za klabu anahudumiwa na kupatiwa msaada au hata ushauri wa jambo lake,” anasema Nsokolo.
Ukiondoa hilo, klabu hizi zimekuwa chachu ya maendeleo katika mikoa yao kwa kuwa mahali ambapo wanajua umuhimu wake na wanathamini mchango wake, zimesaidia kwa kiwango kikubwa katika kuchagia harakati za maendeleo katika mikoa husika.
Bila shaka leo ukiondoa klabu ya waandishi wa habari athari zake zinaweza zisiswe na kipimo katika mkoa husika, kwa sababu ukiondoa faida zilizotajwa hapu juu nyingi zinatumika kama vyumba vya habari kwa waandishi wa kujitegemea ili kuweza kutuma habari zao kwa vyombo yao vya habari ambavyo vingi viko Dar es Salaam, na mtu anayefahamu vyema mchango wa klabu hizi kwenye maendeleo ya tasnia ya habari na ya mwandishi wa habari mmoja mmoja, hatasita wala kupata kigugumizi kusema kwamba klabu za waandishi wa habari ni mhimili muhimu katika kustawisha taaluma ya habari nchini.